Dar es Salaam. Wakati maadhimisho ya siku ya lishe kitaifa yakitarajiwa kufanyika kesho Novemba 21, 2025 mkoani Ruvuma, Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) imesema wanafunzi wa shule za msingi wanaopata chakula cha mchana wanafanya vizuri kwenye masomo ikilinganishwa na wanaoshinda njaa.
Imewasisitiza wazazi na walezi nchini kushiriki katika michango ya lishe mashuleni ili watoto wapatiwe chakula badala ya kuwatelekeza kwa madai kuwa majukumu yote ni ya Serikali na walimu.
Maadhimisho ya siku ya lishe kitaifa yanafanyika yakiwa na kaulimbiu “Afya ni mtaji wako zingatia unachokula,” ikihimiza ulaji unaofaa kama nguzo muhimu ya jamii yenye afya njema, nguvu kazi imara na ustawi wa kiuchumi na kijamii.
Kufanyika kwa maadhimisho haya kunakumbusha umuhimu wa lishe bora katika ukuaji wa mwili na akili, kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, shinikizo la damu, moyo, kiharusi, na kudhibiti udumavu wa mwili na akili kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Katika kusherehekea maadhimisho hayo, leo Novemba 20,2025 Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Mafunzo ya Lishe TFNC, Dk Esther Nkuba akitoa elimu ya lishe katika Shule ya Msingi Ali Hassan Mwinyi Kinondoni amesema wataalamu wa lishe wanatoa elimu kwa wazazi juu ya umuhimu wa kutoa chakula kwa watoto wakati wa masomo.
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Mafunzo ya Lishe TFNC,Dk Esther Nkuba akitoa elimu ya lishe kwa wazazi wa wanafunzi wa shule ya msingi
“Tunatekeleza sera ya kitaifa, kila mzazi anatakiwa kuchangia chakula au kutoa fedha kwa mwanawe anapokwenda shule. Tunapambana na utapiamlo ngazi ya shule ya msingi kwa kuwapa wazazi na wapishi, walimu wa lishe, walimu wakuu na viongozi wa mitaa elimu ya lishe.
Utafiti unaonyesha mtoto anayepata chakula shuleni ufaulu wake wa masomo unakuwa juu sana ikilinganishwa na mwanafunzi ambaye hapati chakula shuleni,” amesema.
Dk Nkuba amesema kupitia mradi wa lishe unaotekelezwa kwa majaribio kati ya TFNC na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula (WFP), kwa shule 15 za Manispaa ya Temeke ni kumaliza utapiamlo kwa watoto, kwani mtoto akiwa mdogo ndio nafasi ya kujenga ubongo na kumbukumbu kwa kupatiwa lishe bora.
“Ili tupate watoto wenye tija ni wakati sasa wazazi kutambua jukumu lao. Mtoto anapotoka nyumbani ale chakula na asitoke tumbo likiwa tupu,” amesema.
Amesema WFP na TFNC wanahimiza lishe bora kwa wanafunzi ili watoto wanaomaliza shule wawe na tija kwa Taifa kwani ndio viongozi na wataalamu watakaokuja kujenga uchumi wa nchi, hivyo kuzalishwa kwa wataalamu wenye changamoto ya lishe si salama kwa Taifa.
Katika mradi huo wa majaribio ambao utaendelezwa baada ya matokeo yake kupatikana, amesema wamelenga kuwafikia wanafunzi 29,000.
Akizungumzia manufaa ya mafunzo ya lishe wanayopatiwa wazazi katika shule za msingi, Tumaini Amour, mzazi wa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mabatini Temeke jijini Dar es Salaam amesema wazazi wengi hawafahamu jinsi ya kuandaa mlo kamili, hivyo mafunzo wanayopata ni msaada kwao.
“Wataalamu wamekuja kutueleza ni mambo gani tunapaswa kufanya ili kuwapa watoto wetu mlo kamili. Tumefundishwa uwepo wa makundi sita ya chakula, hatukuwa tunafahamu. Sasa nimeelewa jinsi ya kumpatia mtoto wangu chakula chenye mlo kamili,” amesema.
Mwalimu mkuu wa Shule ya msingi Madenge, Khadija Hussein, amesema mradi wa lishe bora kwa shule za msingi umewarahisishia kazi.
“Baada ya kupata elimu ya lishe kwetu walimu na wapishi wa shule yetu tulianza kupeleka elimu hiyo kwa wazazi ili wachangie chakula na watoto wakaanza kupata chakula, na utoro ukapungua,” amesema.
Amesema walimu wamekuwa wakipitia wakati mgumu kuwafundisha watoto wenye njaa darasani, hivyo baada ya mradi wa lishe kuanza usikivu wa wanafunzi darasani pamoja na ufaulu umeongezeka.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Temeke kata ya Temeke, Bakir Makere amesema katika vikao vya wazazi shuleni na vya mtaa watatoa elimu ili kila mzazi achangie fedha ili mtoto apate chakula akiwa shuleni.
“Tutahamasishana wazazi katika mitaa yetu wachangie fedha ili watoto wapate chakula wakiwa shuleni kwa lengo la kusoma kwa utulivu na kupunguza utoro mashuleni na ufaulu mdogo,” amesema.
Mwenyekiti kamti ya wazazi Shule ya msingi Mabatini, Hosea Msocha akizungumza na wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo juu ya umuhimu wa lishe kwa wanafunzi
Kulingana na taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Afya, Serikali inaendelea kuhimiza wananchi kutumia vyakula kila siku vinavyopatikana katika mazingira yao hasa mbogamboga, matunda, vyakula vya asili ya wanyama na vilivyoongezwa virutubishi ili kuimarisha afya na hali ya lishe.
“Vilevile ni muhimu kupunguza vyakula vyenye mafuta, sukari na chumvi kwa wingi, pamoja na kufanya mazoezi na kuushughulisha mwili ili kudhibiti uzito wa mwili na kuzuia magonjwa yasiyoambukiza,” taarifa hiyo imeeleza.
Katika maadhimisho yanayofanyika kesho, wananchi wamehimizwa kushiriki ili kupata elimu ya lishe ya ulaji bora katika familia na kuendelea kuunga mkono juhudi za kuimarisha lishe bora kama msingi wa afya na maendeleo endelevu.
Aidha, watoa huduma katika sekta ya afya wanasisitizwa kuendelea kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora.
