Kwa nini Tanzania inapaswa kuwa makini kulinda mafanikio ya afya ya uzazi

Dar es Salaam. Wataalamu wa afya ya uzazi nchini Tanzania, wameitaka Serikali kuchukua tahadhari kubwa kabla ya kuridhia Mkataba wa Makubaliano (MOU) unaopendekezwa na Serikali ya Marekani, ambao kwa sasa unajadiliwa katika nchi kadhaa za Afrika.

Ingawa hati ya mkataba huo bado haijatolewa hadharani, taarifa kutoka kwa wataalamu wa kikanda zinaashiria unaweza kuweka masharti yanayoweza kuzuia utoaji wa taarifa na huduma muhimu za afya ya uzazi.

Makubaliano hayo ni mkakati mpana wa afya ya kimataifa ambao ni pamoja na utekelezaji wa memoranda of understanding (MoUs) na nchi kadhaa za Afrika. America First Global Health Strategy ilizinduliwa na Marekani hivi karibuni.

Mpango huu unaweka mwelekeo mpya wa usaidizi wa afya wa kimataifa, badala ya kupeleka pesa za misaada kwa Asasi za kiraia au NGO na mashirika ya kimataifa, Marekani inataka kufanya makubaliano ya moja kwa moja (bilateral) na serikali za nchi wanufaika.

Kwa mujibu wa taarifa za wataalamu wa kikanda, mkataba unaopendekezwa unaweza kuweka vizuizi katika utoaji wa taarifa za afya ya uzazi, kupunguza huduma zinazoweza kutolewa na hata kuathiri utoaji wa huduma za dharura za baada ya utoaji mimba, ambazo ni halali kisheria na ni muhimu kwa kuokoa maisha.

Katika nchi ambazo mikataba inayofanana imetekelezwa, kumekuwa na mkanganyiko kwa watoa huduma, kupungua kwa elimu ya jamii, kukoma kwa baadhi ya huduma za mkoba, na madaktari kuhofu kutoa huduma kamili kwa hofu ya kukiuka masharti ya wahisani.

Wataalamu nchini Tanzania wanaonya iwapo Serikali itasaini mkataba huo, upatikanaji wa uzazi wa mpango unaweza kupungua, na hivyo kuongeza mimba zisizotarajiwa, utoaji mimba usio salama na vifo vya kina mama, hali itakayoongeza mzigo mkubwa kwa mfumo wa afya nchini.

Akitoa maoni yake, Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Engender Health Tanzania, Dk Moke Makoma amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazopokea msaada mkubwa wa afya ya uzazi kupitia miradi ya uzazi wa mpango, lakini anaona msimamo wa sasa wa walioko madarakani upo kinyume katika sayansi na udaktari.

“Wasiwasi nchi nyingi zikikubali kichwakichwa zinaweza kupata shida, njia za kisasa bado ni muhimu. Wao kupangilia uzazi siyo kipaumbele sasa masharti yake yanaweza kupunguza utoaji wa huduma za uzazi, kuongeza vifo vya kina mama, na kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana katika upatikanaji wa uzazi wa mpango,” amesema.

Hivyo amesema ikiwa Marekani itapunguza usaidizi wake wa moja kwa moja au kuhamisha mfuko kupitia MoU, kuna hatari kuwa baadhi ya huduma za uzazi wa mpango zitapungua.

Dk Makoma amesema upatikanaji wa data ya kiafya (hata pathogens) na makubaliano ya muda mrefu ya MoU unaweza kuleta mabadiliko ya kipaumbele katika afya ya umma ambayo hayahusu tu uzazi, na kuathiri rasilimali zilizokuwa zikielekezwa kwa uzazi wa mpango.

Mwakilishi Mkazi wa UNFPA nchini Tanzania, Jacqueline Mahon amesisitiza kuwa kila dola moja inayowekezwa kwenye uzazi wa mpango inaweza kuokoa hadi dola sita katika gharama za matibabu ya dharura na athari za kijamii na kiuchumi.

Gharama za kutibu athari za utoaji mimba usio salama ni kubwa. Kila mgonjwa anahitaji kati ya dola 45 hadi 100 kulingana na kiwango cha tatizo ikiwamo maambukizi makali, kutokwa damu kupita kiasi, uharibifu wa viungo na madhara ya muda mrefu ya uzazi. Zaidi ya wanawake 66,000 hutibiwa kila mwaka kwa matatizo haya, huku maelfu wengine wakishindwa kufika hospitali kutokana na umbali, gharama au unyanyapaa.

Kwa karibu muongo mmoja, Tanzania imepiga hatua katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango, kuongeza uelewa wa jamii na kuimarisha uwezo wa vituo vya afya kutoa huduma za dharura. Hata hivyo, mafanikio haya ni dhaifu na yanahitaji uwekezaji endelevu na uhuru wa watoa huduma kutoa elimu na huduma kwa mujibu wa sheria za Tanzania.

Mtaalamu mmoja mwandamizi wa afya ya uzazi nchini aliliambia gazeti hili kuwa; “Sera yoyote itakayozuia uzazi wa mpango au huduma za baada ya kutoa mimba, itaongeza moja kwa moja vifo vya akina mama. Wanawake wa vijijini ndiyo watakaoteseka zaidi.”

Mbunge mmoja mwenye uelewa wa masuala ya afya, ambaye hakutaka kutajwa, amesema; “Lazima tuhakikishe makubaliano yoyote ya kimataifa yanaendana na vipaumbele vya Tanzania, si kuyapindua mafanikio tuliyoyapata.”

Wataalamu wanasisitiza kuwa afya ya uzazi si suala la itikadi, ni msingi wa maendeleo ya Taifa, ustawi wa jamii na heshima ya utu wa binadamu. Shirika la Afya Duniani (WHO) na Umoja wa Mataifa yanaielezea mipango ya uzazi kama moja ya uwekezaji bora zaidi katika afya ya umma.

Kwa kuzingatia wimbi kubwa la vijana nchini, upatikanaji wa taarifa sahihi na huduma rafiki za afya ya uzazi ni muhimu kwa uthabiti wa kiuchumi na kijamii wa taifa.

Wito wa wataalamu ni mmoja, Serikali lazima ihakikishe kuwa mkataba wowote kutoka nje hauathiri sheria, sera, na haki za Watanzania.

Wanashauri kuwepo kwa uwazi, ushirikishwaji mpana wa wadau na tathmini ya athari kabla ya kuchukua maamuzi.

Wanaonya kuwa kusaini mkataba wenye masharti kandamizi kutakuwa na madhara makubwa kwa Taifa, ongezeko la mimba zisizotarajiwa, vifo vya akina mama na gharama kubwa kwa mfumo wa afya.

Kwao, Tanzania inapaswa kusimama imara na kulinda mafanikio yake katika afya ya uzazi ambayo ni msingi wa ustawi wa vizazi vijavyo.

Tanzania kwa sasa inakabiliwa na changamoto sugu za afya ya uzazi, ikiwamo kiwango kikubwa cha mimba zisizotarajiwa na vifo vinavyotokana na utoaji mimba usio salama.

Takwimu zinaonyesha kuwa karibu wanawake milioni moja hupata mimba zisizotarajiwa kila mwaka, huku asilimia 40 ya mimba hizo zikimalizika kwa utoaji mimba na uaviaji mwingi ukiwa ni hatari na usiyo salama.

Aidha, kati ya asilimia 16 hadi 19 ya vifo vya akina mama nchini vinahusishwa moja kwa moja na matatizo yanayotokana na utoaji mimba usio salama.

Hii ina maana mamia ya wanawake hufariki kila mwaka kutokana na ukosefu wa huduma sahihi au taarifa sahihi za afya ya uzazi.

Kiwango kikubwa cha mimba zisizotarajiwa nchini kinachangiwa na mahitaji ya uzazi wa mpango yasiyotimizwa.

Takribani mwanamke mmoja kati ya wanne aliye kwenye ndoa anahitaji njia ya kisasa ya uzazi wa mpango lakini hawezi kupata. Kwa vijana balehe, mahitaji hayo ni makubwa zaidi kutokana na unyanyapaa, hofu ya kuhukumiwa na upatikanaji mdogo wa huduma rafiki kwa vijana.