Mbeya. Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kwa kushirikiana na wadau wengine wa zao hilo, wameandaa shindano la kutafuta kahawa bora kutoka mikoa 16 nchini inayolima zao hilo ikiwa ni kuhamasisha wakulima kuzalisha kwa ubora.
Mashindano hayo yanafanyika jijini Mbeya, yakishirikisha sampuli zaidi ya 70 ambapo majaji 15 kutoka ndani na nje ya nchi chini ya jaji mkuu Filip Bartelak kutoka nchini Poland wanaongoza shughuli hiyo ya kumpata mshindi ambaye atawakilisha Tanzania katika maonesho ya Afrika nchini Ethiopia Februari 2026 kisha kuchuana kidunia.
Akizungumza leo Alhamisi, Novemba 20, 2025, Mkurugenzi wa Ubora na masoko kutoka TCB, Frank Nyalusi amesema shindano hilo linalenga kuongeza hamasa kwa wakulima wa zao hilo aina ya Arabika na Robusta.
Amesema pamoja upatikanaji wa zao bora inasaidia Tanzania kuingia kwenye ubora wa uzalishaji na kuchochea soko la ndani na nje ya nchi, akifafanua kuwa zoezi hilo linahusu muonjo, muonekano na uzito wa kahawa.
Jaji mkuu wa shindano hilo kutoka nchini Poland Filip Bartelak (aliyevaa shati jeupe) akiwa na baadhi ya maafisa wa Bodi ya Kahawa wakati wa shindano hilo jijini Mbeya.
“Hili ni shindano ambalo mshindi anapatikana kwa haki, kwakuwa kuna majaji wanaotambulika duniani, kinachofanyika ni kuonja kila sampuli hatuna mkulima, kila Mkoa ulituma zao lake kupitia wakulima na vyama vya ushirika,” amesema.
“Zipo faida za kushiriki mashindano ikiwa ni kujitangaza kama mzalishaji wa kahawa bora kwa kuwekwa kwenye majalada ya kimataifa, lakini mshindi atashiriki mnada wa Afrika huko nchini Ethiopia na kisha duniani,” amesema Nyalusi.
Amesea kwa mwaka jana, Tanzania ilishika nafasi ya kwanza Afrika kwa Kahawa aina ya Robusta, akieleza mkakati wa TCB ni kuhakikisha Arabika nayo inafanya vyema akieleza kuwa kwa sasa uzalishaji umeongezeka kutoka tani 50,000 hadi tani 85,000 japokuwa malengo ni kufikia tani 150,000.
Kwa upande wake, jaji mkuu kutoka Tanzania, Balam Hinyola amesema jumla ya sampuli 70 zimepokelewa, ambapo kazi yao itakuwa ni kuonja na kuchagua kahawa iliyobora, wastani na zaidi kwa kutumia fomu maalumu.
Amesema kahawa bora lazima iwe na asilimia 100, akibainisha kuwa hawafahamu sampuli imetoka wapi au kwa nani, badala yake wao ni kuzipanga kwa ubora, akiwaomba washiriki kuondoa hofu uwapo wa upendeleo au uonevu.
Majaji Balam Hinyola (kushoto) kutoka Tanzania na mwenzake Bariki Mkony wakionja kahawa katika shindano lililoandaliwa na Bodi ya Kahawa nchini (TCB) kwa lengo la kumpata mshindi atakayewakilisha kimataifa.
“Huu ni mwaka wa 14 sasa nikiwa jaji wa mashindano haya, kadri muda unavyokwenda tunaona mnabadiliko chanya kwa wakulima namna ya kuzalisha kahawa bora kwakuwa huwa tunawapa mrejesho,” amesema Hinyola.
Naye Jaji mkuu kutoka nchini Poland, Filip Bartelak amesema lengo ni kuchagua kahawa bora akieleza kuwa moja ya mafanikio katika shindano hilo ni kuongeza ubora na uzalishaji wa zao hilo kwa wakulima.
“Kupitia shindano hili, inachochea wakulima kuzalisha kwa ubora na kuweka Kahawa kwenye mnyororo wa thamani kwakuwa hata bei yake hupanda, tunafurahishwa na muitikio wa wakulima kwenye kujitokeza kushirikisha sampuli,” amesema Bartelak.
