Joshua azikwa, mwanafunzi mwenzake asimulia alivyonusurika mashambulizi ya Hamas

Simanjiro. Mwanafunzi mwenzake wa Joshua Mollel aliyekuwa naye Israel amesimulia jinsi alivyonusurika na mashambulizi ya mabomu ya kikundi cha wapiganaji wa Hamas, kwa kuishi ndani ya handaki kwa siku tatu.

Ezekiel Kitiku, aliyekuwa miongoni mwa wanafunzi 260 waliokuwapo Israel, amesema anamshukuru Mungu kwa kunusurika katika tukio hilo.

Kitiku, mhitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua) mkoani Morogoro, amesema hayo leo, Novemba 20, 2025, wakati wa maziko ya Joshua Mollel mkoani Manyara, aliyeuawa na kikundi cha Hamas huko Israel miaka miwili iliyopita.

Kitiku amesema siku ya tukio alikuwa kwenye handaki lililopo ndani ya zizi la ng’ombe, ambako alikuwa akifanya kazi ya usiku, wakati Joshua na Mtenga walikuwa kwenye mashamba tofauti.

“Siku ya tukio, saa 12:20 asubuhi, mabomu yalianza kurindima. Nilitumbukia kwenye handaki na kukaa humo kwa siku tatu, nikijikimu kwa kula vipande vitatu vya yogati nilivyokuwa navyo, pamoja na maji yaliyoniwezesha kustahimili,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Jimbo la Masai Kusini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mchungaji Osupati Laizer, amewapa faraja wazazi wa marehemu Joshua Mollel, akiwahimiza wasikate tamaa kwa kuwa Mungu anaendelea kuwa pamoja nao na atawapa nguvu, faraja na hata baraka nyingine.

Mbali na kuwatia moyo, Mchungaji Laizer amewataka wazazi hao kuendelea kuwa na shukrani, akisema hata Nabii Ayubu alisimama imara katika imani yake, licha ya kupitia majaribu makubwa.

Akizungumza wakati wa maziko ya Joshua, Mchungaji Laizer amesema Mungu anapaswa kushukuriwa katika kila hali, hata kupitia tukio hilo zito.

Amesema kipindi cha zaidi ya miaka miwili ambacho familia ya marehemu Joshua imeishi bila kujua hatima yake, kilikuwa kigumu na chenye majonzi makubwa, lakini hatimaye leo wameshuhudia safari yake ya mwisho.

“Nawapeni moyo, Mungu atawapa Joshua mwingine msikate tamaa ila shukuruni kwani hata Nabii Ayubu alisimama kidete kwenye imani yake baada ya kupata masaibu,” amesema.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Simanjiro, Warda Abeid, amesema tukio hilo linapaswa kuwa funzo kwa Watanzania kwamba amani ni tunu ya thamani kubwa inayostahili kulindwa na kukumbatiwa wakati wote.

“Hivi karibuni baadhi ya Watanzania walichezea amani kwa kufanya vurugu na machafuko yasiyo na maana kwa jamii,” amesema Warda.

Ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Israel kwa kuwa karibu na familia ya Joshua kwa kipindi chote cha tukio hilo.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Saidi Shaib, ametoa pole kwa familia ya Joshua kutokana na kipindi chote kigumu walichopitia kutokana na tukio hilo.

“Poleni sana, tumehitimisha jambo hili kwa amani huku tukimtanguliza Mungu ambaye ni mpangaji wa kila jambo,” amesema.

Melkizedeki Emmanuel akitoa historia ya marehemu Joshua amesema alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Orkesumet kuanzia mwaka 2009 hadi 2014.

Mwaka 2015, alijiunga na Shule ya Sekondari Simanjiro kabla ya kuhamia Shule ya Sekondari KAC jijini Arusha, ambako alihitimu mwaka 2018.

Ameongeza kuwa Joshua alisoma kozi ya famasia  Kigamboni City College of Health and Allied Sciences mwaka 2019–2020, na baadaye, mwaka 2020, akabadilisha fani kutoka famasia kwenda uhamasishaji.

“Mwaka 2020 alianza masomo ya stashahada ya kilimo katika Chuo cha Kilombero Agricultural Training and Research mkoani Morogoro na kuhitimu mwaka 2023,” amesema.

Amesema alipata ufadhili wa Serikali kusoma kilimo kwa njia ya vitendo nchini Israel mwaka 2023 na aliondoka Tanzania Septemba 19, 2023.

“Marehemu Joshua hakuajiriwa ila alipata uzoefu katika nyanja mbalimbali kama kusimamia sensa ya watu na makazi mwaka 2022 na kuhitimu mafunzo ya viuatilifu TPRI,” amesema Emmanuel.

Amesema familia inatoa shukrani kwa Serikali ya Israeli kwa ushirikiano na kufanya jitihada za kuhakikisha mwili wa marehemu Joshua unapatikana.

 “Tunatoa shukrani kwa Serikali ya Tanzania, hususan Wizara ya Mambo ya Nje, kwa uratibu na msaada walioutoa kipindi chote, hasa Balozi wa Tanzania nchini Israeli, Alex Kallula,” amesema.