Mashahidi 26 kutoa ushahidi, kesi wizi wa mafuta mali ya TPA

Dar es Salaam. Mashahidi 26 na vielelezo 13 vinatarajiwa kutolewa mahakamani katika kesi ya wizi wa mafuta na kuharibu bomba la mafuta inayomkabili aliyekuwa dereva wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Tino Ndeketa (45) na wenzake saba.‎

‎Washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 30189 ya mwaka 2024 yenye mashtaka manne yakiwemo ya kuharibu miundombinu, kutakatisha fedha na wizi na mafuta yenye thamani ya Sh33milioni mali ya TPA.

‎Mbali na Ndeketa ambaye ni mkazi wa Tungi Kigamboni, wengine ni wafanyabiashara, Fikiri Kidevu (33), Amani Yamba (53), Mselem Abdalah (44) carpenter, Kila Sangiti (30) maarufu kama mudy mzeze, Twaha Salumu (47) maarufu Mwarabu na Hamis Hamis (49), mkazi wa Kigamboni.‎

‎Mashahidi hao wanatarajia kutoa ushahidi wao, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuruhusu Mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo.‎

‎Washtakiwa hao wamesomewa hoja za awali (PH) leo, Alhamisi Novemba 20, 2025, baada ya upelelezi wa shauri hilo kukamilika.‎

‎Wakili wa Serikali, Titus Aron amewasomea maelezo hayo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.‎

‎Wakili Aron amedai vielelezo hivyo 10 ni pamoja na magari manane, kadi za magari, maelezo ya onyo, hati ya ukamataji, ripoti kutoka TPA, ripoti ya mikataba ya nyumba, taarifa ya Ewura na TRA.‎

‎Hata hivyo, wakili Aron alidai upande wa Jamhuri unaweza kuongeza mashahidi au kupunguza, wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo.‎

‎Baada ya kueleza hayo aliwasomea upya mashtaka yao na kisha kuwasomea hoja za awali.‎

‎Baada ya maelezo hayo, Hakimu Beda alipanga kesi hiyo kuanza kusikilizwa Novemba 26, 2025 ambapo aliwataka upande wa mashtaka wanapeleka mashahidi.

‎‎Hakimu Beda baada ya kueleza hayo, washtakiwa walirudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili halina na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Awali, washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka 20, lakini baada ya upelelezi kukamilika, Jamhuri ilifanya mabadiliko ya hati ya mashtaka kwa kuondoa mashtaka 16 na kubakisha mashtaka manne.

Katika mashtaka hayo manne,  mashtaka mawili kati ya hayo ni ya uharibifu wa mali wanayodaiwa kutenda kati ya Januari Mosi, 2019 na Desemba 31, 2022 eneo la Tungi, Kigamboni, ambapo siku hiyo waliharibu  bomba la kusafirishia mafuta aina ya Petroli na Dizeli mali ya Mamlaka ya Bandari Tanzania( TPA).‎

‎Pia wanadaiwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2020 eneo la Tungi Kigamboni, waliiba lita 16, 225 za mafuta ya dizeli yenye thamani ya Sh33.9 milioni mali ya TPA.‎

‎Siku na eneo hilo hilo, washtakiwa hao wanadaiwa kutakatisha fedha kiasi cha Sh33.9 milioni, wakati wakijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la wizi.

‎‎Kwa mara ya kwanza, walipandishwa kizimbani mahakamani, Oktoba 22, 2024 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi.