Mwanza. Jumla ya watuhumiwa 19 wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana, Mwanza na kusomewa mashitaka yanayowakabili katika kesi mbili tofauti.
Washtakiwa hao ni wale waliokamatwa baada maandamano yaliyozua vurugu siku ya Uchaguzi Mkuu, Oktoba 29, 2025.
Watu hao ni sehemu ya wale 172 waliokamatwa na kufunguliwa mashtaka katika Wilaya ya Nyamagana.
Leo Alhamisi Novemba 20, 2025, kesi yao imefikishwa mahakamani kwa ajili ya kutajwa kwa mara ya pili.
Katika shauri la kwanza namba 26497/2025, washtakiwa sita wanakabiliwa na makosa ya kufanya maandamano kinyume cha sheria, kinyume na vifungu vya 74(1)(2), 76 na 35 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 (marejeo ya 2023), pamoja na shtaka la unyang’anyi wa kutumia silaha kinyume na kifungu cha 287A.
Hata hivyo, shauri hilo limeahirishwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Nyamagana, Ramla Shihagilo kwa niaba ya Hakimu Mkuu Mkazi, Fortunas Kubaja ambaye hakuwepo mahakamani hapo.
Hakimu Shihagilo amesema upelelezi bado haujakamilika, hivyo shauri hilo litatajwa tena Novemba 27, 2025, huku watuhumiwa wakiendelea kusalia rumande.
Katika kesi ya pili, watuhumiwa 13 wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kuchoma moto nyumba ya John Buzile kinyume na kifungu cha 319(a)(b) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu na unyang’anyi wa kutumia silaha.
Baadhi ya watuhumiwa wanaokabiliwa na mashtaka ya kufanya maandamano kinyume na sheria, baada ya uchaguzi mkuu, wakitoka mahakamani leo baada ya kusomewa mashtaka yao kwenye Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana, Mwanza. Picha na Damian Masyenene
Shauri hilo limesikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Clemment Tuji huku upande wa mashtaka ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Benedicto Ruguge na upande wa utetezi ukiwakilishwa na mawakili Majula Kiboga, Benson Bernad, Erick Korogo na Gibson Ishengoma.
Akiwasomea mashtaka, Wakili Ruguge amedai kuwa Oktoba 30, 2025, katika eneo la Nyegezi, watuhumiwa kwa pamoja na wengine ambao bado hawajakamatwa, walichoma moto nyumba ya Buzile na kumtishia kwa kutumia silaha mbalimbali.
Baada ya kusomewa mashtaka, upande wa utetezi uliibua mapingamizi matatu yaliyosababisha mvutano wa kisheria uliodumu kwa takriban saa mbili kuanzia saa 4:00 hadi 6:30 mchana.
Wakili Erick Korogo, akiwasilisha pingamizi la kwanza, alipinga hoja ya upande wa mashtaka kwamba upelelezi haujakamilika.
Alirejea kifungu cha 134(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, akisisitiza kuwa sheria mpya ya haki jinai inaelekeza upelelezi ukamilike kabla ya mtuhumiwa kukamatwa.
“Waliwezaje kuwakamata na kuwaleta mahakamani kabla upelelezi haujakamilika? Tunaomba waachiwe huru na upelelezi ukamilike ndipo shauri lifunguliwe,” Korogo aliiomba Mahakama.
Katika pingamizi la pili, aliiomba pia Mahakama kuondoa kwenye rekodi kipengele cha mashtaka kinachosema “pamoja na wengine ambao hawajakamatwa,” akidai kuwa hakipo kwenye hati ya mashtaka iliyopo mahakamani.
Hoja ya tatu ilihusu ombi kwa Mahakama kuiamuru Jamhuri kuikabidhi hati ya mashtaka na vielelezo muhimu ndani ya siku saba, kama sheria inavyoelekeza.
Akijibu hoja hizo, Wakili Ruguge amedai kwa mujibu wa kifungu cha 134(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, makosa makubwa kama unyang’anyi wa kutumia silaha hayahitaji upelelezi kukamilika kabla ya watuhumiwa kufikishwa mahakamani.
Aidha, amekubaliana na hoja ya utetezi kuhusu kupeana vielelezo muhimu kwa sababu ni haki ya washtakiwa.
Baada ya majibu hayo, mvutano uliendelea na kumlazimu Hakimu Tuji kuahirisha shauri kwa dakika 20 mpaka saa 7:00 mchana ili kupitia hoja za pande zote mbili.
Kesi hiyo iliendelea tena saa 7:33 mchana kwa ajili ya uamuzi mdogo.
Katika uamuzi wake, Hakimu Tuji alitupilia mbali mapingamizi yote matatu. Alibainisha kuwa upande wa mashtaka haujakosea kufungua shauri kabla ya upelelezi kukamilika, kwa mujibu wa kifungu cha 134(4).
Kuhusu pingamizi la pili, amesema licha ya maneno yaliyotajwa kwamba hayapo kwenye hati ya mashtaka, hakukuwa na rejea ya sheria iliyoonekana kukiukwa, hivyo akasema pingamizi halina msingi.
Katika hoja ya tatu, aliagiza upande wa mashtaka kuwapatia upande wa utetezi hati ya mashtaka na vielelezo muhimu ndani ya siku saba baada ya marekebisho ya hati ya mashtaka kukamilika.
Shauri hilo sasa litatajwa tena Desemba 3, 2025, huku watuhumiwa wakiendelea kusota rumande wakisubiri hatua zaidi za kisheria.
