Sababu nane za rufaa shauri la Polepole

Dar es Salaam. Jopo la mawakili wa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi na Cuba, Humphrey Polepole, limekata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam likitoa sababu nane za kufanya hivyo.

Katika rufaa hiyo, mawakili wakiongozwa na Peter Kibatala, wanapinga uamuzi wa Mahakama Kuu iliyotupilia mbali shauri la maombi ya amri ya kumfikisha mahakamani au kumwachia kwa dhamana Polepole anayedaiwa kutekwa na watu waliovamia makazi yake Ununio, jijini Dar es Salaam Oktoba 6, 2025.

Katika shauri hilo namba 24514/2025 lililosikilizwa na Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Salma Maghimbi, wajibu maombi ambao sasa ni wajibu rufaa ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZCO) na Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo (ZPC).

Uamuzi wa Jaji Maghimbi, uliosomwa Oktoba 24, 2025 na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Livin Lyakinana, ulitupilia mbali shauri hilo, akisema mwombaji alishindwa kutekeleza jukumu lake la kuithibitishia mahakama kuwa wajibu maombi ndio waliomchukua Polepole.

Mahakama ilisema kilichowasilishwa mahakamani ni hisia tu kuwa wajibu maombi ndio waliomchukua au wanajua aliko.

Baada ya uamuzi huo, Kibatala kwa niaba ya mawakili wenzake alisema walishawasilisha notisi ya kusudio la kukata rufaa.

Baada ya taratibu kukamilika, Kibatala amesema wamewasilisha sababu nane za rufaa chini ya hati ya dharura.

Akizungumza na Mwananchi leo Novemba 20, 2025 amesema hati ya dharura ya rufaa inahusisha mrufani ambaye hajulikani aliko tangu alipotekwa Oktoba 6, 2025 na hajawahi kuonekana wala kusikilizwa. Anasema maisha yake yanaweza kutegemea uamuzi wa haraka wa rufaa hiyo.

Jopo hilo linadai kuwa, mosi, Mahakama Kuu ilikosea kisheria kuamua kwamba mwombaji wa rufaa alishindwa kuthibitisha kesi yake ya kupewa amri ya Habeas Corpus ya kumleta Polepole.

‎Mbili, kwa kushindwa kuamua kwamba hakukuwa na pingamizi dhidi ya kiapo kilichoambatanishwa na maombi ya mwombaji kutokana na upungufu usiotibika katika kiapo cha majibu na viapo vya kuunga mkono vya wajibu maombi.

Tatu, kwa kushindwa kutathmini ipasavyo ushahidi uliopo kwenye rekodi na nne, kwa kushindwa kubaini na kuamua kwamba katika kesi za aina hiyo, mara nyingi hakuna ushahidi wa moja kwa moja na usiopingika.

‎Tano, kwa kushindwa kutekeleza ipasavyo nafasi yake kama msuluhishi wa mwisho na mlinzi wa haki za wananchi na sita, kwa kushindwa kuamua kesi hiyo kwa kuzingatia ushahidi wa kimazingira.

‎Sababu ya saba ni kwa kuamua kwamba kasoro zilizopo katika mawasilisho ya wajibu maombi zinatibika kwa kutegemea kanuni ya malengo ya msingi ya utoaji haki na nane, kwa kukataa hoja za kisheria ambazo ziliwasilishwa kikamilifu na pande zote mbili kulingana na sheria.

Kibatala amesema baada ya kuwasilisha sababu hizo za rufaa, wanasubiri kupangwa majaji na tarehe ya usikilizwaji wa rufaa hiyo.

Katika shauri la msingi chini ya hati ya dharura iliyothibitishwa na Kibatala, alidai Polepole aliripotiwa kutekwa na watu wanaosadikiwa kuwa ni maofisa wa Jeshi la Polisi waliovamia nyumbani kwake Ununio Oktoba 6, 2025.

Alidai mpaka siku hiyo Polepole hakuwa ameshtakiwa kwa kosa lolote la jinai katika mahakama yoyote ya kisheria na kwamba, inaaminika amewekwa kizuizini mahali kusikojulikana na wajibu maombi.

‎”Hivyo haki zake za kikatiba zimekiukwa bila sababu za msingi. Ustawi wa mwombaji unahitaji uangalizi na uingiliaji wa haraka, ikiwemo kujua hali ya maisha yake,” alidai Kibatala katika hati ya maombi.

‎Aliiomba mahakama iwaelekeze wajibu maombi wamwachie huru mwombaji (Polepole) kwa dhamana au wamfikishe katika mahakama ya kisheria na kumshtaki kwa mujibu wa sheria.

Kibatala alieleza kuwa Polepole ni raia wa Tanzania aliyeitumikia nchi yake katika nafasi mbalimbali za mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam na Balozi wa Tanzania nchini Malawi na Cuba.

Alieleza kuwa mwaka huu, kwa hiari alijiuzulu wadhifa wa ubalozi, akieleza sababu mbalimbali zikiwamo kutokuridhika na namna mambo yanavyoendeshwa ndani ya Serikali na nchini Tanzania.

Kibatala alieleza katika taarifa ambazo alikuwa akizitoa mara kwa mara, Polepole alikuwa akilalamika kuhusu usalama wake kuwa hatarini kutokana na vitisho ambavyo amekuwa akipokea kutoka kwa watu wasiojulikana kutokana na msimamo wake katika masuala mbalimbali.

Alieleza mjibu maombi wa tano (ZPC – Jumanne Muliro) alinukuliwa katika taarifa kwa vyombo vya habari akipuuza tuhuma za kutekwa kwa Polepole.

Alisisitiza kuwa mpaka wakati anaapa kiapo hicho, Polepole alikuwa hajulikani alipo na hakuna hata mmoja kati ya wajibu maombi ambaye alikuwa ametoa mrejesho wowote kuhusu alipo, hali yake ya ustawi na hadhi yake ya kisheria jambo linaloongeza kiwango cha wasiwasi nchini.

“Nina sababu za kuamini kwamba wajibu maombi na hasa mjibu maombi wa tano ZPC, ana ufahamu na yuko na mamlaka ya kumshikilia mwombaji,” alidai Kibatala.