Mwenyekiti AAFP aishauri ACT Wazalendo kuingia SUK

Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima (AAFP) Taifa, Said Soud Said amekishauri Chama cha ACT-Wazalendo kuingia ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa masilahi ya maendeleo ya Zanzibar.

Soud aliyekuwa Mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama hicho, amesema ni wakati wa ACT-Wazalendo kushiriki ndani ya SUK ili kuungana na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi kutekeleza mambo mbalimbali ya maendeleo.

Alioa kauli hiyo leo Alhamisi Novemba 20, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mwera Mkoa wa Mjini Magharibi.

“Niwasihi ACT-Wazalendo waingie kwenye SUK maana lengo ni kujenga na si kubomoa, washirikiane katika kuleta maendeleo,” amesema Said Soud ambaye katika uchaguzi huo alipata nafasi ya tisa.

Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, chama kinachopata asilimia 10 ya kura kinapaswa kuwa ndani ya Serikali kuungana na chama kinachokuwa kimeshinda uchaguzi mkuu.

Katika matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 29, 2025, Chama cha Mapinduzi (CCM) kiliibuka mshindi kwa kupata asilimia 74.8 ya kura zote kikifuatiwa na ACT-Wazalendo kilichopata asilimia 23.22 zinazokiwezesha kuwa ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Hata hivyo, pamoja na kukidhi vigezo hivyo vya kikatiba na sheria ya uchaguzi ya mwaka 2018, viongozi wa chama hicho wamekuwa wakisema kwasasa sio kipaumbele chao kuingia au kutokuingia kwenye SUK badala yake wanataka kwanza kusimamia ipatikane haki ya uchaguzi halali.

Kauli hiyo imekuwa ikirejewa kadhaa na mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Othman Masoud anapozungumza na wanachama na wafuasi wa chama hizo katika ziara maalumu aliyoanza baada ya uchaguzi mkuu.

Othman ambaye ndiye alipeperusha bendera ya chama hicho katika ngazi ya urais, alianza ziara kisiwani Pemba na sasa ameanza Unguja, kubwa zaidi wakionesha msimamo wao wa kutoingia kwa sasa ndani ya SUK kwa kile wanachodai uchaguzi haukuwa wa haki.

Hivi karubuni wakati akiwaapisha mawaziri viwanja vya Ikulu Zanzibar, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alikisihi chama hicho kuingia SUK lakini kwa nyakati tofauti pia viongozi wa chama hicho walisema hawawezi kukimbilia SUK ilhali wanaona mambo bado hayako sawa na kwamba Ktiba imetoa siku 90 kutafakari, hivyo hawana sababu ya kuliendea haraka jambo hilo.

Said Soud amesema ni vyema vyama vyote vikaungana kutoa ushirikiano kwa masilahi ya nchi na vishauri pale vinapoona kuna mambo ya msingi yanayotakiwa kufanyiwa kazi Kwa masilahi ya Taifa na sio kwa vyama au mtu binafsi.

“Sisi chama chetu tulikuwa na sera nzuri, tutahakikisha sera zile tunatafuta njia nzuri ili zitekelezwe,” amesema Said.