Dodoma. Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo ameitaka Benki ya Ushirika Tanzania (Coop bank) kuimarisha huduma za kifedha pamoja na wanaushirika ili kufikia malengo yenye tija kwenye sekta ya kilimo nchini.
Waziri Chongolo ameahidi kuendeleza ushirikiano na benki hiyo huku akiwataka watendaji wa benki ya Coop kuongeza ubunifu zaidi katika utoaji huduma.
Chongolo ameyasema hayo leo Alhamisi Novemba 20, 2025 alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa benki hiyo, Godfrey Ng’urah ofisini kwake jijini Dodoma.
“Ningetamani kuona katika biashara yoyote inayohusu kilimo basi benki ya ushirika inakuwa mnufaika wa kwanza,” amesema Chongolo.
Mbali hilo, Chongolo amepongeza ukuaji wa kasi wa benki ya Ushirika Tanzania (Coop bank) kwa kutoa majawabu ya mitaji kwa wanaushirika.
Amesema hiyo inatokana na kukuza kiwango cha fedha katika kitabu cha mikopo kutoka Sh15 bilioni Januari 2025 hadi sasa kufikia Sh52 bilioni sawa na ukuaji wa asilimia 245 huku amana ikiongezeka kutoka Sh19 bilioni hadi Sh60 bilioni sawa na asilimia 216 ya ukuaji.
Benki hiyo pia imekuza mizania yake kutoka Sh49 bilioni Januari 2025 hadi sasa kufikia Sh114 bilioni, sawa na ukuaji wa asilimia 133 na kwamba hiyo ni hatua nzuri katika kuendelea kutekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa benki hiyo Aprili 28, 2025.
“Ushirika ni kama nyumba yenye msingi imara katika kusaidia wakulima. Na ushirika wetu ni wa kilimo kuanzia maandalizi ya shamba hadi kupata matokeo. Hivyo, jambo la msingi ni benki ya Coop kuimarisha huduma za kifedha na wanaushirika ndani yake ili kufikia malengo yenye tija,” amesema Chongolo.
Waziri Chongolo ameahidi kuendeleza ushirikiano na benki hiyo, huku akiwataka watendaji wa benki ya Coop kuongeza ubunifu zaidi katika utoaji huduma.
Ng’urah amesema benki yake imeendelea kutekeleza dhamira ya kuchagiza uchumi jumuishi kwa kutoa huduma za kifedha, uwezeshaji wa kujenga maghala na masoko.
“Tuna matawi manne kwa sasa katika mikoa ya Dodoma, Kilimanjaro, Mtwara na Tabora. Malengo ya benki ni kuongeza matawi mengine manne mwisho wa mwaka katika mikoa ya Dar es Salaam, Kagera, Mwanza na Songwe,” amesema Ng’urah.
