Moshi, Tanzania — Ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na wawekezaji binafsi katika kiwanda cha Sukari—TPC Limited umepelekea mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, na kuifanya kampuni hiyo kuwa miongoni mwa wazalishaji wakuu katika sekta ya viwanda.
Sherehe za kuadhimisha miaka 20 ya ushirikiano zilifanyika Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, Jumatano, Novemba 19, 2025, wakati wa chakula cha jioni, masaa kadhaa baada ya uzinduzi wa ujenzi wa Mradi wa kiwanda kipya cha kuchakata molases ‘TPC Distillery’ wenye lengo la kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na kupanua wigo wa viwanda.
Kuzinduliwa kwa ujenzi wa mradi huo ni hatua muhimu katika upanuzi wa TPC, ambapo unatoa fursa ya upanuzi wa shughuli za kampuni katika utengenezaji wa Extra Neutral Alcohol (Ethanol), mbolea ya potasiumu, na nishati mbadala, huku ukichangia zaidi ya megawati sita (6 MW) kwenye gridi ya taifa.
Ushirikiano kati ya serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH), na TPC ulianza wakati serikali ilipobinafsisha TPC Limited kwa kuuza asilimia 75 ya hisa zake na kubakisha asilimia 25, jambo lililoacha mlango wazi, kwa uwekezaji mpya, utawala wa kisasa na ukuaji wa muda mrefu.
Baada ya miaka 20, matokeo ya uamuzi huo yanaonekana katika shughuli za kampuni, utendaji wa kifedha, na mchango wake katika jamii.
TPC, ambayo huko nyuma ilikuwa inapitia wakati mkugumu, imepata mabadiliko makubwa ya kisasa, shukrani kwa uwekezaji wa zaidi ya Sh265 bilioni katika ukarabati wa viwanda na mifumo ya usimamizi wa mazingira.
Maboresho hayo yameongeza ufanisi wa uzalishaji na kufanya kampuni kutambuliwa kitaifa kwa utendaji bora na uhifadhi wa mazingira.
Kifedha, ushirikiano huu umetoa faida kubwa kwa Serikali.
Mwaka 2023 peke yake, TPC ililipa Sh16.5 bilioni kama gawio kwa serikali, kupitia OMH, kiwango cha juu kabisa katika historia yake.
Kampuni pia inalipa zaidi ya Sh74 bilioni kila mwaka kama kodi na michango mbalimbali,
Mchango wa kijamii wa uwekezaji huu pia umekuwa mkubwa.
Hivi sasa, TPC inawaajiri zaidi ya watu 4,000 na imefadhili miradi mbalimbali ya kijamii, ikiwemo elimu, afya, maji, na miundombinu katika maeneo jirani.
Akizungumza wakati wa chakula cha jioni, Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, alisema mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 20 yanadhihirisha thamani ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.
“Mafanikio haya yanaonesha jambo moja: Kuwekeza Tanzania ilikuwa uamuzi sahihi—na mmepata mshirika sahihi katika biashara,” alisema, akisisitiza ushirikiano imara kati ya serikali na wawekezaji binafsi.
Bw. Mchechu alithibitisha dhamira ya serikali kuendeleza ushirikiano huu, akiongeza, “Tutaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji, uvumbuzi, na ukuaji wa viwanda.”