Yanga kicheko Zenji, Kocha Mreno ashusha pumzi

KIKOSI cha Yanga kinaendelea kujifua kikiwa kambini Zanzibar tayari kwa pambano la kwanza la makundi dhidi ya Far Rabat ya Morocco, huku benchi la ufundi likipata mzuka kutokana na wachezaji wa mwisho waliokuwa timu za taifa kuwasili visiwani humo.

Yanga itashuka kesho kwenye Uwanja wa New Amaan, mjini Unguja kuumana na Far Rabat katika mechi ya kwanza ya Kundi B itakayoanza saa 10:00 jioni, huku benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Mreno Pedro Goncalves ikiendelea kuwapa mbinu za kivita.

Pambano la kesho kwa Yanga litakuwa pia ni la kwanza kwa kocha Pedro katika mechi za CAF tangu alipotua Jangwani kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Romain Folz aliyeiongoza katika mechi tatu za awali, mbili za raundi ya kwanza dhidi ya Wiliete Benguela ya Angola na moja ya raundi ya pili dhidi ya Silver Straikers ya Malawi.

YANG 01

Mechi ya marudiano dhidi ya miamba wa Malawi ilisimamiwa na kocha msaidizi, Patrick Mabedi na kutinga makundi.

Yanga ilienda Zanzibar mapema wiki hii, huku ikiwakosa baadhi ya wachezaji waliokuwa timu za taifa zilizokuwa zikiwajibika kulingana na kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA), lakini taarifa njema kwa mashabiki wa klabu hiyo ni kukamilika kwa jeshi zima kambini.

Kipa Djigui Diarra na kiungo mkabaji, Duke Abuya ndio waliokamilisha jeshi hilo baada ya kudaiwa wametinga kambini jana kuungana na wenzao kujiandaa kwa mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayosubiriwa na mashabiki wengi wa soka kuona wenyeji wanaanzaje makundi.

YANG 02

“Kipa Diarra na Abuya wameshawasili kambini na kwa maana jeshi sasa limekamilika na benchi la ufundi limefurahia kwa sababu limekuwa likitaka kumalizia mazoezi ya mwisho wakiwa kamili kabla ya kukabiliana na wageni wetu Jumamosi,” mmoja wa viongozi wa Yanga alisema.

Wachezaji wengine waliokuwa Taifa Stars waliwahi mapema na hata Celestin Ecua, Lassine Kouma waliokuwa timu ya taifa ya Chad pamoja na Prince Dube waliwahi mapema kambini na hivyo kuongezeka kwa kina Diarra kunamfanya Pedro kuwa na jeshi kamili.

YANG 04

Kwa mujibu wa ratiba ya mazoezi ya Yanga leo saa 3 asubuhi itajifua kwenye Uwanja wa New Amaan ambapo itaruhusu pia vyombo vya habari kabla ya saa 4 kuwepo kwa mkutano wa makocha kwa ajili ya mechi hiyo ya kesho itakayochezeshwa na mwamuzi Ahmad Imtehaz Heerallal kutoka Mauritania.

YANG 03

Yanga inahitaji ushindi katika mechi ya kesho ili kuanza vyema makundi kwa msimu huu kwani msimu uliopita katika michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilianza kwa kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Al Hilal ya Sudan kabla ya kwenda kupasuka 2-0 kwa MC Alger ya Algeria.

Matokeo hayo kwa Yanga iliyokuwa chini ya kocha mpya enzi hizo, Sead Ramovic aliyekuwa amechukua nafasi ya Miguel Gamondi kwa kiasi kikubwa yalichangia kuikwamisha kutinga robo fainali kwa msimu wa pili mfululizo, kwani ilikusanya pointi nane nyuma ya Al Hilal na MC Alger.