Dakika 360 kwa Pacome, Rushine balaa zito

NYOTA wa vikosi vya Yanga na Simba akiwamo Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli, Rushine De Reuck na Jonathan Sowah, wana kazi kubwa ya kufanya katika kipindi cha takribani dakika 360 sawa na mechi nne zilizobeba maana kubwa.

Katika kipindi hicho, kuna mechi zinazochezwa zikikaribiana zikipishana siku tatu hadi nne, huku zikiwalazimu kusafiri umbali mrefu.

Mechi hizo hakuna ya kusema ina afadhali, zote ni ngumu kwa Yanga na Simba ambazo zimekuwa zikipigana vikumbo kila msimu kusaka rekodi ndani na kimataifa.

Mbali na wakongwe hao, hata Azam na Singida Black Stars, mastaa wao nao wanaingia kwenye mkumbo huo kutokana na maboresho ya ratiba ya Ligi Kuu Bara iliyotolewa Novemba 17, 2025 na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).

Maboresho hayo yameziba viporo vilivyojitokeza siku chache zilizopita kutokana na ligi kusimama ghafla kipindi cha takribani wiki moja, wakati wa vurugu zilizotokea kuanzia Oktoba 29, 2025. Hadi sasa, Yanga imecheza mechi nne za ligi, wakati Azam, Simba na Singida Black Stars zikishuka dimbani mara tatu, huku tayari ligi imefika mzunguko wa sita.

Timu hizo zote wikiendi hii zitakuwa na mechi za kimataifa hatua ya makundi, ambapo Yanga na Simba zinashiriki Ligi ya Mabingwa, huku Azam na Singida Black Stars zikicheza Kombe la Shirikisho na viporo vyao vimetokana na ratiba kuwabana na kusababisha hata wapinzani waliopaswa kucheza nao kwenye ligi, kuwa na michezo michache kama TRA United (3), Tanzania Prisons (4), Mtibwa Sugar (5) na Coastal Union (5).

Katika dakika 360 zinazowakabili mastaa wa timu hizo, ndani yake kuna takribani siku 15, hiyo ni kuanzia Jumamosi ya Novemba 22, 2025 hadi Jumapili ya Desemba 7, 2025 ambapo ndipo ligi itasimama kwa ajili ya kupisha Fainali za AFCON zinazofanyika Morocco.

Katika michuano hiyo ya AFCON 2025 inayoanza Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026, Tanzania inashiriki, hivyo kuifanya ligi kusimama hadi Januari 21, 2026 itakapoendelea. Hata hivyo, ligi itakapoendelea, wawakilishi hao wa kimataifa watakuwa na mechi za makundi za CAF, ikiwalazimu kuzalisha viporo vingine.

Katika siku hizo 15, Yanga itaanza Jumamosi hii Novemba 22, 2025 kuikaribisha AS FAR Rabat ya Morocco katika mechi ya Kundi B ikichezwa kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar, saa 10:00 jioni.

Baada ya mechi hiyo, itasafiri kwenda Algeria kukabiliana na JS Kabylie, katika mechi ya pili hatua ya makundi. Hii itachezwa Novemba 28, 2025.

Desemba 2, 2025, Yanga itakuwa na mechi ya Ligi Kuu Bara jijini Mbeya dhidi ya Tanzania Prisons, kisha itaenda Tanga kuikabili Coastal Union, Desemba 7, 2025.

Kwa upande wa Simba, inaanza kazi Jumapili hii Desemba 23, 2025 kwa kucheza dhidi ya Petro Atletico ya Angola kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwa ni mechi ya Kundi D.

Ratiba inaonyesha Novemba 28, Simba itakuwa Mali kucheza na Stade Malien kwa mechi ya pili ya hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa, kisha Desemba 3, itasafiri kwenda Tabora kuikabili TRA United kwa mechi ya Ligi Kuu Bara.

Itamaliza siku hizo ngumu kwa kuikaribisha Azam, Desemba 6, 2025 ikiwa ni mechi ya Ligi Kuu itakayochezwa Kwa Mkapa.

Azam iliyopangwa Kundi B la Kombe la Shirikisho Afrika ikifuzu kwa mara ya kwanza, Jumapili hii Novemba 23, 2025 itakuwa DR Congo kucheza na AS Maniema, kisha Novemba 28, 2025 itaikaribisha Wydad kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.

Baada ya hapo, itacheza mechi mbili za ligi, zote jijini Dar es Salaam, ikianza na Singida BS (Desemba 3, 2025) kisha Simba (Desemba 6, 2025).

Singida BS nayo ipo Kundi C Kombe la Shirikisho, Jumamosi Novemba 22, 2025 itaikabili CR Belouizdad huko Algeria, kabla ya kurudi nyumbani kucheza na Stellenbosch, Novemba 30, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex.

Mechi mbili zinazofuatia hapo ni za ligi dhidi ya Azam (Desemba 3, 2025) jijini Dar kisha dhidi ya TRA United (Desemba 6, 2025) mkoani Singida.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amezungumzia mechi hizo na maandalizi ya kikosi hicho akisema: “Baada ya mechi yetu ya mwisho dhidi ya JKT Tanzania, wachezaji walipata mapumziko kidogo, wale waliokuwa hawana majukumu ya timu za taifa wakarejea kambini na kuanza program ya mazoezi, jambo la kumshukuru Mungu asilimia kubwa ya wachezaji ni wazima, tunaamini watatupa matokeo mazuri katika mechi zinazotukabili.”

Meneja wa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, alisema: “Kwanza tunazitaka pointi tatu za mechi hii ya mbele yetu dhidi ya FAR Rabat, lakini kubwa zaidi tunataka kufanya vizuri katika kila mechi bila ya kujali ratiba ilivyo.”