Uhusiano wa amani na haki katika Uislamu

Hakika fadhila na hisani za Allah kwa wanadamu ni kubwa zisizo na ukomo wala mipaka, neema zake haziwezi kuhesabiwa wala kuandikwa.

Miongoni mwa neema zake kubwa zaidi ni amani na utulivu. Hizi ni nguzo muhimu za maisha na miongoni mwa mahitaji ya lazima kwa kila binadamu na hata viumbi wengine wa mwituni na baharini.

Uislamu umehimiza kwa hali yoyote ile kuyalinda mambo matano ya lazima, ambayo sharia zote za mbinguni zimekubaliana juu ya umuhimu wake, mambo hayo ni dini, nafsi, akili, heshima na mali.

 Mambo haya hayawezi kulindwa iwapo amani na utulivu zitatoweka. Wanazuoni wa kiislamu wanaielezea amani kuwa ni “Hali ya mtu binafsi au jamii, ndani ya taifa au nje yake, kuhisi utulivu wa maisha na kuondolewa sababu zote za hofu. Al-Ghazali –Allah amrehemu anaweka wazi kwamba kusimama kwa dini kunategemea kusimama kwa dunia … na utaratibu wa dini una msingi yake katika elimu na utekelezaji wa ibada, lakini elimu na ibada haziwezi kufanyika bila ya kuwa na afya, uhai, mahitaji muhimu kama makazi, mavazi, chakula, na amani.”

Nchi yetu tangu uchaguzi wa Oktoba 29 inapitia katika kipindi kigumu, katika mambo matano ambayo dini za mbinguni zimekubaliana kuyalinda, akili na heshima ndio mambo ya mwanzo kushambuliwa hata kabla ya siku ya maandamno, wezi wa akili na wavunjifu wa heshima za watu walianza kuziharibu baadhi ya akili za watu kupitia mitandao ya kijamii.

 Amani ya akili na fikra ni muhimu kama ilivyo amani ya roho na mali. Kama vile roho na mali zina wezi wanaoweza kuziiba, vivyo hivyo akili pia zina wezi. Hawa ni watu wanaoharibu fikra za watu. “wezi wa akili” ni hatari zaidi kuliko wale wanaoiba mali.

Dini nayo iliathirika kwani Ijumaa baadhi ya misikiti walishindwa kusali kwa sababu ya ukosefu wa amani. Mali na roho za watu ndio zilizoathirika kwa kiwango kikubwa. Bila shaka kila mmoja wetu amepata somo la umuhimu wa amani, wahenga walisema: Kuielezea hali kwa vitendo hufahamika zaidi kuliko kuielezea kwa maneno.

Amani ikipotea, mzunguko wa maisha husimama, bali hata maendeleo hurudi nyuma. Kwa kuzingatia hilo Nabii Ibarahim (a.s) aliwaombia watu wa Makka dua: “Na aliposema Ibrahim: Ee Mola wangu mlezi! Ufanye huu uwe mji wa amani, na uwaruzuku watu wake matunda..” (2:126).

Katika vurugu za uchaguzi vyakula vilipanda na kufikia nyanya moja kuuzwa Sh2,000, hofu ilitawala kutoka eneo moja hadi nyingine. Allah Mtukufu ameonya kwa watu walioikana neema ya amani kwa kusema: “Na Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mji ulio kuwa na amani na utulivu, riziki yake ikiufikia kwa nafasi kutoka kila mahali. Lakini ukazikufuru neema za Mwenyezi Mungu; kwa hivyo Mwenyezi Mungu akauvika vazi la njaa na hofu kwa sababu ya yale waliyo kuwa wakiyafanya. (16:112).

Vitabu vyote vya mbinguni vimekuja kubainisha haki, uadilifu na tabia njema na kukataza dhuluma, ukandamizaji na tabia mbaya. Allah Mtukufu anasema: “Na kwa haki tumeiteremsha(Qur’an), na kwa haki imeteremka…” (17:105). Lakini Uislamu unaeleza haifai kuidai haki kwa muda kama kutakuwa na mazingira ya umwagikaji damu, ili kuchunga maslahi ya roho za watu.

Mkataba wa Hudaibiya uliojiri baina ya makafiri wa Makka na Mtume wa Allah mwaka wa sita Hijria unathibitisha hili. Mtume wa Allah alitoka Madina na Masahaba wapatao 1500 kutekeleza ibada ya Umra Makka, alipofika Hudaibiya Makuraishi (makafiri) walimzuia.

Baada ya majadiliano mazito kujiri, pandi zote mbili zilifunga mkataba wa amani wenye vipingile vingi vinavyo wakandamiza waislamu. Hali hii iliwafanya Masahaba wa Mtume kupinga mkataba huo. Lakini Mtume wa Allah aliwasihi kukubali vipingile hivyo, ili kulinda umwagikaji damu.

Mtume alimwamuru mwandishi wake kuandika katika hati ya mkataba: “Haya ndiyo makubaliano yaliyoafikiwa baina ya “Muhamaadi Mtume wa Allah na Makafiri wa Makka” Lakini makafiri walipinga kuandikwa “Muhammad Mtume wa Allah” badala yake iandikwe “Muhammd bin Abdillah” Ili kulinda damu ya waislamu, Mtume alikubali matakwa yao, lakini aliwaambia” Mimi ni Mtume wa Allah” hata kama mnapinga hilo kuandikwa.

Huu ni ushahidi kuwa haki ndio msingi wa amani, lakini katika mazingira ya umwagaji damu, ni vema kuacha kuidai haki kwa muda, ili kulinda damu za watu, lakini sio kuinyamazia haki hiyo, ili  anayeizuia ajue kuwa ipo kama Mtume wa Allah alivyofanya.

Allah anasema: “Tuliwaandikia wana wa Israili ya kwamba aliyemuua mtu ambaye hakuua au hakufanya uharibifu katika nchi, basi ni kama amewaua watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote…” (5:32).

Kulinda roho za watu kunathamani kubwa katika dini ya Uislamu kuliko kitu kingine. Mwaka wa nane Hijria (miaka miwili mbele), Mtume aliingia katika mji wa Makka kwa amani huku akisema: “Nasema: haki imefika, na batili imetoweka. Hakika batili lazima itoweke! (17:81).http://quranitukufu.net/quraniswahili/c17.html – 81