Tanzania yaporomoka nafasi tano viwango vya ubora FIFA

Tanzania imeporomoka kwa nafasi tano kwenye viwango vya ubora vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) katika chati ya viwango ya mwezi Novemba.

Kichapo cha mabao 4-3 ambacho timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ imekipata katika mechi ya kimataifa ya kirafiki, Novemba 15, 2025 kinaonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa kuiangusha Tanzania kutoka nafasi ya 107 iliyokuwepo awali hadi nafasi ya 112.

Anguko kwenye chati ya ubora wa FİFA, linaonekana kutoigusa Tanzania bali hapa majirani zetu Kenya na Uganda.
Wakati Uganda ikianguka kutoka nafasi ya 83 hadi ya 85 wakati Kenya iliyokuwa nafasi ya 109 imeshuka kwa nafasi nne na kuangukia nafasi ya 113.

Morocco ambayo kidunia imepanda hadi nafasi ya 11, kutoka ile ya 12 ambayo ilikuwepo awali, bado inaendelea kuwa kinara katika Bara la Afrika ikifuatiwa na Senegal.

DR Congo ambayo imefanya vizuri katika mechi za mchujo za Bara la Afrika za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 ikizifunga Cameroon na Nigeria, imepanda kwa nafasi nne kutoka ya 60 ambayo ilikuwepo awali hadi ya 56.

Nigeria yenyewe imepanda kwa nafasi tatu hadi ya 38, ikitokea nafasi ya 41 ambayo ilikuwepo katika viwango vya FIFA vya mwezi Oktoba, 2025.

Hakuna mabadiliko katika nafasi nne za juu za chati hiyo ambapo timu nne zilizokuwa hapo zimebaki kama zilivyo kinara ikibaki kuwa ni Hispania kama ilivyokuwa hapo kabla.

Argentina imeendelea kushika nafasi ya pili nyuma ya Hispania na nafasi ya tatu inaendelea kushikiliwa na Ufaransa huku nafasi ya nne ikiwepo England.