Baba amuua mwanaye wa miaka miwili kwa kumnyonga, naye ajinyonga

Mbeya. Mtoto wa miaka miwili Deniva Derick (2) ameuwawa kwa kunyongwa hadi kufa kwa kutumia kamba ya manila na Baba yake mzazi Derick Mwangama (23), ambaye naye alijinyonga na kupoteza maisha.

Imeelezwa kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 18, 2025 katika Kijiji cha Isaka, Kata ya Nkunga,Tarafa ya Ukukwe, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya leo Novemba 21,2025 amesema awali kabla ya tukio hilo baba mzazi wa mtoto huyo ambao wote ni marehemu, alikwenda nyumbani kwa mzazi kwenzie Violeth Edward (19) na kumchukua kwa nguvu mtoto huyo huku akiwa na jazba.

Kuzaga amesema baada ya kuondoka naye, baadaye mwili wa mtoto ulikutwa ukiwa umenyongwa na kisha kutekelezwa kando ya Mto Kiwira.

Amesema baba wa mtoto huyo ambaye ni marehemu baada ya kufanya mauaji hayo ya mwanaye, alijinyonga kwa kutumia kamba ya manila kwenye mti wa parachichi kando ya mwili wa mtoto wake.

“Uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha tukio hilo ni kuibuka kwa mgogoro baina wenza hao ambao walikuwa wametengana,” amesema.

Katika hatua nyingine Kamanda Kuzaga amesema amesikitishwa na tukio hilo na kuwataka wazazi pindi wakiwa na migogoro ya kifamilia kutafuta njia sahihi ya kutatua kwa kushirikisha watu wa jirani ili kuepuka madhara kama hayo.

“Watu walio kwenye ndoa wajitahidi kuepuka migogoro kwa kutafuta njia sahihi ya kutatua kwa amani ili kuachana na uamuzi wa kujikatisha uhai,” amesema.

Mkazi wa eneo hilo, Damian Haule amesema miaka ya sasa migogoro mingi ya kufamilia chanzo kikubwa ni wanawake wakimiliki uchumi mkubwa hudharau wenza wao na kubeba jukumu la kutunza na kuhudumia familia.

“Huku mitaani tunashuhudia hali siyo nzuri wanaume wana dhalilishwa na hata kutukanwa matusi ya nguoni na wenza wao jambo ambalo hupelekea kuchukua maamuzi magumu,” amesema.

Mwananchi mwingine Erasto Mwakalonge amesema kimsingi miaka ya sasa ndoa zimekuwa chungu kwa wanaume hususani mwanamke akibarikiwa kuwa na uchumi kumzidi mwenza wake.