KOCHA Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves amesema katika mechi ya kesho Jumamosi Novemba 22, 2025 dhidi ya AS FAR Rabat, licha ya wapinzani wao kuwa na rekodi kubwa kimataifa kulinganisha na kikosi alichonacho, lakini hawataingia uwanjani kinyonge.
Pedro, raia wa Ureno ameyasema hayo leo Novemba 21, 2025 mbele ya Waandishi wa Habari hapa Zanzibar kwa ajili ya mechi ya kesho Jumamosi ya Kundi B la Ligi ya Mabingwa Afrika, huku akisisitiza ana kikosi chenye uwezo wa kuanza na ushindi.
Mechi hiyo ya kwanza kwa timu hizo, imepangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja kuanzia saa 10:00 jioni.
“Kesho ni mechi ya kwanza. Nafikiri kila mtu aliona kundi hili kuwa na ushindani mkubwa zaidi, likiwa na klabu nne bora kabisa Afrika. Tatu tayari zimeshawahi kuwa mabingwa, nasi tuna ndoto ya kuwa mabingwa siku moja pia,” amesema Pedro akianza kwa kutoa matumaini ya siku moja Yanga itashinda ubingwa wa CAF.
Kuhusu FAR Rabat inayofundishwa na Alexandre Santos, Pedro amesema: “Wapinzani wetu ni klabu yenye nguvu, timu ambayo imepiga hatua kubwa katika misimu miwili iliyopita.
“Ninawafahamu vizuri, wana kocha mzuri kama ilivyo kwa makocha wengi wanaofundisha Ligi ya Mabingwa. Amefanya kazi kwa mwaka mmoja akiijenga timu iliyo imara katika kila eneo.”
Kuhusu kikosi cha Yanga, Pedro amefichua kwamba: “Lakini sisi pia tumejiandaa kwa muda mrefu na tunaamini kuwa kesho, kwa msaada wa mashabiki wetu hapa Zanzibar, tutapata nguvu ya ziada. Inanipa furaha kubwa kuona namna wanavyotupa nguvu.
“Naamini kesho kutakuwa na mazingira mazuri sana, mashabiki wakiwa na ari na wachezaji wetu wakionesha kujituma, tutaweza kufanikisha azma yetu.”
Pedro ameongeza: “Ni kweli pia kwamba wapinzani wetu wa kesho wamefanya mabadiliko makubwa kwenye kiungo cha kati.
“Kuhusu sisi, tuna kikosi cha wachezaji 32. Kwa bahati mbaya, wawili ni majeruhi. Hata hivyo, bado tuna faraja na motisha ya kufanya kazi kwa bidii kwa sababu tuna lengo kubwa mbele yetu. Ni changamoto kubwa, lakini tupo tayari kupambana na kushinda.”
Mmoja wa majeruhi wa Yanga ni Clement Mzize aliyefanyiwa upasuaji wa goti hivi karibuni.
Mwisho kabisa, Pedro amesisitiza kesho Yanga itakuwa ya tofauti na mechi mbili zilizopita alizoiongoza timu hiyo za ligi alizoshinda zote dhidi ya Mtibwa Sugar (2-0) na KMC (4-1).
Yanga katika Kundi B mbali na AS FAR Rabat ya Morocco, imepangwa pia na Al Ahly ya Misri na JS Kabylie kutoka Algeria.
Baada ya mechi ya kesho, wikiendi ijayo ya Novemba 28, 2025 itakuwa Algeria kukabiliana na JS Kabylie, kisha itasubiri hadi mwakani kupambana na Al Ahly nje ndani.
Katika kundi hilo, AS FAR Rabat imebeba Kombe moja la Ligi ya Mabingwa, JS Kabylie imeshashinda mataji hayo mawili, huku Al Ahly ikiwa bingwa wa kihistoria ikishinda 12. Yanga bado.
