ALEXANDRE Santos, kocha mkuu wa AS FAR Rabat raia wa Ureno, ameitaja Yanga ni kati ya timu zenye wachezaji wazawa wenye kiu ya mafanikio, hivyo kukabiliana nayo ni lazima uwe makini.
Kauli ya Santos imekuja FAR ikijiandaa kucheza mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Kundi B dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, kesho Jumamosi Novemba 22, 2025, saa 10:00 jioni.
“Kesho, tutakutana na timu ya Afrika iliyojaa wachezaji wa ndani wenye kiu na malengo, hivyo lazima tuwe makini kuwakabili,” amesema Santos.
Katika hatua nyingine, Santos amezungumzia mabadiliko ya kikosi cha FAR kutokana na maingizo mapya yaliyofanyika msimu huu, akisema: “Tumefanya mabadiliko kwa muda mfupi kama walivyofanya, lakini tutapambana kwa kutumia silaha zetu, uwezo wetu, wachezaji wetu wapya na waliopo, tutajitahidi kuona ni nani bora.
“Tunahitaji kushinda, lakini ni lazima tuwe tayari kwa ushindi huo. Tunahitaji kuonyesha ndani ya timu kuwa tunaweza kushinda zaidi na kuwa bora zaidi. Hilo ndilo lengo letu.”
Santos amesisitiza mechi ya kesho ina umuhimu zaidi kwao kupata ushindi akisema: “Mechi hii ndio muhimu zaidi kwetu. Tunachoweza kufanya ni kucheza vizuri na kushinda. Lengo letu si kwenda kucheza kwa kubahatisha bali kwa kujitolea.
“Bado tupo katika hali ya kujifunza, lakini tutafanya bora zaidi. Tunahitaji mechi ngumu ili kuonyesha uwezo wetu halisi. Tunahitaji kuwa thabiti, ubora wa hali ya juu.”
AS FAR Rabat iliyowahi kubeba taji la Ligi ya Mabingwa mara moja mwaka 1985 na Kombe la Shirikisho mwaka 2005, ina mtihani wa kufanya vizuri zaidi katika michuano ya CAF msimu huu baada ya msimu uliopita kuishia robo fainali ilipochapwa jumla ya mabao 4-3 na Pyramids iliyoenda kubeba ubingwa.
Kwa upande wa Yanga, msimu uliopita katika Ligi ya Mabingwa iliishia makundi, kabla ya hapo, 2023-2024 iliishia robo fainali.