Dar es Salaam. Zikiwa zimepita siku nne tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipoteua Baraza la Mawaziri, joto la uteuzi limehamia kwa nafasi za makatibu wakuu na naibu wao, wakuu wa mikoa na wilaya, makatibu tawala wa mikoa na wale wa wilaya pamoja na wakurugenzi wa halmashauri.
Uteuzi wa mawaziri umetoa mwelekeo wa mabadiliko anayoyafanya kiongozi huyo, kwani ameteua mawaziri wapya wanane, huku akiwaacha nje saba waliokuwa kwenye baraza lililopita na wengine wakisalia katika nafasi zao.
Samia aliapishwa Novemba 3 kushika muhula wa pili baada ya uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Kwa sasa anaendelea kuunda Serikali yake mpya kwa kuteua viongozi wa ngazi mbalimbali watakaomsaidia kazi katika miaka mitano ijayo.
Baada ya kumteua Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, Rais Samia aliteua mawaziri 27, huku akianzisha wizara maalumu ya Maendeleo ya Vijana katika Ofisi ya Rais.
Nafasi za uteuzi zinazosubiriwa kwa sasa ni makatibu wakuu na naibu wao, wakuu wa mikoa na wilaya, makatibu tawala wa mikoa na wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri.
Baada ya uteuzi huo wa awali, kituo kinachofuata ni panga pangua ya makatibu wakuu wa wizara 26, manaibu wao sambamba na wakuu wa mikoa 26 ya Tanzania Bara na makatibu tawala wa mikoa.
Vilevile, wakuu wa wilaya 139 na makatibu tawala wa wilaya hizo, pamoja na watendaji wengine kwenye halmashauri 184 pamoja na taasisi na mashirika ya umma.
Waliopo kwenye nafasi hizo kwa sasa unaweza kusema wako matumbo joto kutokana na mabadiliko ambayo Rais Samia ameshayafanya kwa nafasi za juu kwa kuwaondoa waliokuwapo na kuweka wapya au kuwabadilisha nafasi baadhi yao.
Wakati walio kwenye nafasi wakiwa tumbo joto, baadhi ya makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanasubiri kukumbukwa katika uteuzi serikalini kutokana na mchango wao wakati wa kampeni za chama hicho katika uchaguzi mkuu uliopita.
Makada hao wanazitazama nafasi za ukuu wa mkoa na wilaya na ukurugenzi wa halmashauri, jambo linaloongeza joto kwa viongozi walioshika nyadhifa hizo.
“Tumezoea hizo nafasi wanapewa makada waliokisaidia chama kwenye uchaguzi mkuu au nyakati ngumu. Vinginevyo, ni itakavyompendeza mwenyekiti wa chama (Rais) kwa watu wake,” amesema Derrick Masunga, kada wa CCM Kata ya Pugu.
Ni mtazamo wa mchambuzi wa masuala ya uchumi na kijamii, Oscar Mkude kuwa yanawezekana yakawepo mabadiliko makubwa katika utendaji wa Serikali, akieleza hatua hiyo ni muhimu kutokana na changamoto ambazo Taifa linapitia kwa sasa.
Mkude amesema matukio ya Oktoba 29, 2025, ambayo Rais tayari ameyataja hadharani kuwa “yametutia doa”, yanaweza kuathiri utendaji wa Serikali endapo hakutakuwa na nguvu mpya yenye weledi katika maeneo ya msingi ya uongozi.
Oktoba 29, kuliibuka maandamano yaliyoambatana na vurugu zilizosababisha uharibifu wa mali na vifo.
“Lazima tuwe na wakuu wa mikoa, wilaya na makatibu tawala wanaoweza kutafsiri sera na kuzitekeleza kwa ufanisi bila kuongeza gharama kwa Serikali,” amesema Mkude.
Ameeleza kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakitumia fursa ya kugombea ubunge kama ngazi ya kupata nafasi za utendaji serikalini zikiwamo ukuu wa wilaya au mkoa.
Anasema licha ya nafasi hizo kuonekana za kisiasa, zinahitaji wataalamu wenye uwezo mkubwa wa kiutendaji.
“Mkuu wa mkoa au wilaya anatakiwa awe na uwezo wa kusimamia vizuri ili kuepusha kukwamisha utendaji wa walio chini yake. Katika kipindi hiki kigumu, mabadiliko lazima yaonekane,” amesema.
Mkude amesema matumizi ya Serikali katika ngazi za wilaya na sekretarieti za mikoa yanapaswa kuwa ya kueleweka kwa kuwa huko ndiko huduma muhimu za wananchi hutolewa na ndiko matumizi makubwa huanzia.
“Ikiwa viongozi wataendelea na mtindo wa zamani, utekelezaji wa miradi na huduma kwa wananchi utachelewa kuonekana,” amesema.
Amesema ni muhimu kwa Serikali kuimarisha utendaji kwa kuweka viongozi wenye uwezo, weledi na wanaoweza kusimamia rasilimali za umma kwa ufanisi zaidi.
Kwa mtazamo wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Loisulie, mabadiliko katika Serikali ya awamu ya sita hayakwepeki.
Anabainisha sababu kuu tatu zinazoweza kuchochea hatua hiyo, ikiwamo hitaji la kuleta mawazo mapya katika utendaji wa Serikali.
Dk Loisulie amesema Serikali yoyote inapopitia hatua za mageuzi ni muhimu kuakisi sura mpya ili jamii ione mwelekeo mpya wa kiuongozi.
“Mawazo mapya ni muhimu na kwa kuwa hii ni Serikali ya awamu ya sita, lazima iundwe upya ili hata jamii ikitazama ione kuna upya,” amesema.
Sababu ya pili amesema mabadiliko yanahitajika ili kuendana na mahitaji ya sasa pamoja na changamoto mpya zilizojitokeza, hivyo kuna ulazima wa kuangalia watu wenye uwezo na ujuzi wa kusaidia kusukuma mbele ajenda za Serikali.
Sababu ya tatu, amesema inahusu utendaji wa viongozi waliopo madarakani.
“Kila mmoja ataangaliwa utendaji wake baada ya kupewa nafasi. Aliyefanya vizuri atabaki, lakini yule ambaye hakuonyesha ufanisi atalazimika kupisha wengine wapya,” amesema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa George Kahangwa amesema hatarajii mabadiliko makubwa katika maeneo hayo kwa sababu katika ofisi hizo kuna watu wamekuwa wakiendelea na kazi.
“Kwa makatibu wakuu, zile ofisi si za kisiasa na makatibu tawala wa mikoa wapo lakini kinachoweza kutokea anaweza kuwahamisha kutoka eneo moja kwenda lingine,” amesema.
Amesema matumaini yake hata uhamisho unaweza kutokea na inaweza usiwe wa haraka kulingana na anavyoendelea kuongoza, ingawa aligusia kwa wale ambao umri wao wa utumishi unafikia ukomo lazima nafasi zao zitajazwa.
“Mtazamo wangu, katika maeneo hayo sitarajii mabadiliko makubwa na haraka lakini kama ingekuwa Rais mpya kaingia madarakani, angekuwa anapanga safu yake,” amesema.
Profesa Kahangwa amesema wapo waliokuwa wakuu wa mikoa na wilaya, Rais aliwataka waseme mapema nia zao kabla ya uchaguzi mkuu ili atafute watu wa kujaza nafasi zao.
“Ikiwa kujaza nafasi za waliokuwa wabunge ilishafanyika tayari, hivyo kama itakuwepo nafasi, basi wakati anazunguka kwenye kampeni nchi nzima kuna mahali aliona kunapwaya au kupata taarifa kuhusu utendaji wa watu, ni wazi kuna watakaoondoka kwa sababu ya kiutendaji,” amesema.
Profesa Kahangwa amesema kwa kuwa Rais Samia amezungumzia suala la kuwapa nafasi vijana, basi katika nafasi za watendaji wapya matarajio ni kuwa vijana watakuwa wengi.
