Na John Bukuku – Dar es Salaam
IGP Mstaafu, Balozi Ernest Mangu, ameelezea kuridhishwa na maendeleo ya Chuo cha Bandari wakati akihutubia katika mahafali ya 24 yaliyofanyika Novemba 21, 2025, katika Kampasi ya Temeke jijini Dar es Salaam. Amesema kuwa hafla hiyo imempa nafasi ya kushuhudia hatua mbalimbali za utekelezaji wa majukumu ya chuo, ambacho ni taasisi muhimu katika maendeleo ya sekta ya bandari na uchukuzi.
Amebainisha kuwa mahafali hayo yamewakutanisha wadau mbalimbali kusherehekea mafanikio ya jumla ya wahitimu 757 wa ngazi za astashahada, stashahada na kozi za muda wa mwaka mmoja hadi mitatu. Amepongeza juhudi binafsi za wahitimu pamoja na malezi ya wazazi na walezi waliowawezesha kukamilisha hatua hiyo muhimu kwa ustawi wa maisha yao na taifa.
Aidha, amesema kuwa ameridhishwa na jitihada za chuo katika kuandaa wataalamu waliobobea kwenye sekta ya uchukuzi, na amekishukuru chuo kwa kuendelea kuandaa mitaala inayoendana na mahitaji ya kisekta kwa lengo la kuzalisha wataalamu wa bandari na usafirishaji. Amesema hatua hiyo inaendana na dhamira ya serikali kupitia uongozi wa TPIF ya kuhakikisha chuo kinaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi.
Amepongeza Menejimenti ya TPA na Bodi ya Magavana wa Chuo kwa kuendelea kukisimamia na kukipatia rasilimali muhimu zinazowezesha kuandaa nguvukazi yenye ujuzi na umahiri wa kukabiliana na changamoto za kiutendaji katika kipindi cha maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Aidha, amebainisha kuwa uwekezaji uliofanywa na TPA katika mwaka wa fedha 2024/2025 wa ununuzi wa mitambo ya kufundishia kwa uigaji yenye uwezo wa kufundisha mashine 10, ikiwemo oil and gas drilling, bulldozer, damper truck na mingine, uliogharimu zaidi ya dola milioni 1.4, ni uthibitisho wa dhamira ya dhati ya kuboresha uwezo wa chuo kutoa mafunzo ya vitendo kwa wataalamu wa sekta ya bandari na ujenzi wa miundombinu.
Amesema mafunzo ya muda mfupi yanayotolewa na chuo katika maeneo maalum ya utaalamu ni fursa muhimu kwa wahitimu kuongeza thamani katika soko la ajira pamoja na kushiriki kikamilifu katika miradi mikubwa ya kimkakati ya serikali. Ameongeza kuwa mafunzo hayo yanawawezesha vijana hata kupata nafasi za ajira katika nchi za jirani zenye uhaba wa wataalamu.
Aidha, amebainisha kuwa mipango ya serikali ya kuendeleza bandari za Bagamoyo, Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na zile za Maziwa Makuu sambamba na uunganishaji wa bandari kavu, reli, barabara na anga itachochea ukuaji wa biashara na kuvutia ajira mpya kwa vijana waliomaliza mafunzo katika Chuo cha Bandari.
Amesema uendeshaji wa bandari duniani kote hutegemea nguvukazi yenye umahiri wa hali ya juu, hivyo wahitimu wa chuo hicho wana fursa kubwa kutokana na mafunzo yanayohusisha moja kwa moja shughuli za bandari na usafirishaji. Katika hatua nyingine, ameielekeza menejimenti kukamilisha mchakato wa muundo mpya wa chuo utakaokuwa na kitengo cha Research and Business Development kwa lengo la kuboresha utendaji wa sekta ya bandari.
Aidha, amesema chuo kinapaswa kuharakisha ujenzi wa miundombinu wezeshi ikiwemo vifaa vya kujifunzia na kufundishia, huku akiitaka TPA kuendelea kuwezesha wakufunzi kupata mafunzo zaidi ndani na nje ya nchi ili kuongeza umahiri unaokidhi viwango vya kimataifa. Ameelekeza pia chuo kuanzisha kanuni za mafunzo ya lazima kwa watendaji wa sekta ya bandari ili kuongeza usalama na ufanisi katika maeneo ya kazi.
Pia, IGP Mstaafu Mangu ameelekeza vyuo vya uchukuzi kuanzisha ushirikiano katika utoaji wa mafunzo kwa sababu sekta ndogo za bandari, reli, anga na usafirishaji zinategemeana.
