Polisi yaonya kauli zinazochochea chuki, kuvuruga amani

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi nchini limetoa tahadhari kuhusu kuongezeka kwa kauli za uchochezi zinazoweza kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu wa taifa.

Katika taarifa yake, jeshi hilo limesema linafuatilia kwa ukaribu mwenendo wa hali ya usalama nchini na litaendelea kuchukua hatua stahiki dhidi ya mtu yeyote au kundi litakalobainika kukiuka sheria kwa kutoa kauli zenye mwelekeo wa kuchochea vurugu au migawanyiko katika jamii.

Onyo hilo linakuja wakati ambapo kumekuwepo na mfululizo wa matamko kutoka kwa baadhi ya makundi na watu binafsi kufuatia vurugu zilizotokea wakati wa uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, matamko ambayo yameibua mjadala na misimamo tofauti katika maeneo mbalimbali nchini.

Katika taarifa iliyotolewa leo Ijumaa, Novemba 21, 2025 kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nchini jijini Dodoma, Jeshi hilo limeeleza kuwa limebaini uwepo wa baadhi ya watu wanaotumia majukwaa mbalimbali ya mawasiliano kutoa kauli ambazo zinaweza kuchochea mgawanyiko na kuathiri mshikamano wa jamii.

Jeshi la Polisi limefafanua kuwa matamshi ya kuendeleza chuki, kuhamasisha migawanyiko au kuibua hisia zinazoweza kusababisha uvunjifu wa amani ni kinyume cha sheria na ni tishio kubwa kwa usalama na utulivu wa nchi.

Aidha, limesisitiza kuwa halitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mtu yeyote atakayejihusisha na matumizi ya lugha iwe laini au kali yenye viashiria vya uchochezi, likibainisha kuwa hatua hizo ni muhimu katika kudhibiti chuki na kuzuia vurugu ambazo zina madhara makubwa kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

“Tutaendelea kufanya kazi kwa umakini ili kuhakikisha amani inaendelea kutawala, hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inahitaji maridhiano ya kitaifa kurejesha utulivu.

“Ikizuka vurugu, athari zake ni pana na humgusa kila mwananchi katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kiusalama,” imesema taarifa hiyo iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini.