Swali la askofu Gwajima lajibiwa upya

Dodoma. Hatimaye Serikali imelijibu upya swali la Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima ambaye wiki iliyopita aligoma kuuliza swali la nyongeza akidai Serikali haikuwa imejibu swali lake la msingi.

Mei 31, 2024, Askofu Gwajima aliuliza swali akitaka kujua kuna mpango gani wa dharura wa kudhibiti mito inayopanuka na kuhatarisha maisha na mali za wananchi katika Jimbo la Kawe.

Akijibu swali hilo,  Naibu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais. Muungano na Mazingira, Khamis Hamza Khamis alisema Serikali imechukua hatua za dharura za kukabiliana na hali hiyo kwa Mkoa wa Dar es Salaam.

Jibu hilo halikumridhisha Gwajima na alipopewa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza na Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson, alikataa akisema:

“Mimi nimeuliza kuna mpango gani wa dharura wakudhibiti mito inayopanika na kuhatarisha maisha ya wananchi katika Jimbo la Kawe, lakini yeye anajibu Dar es Salaam. Kwa hiyo sitakuwa na swali (la nyongeza) na kama itakupendeza naomba lijibiwe tena baadaye,” alisema.

Swali hilo leo Juni 7, 2024, limejibiwa tena na Naibu waziri yuleyule, Khamis Hamza Khamis kuwa Serikali inatambua changamoto za mito kapanuka kutokana na mvua kubwa zilizonyesha.

Amesema Serikali imeanza kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni kutenga fedha katika bajeti.

“Katika bajeti ya mwaka wa fedha 24/25, Ofisi ya Makamu wa Rais imetenga Sh1 bilioni kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu utakaowezesha ujenzi kwa maeneo yatakayopendekezwa kwa Mkoa wa Dar es Salaam,”amesema.

Aidha, amesema Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni kwa kushirikiana na Bonde la Wami-Ruvu tayari imeingia mkataba na kampuni ya MEG Business Solution Limite tangu Aprili 19, 2024.

Amesema mkataba huo ulikuwa ni kwa ajili ya kusafisha tope, taka ngumu na kudhibiti mmomonyoko wa kingo za Mto Mbezi eneo la Ukwamani Mzimuni pamoja na ufukwe uliopo mtaa wa Mbezi A Kata ya Kawe.

Hivyo, amesema kukamilika kwa kazi hizo kutachangia kudhibiti kupanuka kwa Mto Mbezi katika Kata ya Kawe.

“Natoa wito kwa Serikali za mitaa kote nchini kusimamia kikamilifu Sheria ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 ili kuzuia shughuli za kibinadamu,” amesema.

Amezitaja shughuli hizo ni kama vile uchimbaji wa mchanga usiofuata utaratibu na kuelimisha jamii juu ya utunzaji wa mazingira ili kudhibiti upanukaji wa mito na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Viti Maalumu Mariam Kisangi amesema mito iliyoko Dar es Salaam imeathirika na changamoto hiyo na kusababisha baadhi ya  nyumba kubomoka, maeneo ya wazi kujaa maji na kusababisha magonjwa kwa wananchi.

KLutokana na hali hiyo, amehoji Serikali ina mpango gani wa muda mrefu na mfupi badala ya kusubiri bajeti ambayo inahusisha na maeneo mengine.

Akijibu swali hilo, Khamis amesema watakapopata fedha hizo watakwenda kuanza upembuzi yakinifu.

“Lakini kama nivyoeleza, tayari tumeshaingia makubaliano na makubaliano hayo yanakwenda kuanza haraka sana mwaka huu, uendelee kuwa Subira, Serikali inatambua changamoto hizo,” amesema.