Wamorocco wamtibulia Aucho | Mwanaspoti

KUNA pigo moja kubwa ambalo Singida Black Stars imelipata wakati ikijipanga kuanza mechi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria inayopigwa usiku wa leo ugenini lililosababishwa na Wamorocco kwani wanamkosa kiungo muhimu, Khalid Aucho.

Singida itakuwa Algeria leo saa 4 usiku katika mechi ya ufunguzi wa Kundi C la michuano hiyo ya kwanza kwao kihistoria tangu klabu hiyo ianzishwe, lakini hadi sasa ni Aucho pekee ndiye itakayemkosa kutokana na kuponzwa na siasa za Morocco na Algeria.

Iko hivi. Aucho ameponzwa na mvutano wa kisiasa uliopo kati ya Morocco na Algeria ambao umemzuia kiungo huyo mkongwe raia wa Uganda kupata visa ya kuingia nchini humo kwa wakati.

Aucho alikuwa Morocco ambako Uganda ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya taifa hilo Novemba 18 na kupoteza kwa mabao 4-0 ambao kiungo huyo alicheza kwa dakika 90.

AU 01

Hata hivyo, Aucho asingeweza kupata visa ya kuingia Algeria akiwa Morocco kutokana na mzozo mkubwa uliopo kati ya mataifa hayo mawili na kulazimika kurejea Tanzania ili aweze kupata visa.

Hadi jana, bado kulikuwa na uwezekano mdogo wa Aucho kuwahi mechi hiyo, lakini taarifa njema kwa Singida ni kwamba, kipa namba moja Amas Obasogie na kiungo mshambuliaji Andrew Phiri upande wao mambo yameenda freshi kwa kuliwahi pambano hilo la ugenini.

“Hakuna uhakika kamili kama (Aucho) atawahi, yaani hata akija anaweza kufika saa chache kabla ya muda wa mechi, tulishajiweka katika mazingira ya kwamba tutamkosa,” alisema bosi mmoja wa juu wa Singida BS na kuongeza;

“Tumeshusha presha baada ya kuwapokea Obasogie na Phiri ambao nao tuliwaacha nyuma kwa kuwa walikuwa wanasubiri visa ila zao ziliwahi kutoka na wakaanza safari haraka.”

Obasogie na Phiri nao walichelewa kupata visa, lakini waliwahi kurejea nchini wakitoka katika timu za mataifa yao ambapo juzi waliwahi Algeria na jana walifanya mazoezi na wenzao.

AU 02

Kama Singida itamkosa Aucho, basi kocha Miguel Gamondi atalazimika kuelekeza hesabu zake kwa viungo wakabaji wawili Mohammed Damaro na Khalid Habib ‘Gego’ ambao wamesafiri na timu hiyo.

Singida inatarajiwa pia kukutana na AS Otoho ya Congo Brazzaville na Stellenbosch ya Afrika Kusini, iliyotolewa nusu fainali ya michuano hiyo msimu uliopita na Simba kwa kufungwa bao 1-0 na kuifanya Simba kutinga fainali iliyopoteza kwa RSD Berkane ya Morocco kwa mabao 3-1.