Dar es salaam, Novemba 20, 2025 — Benki ya Stanbic imekabidhi msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 25 kwenye Kituo cha Afya Goba jijini Dar es salaam , ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kusaidia kuboresha huduma za afya nchini.
Msaada huo, unaojumuisha vifaa vya Unit suction machine 1, Patient Monitor 1, Oxygen Concentrator 1, Roll cloth cotton 3, Unit manual vacuum aspirator 2, Vishkwambi (Tablets 3, TV1, Kompyuta za mezani 2 na Armored cable 1 ulikabidhiwa na Meneja wa kanda Benki ya Stanbic k, Bi. Edditrice Marco kwa niaba ya benki hiyo, na kupokelewa na Mganga Mfawidhi wa kituo cha Afya Goba, Dkt Elias Ndahani na kushuhudiwa na mgeni rasmi, Afisa Tarafa ya Kibamba, Beatrice Mbawala.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya makabidhiano, Meneja wa Stanbic Kanda, Bi. Edditrice Marco alisema kuwa msaada huo kutoka tawi letu la Industrial branch ni sehemu ya mpango endelevu wa uwajibikaji wa kijamii wa Benki ya Stanbic unaolenga kurudisha fadhila kwa jamii, sambamba na maadhimisho ya Miaka 30 ya Kukua Pamoja tangu benki hiyo ianze kutoa huduma nchini Tanzania.
“Tunatambua mchango mkubwa wa sekta ya afya katika ustawi wa jamii. Kupitia msaada huu, tunalenga kusaidia hospitali na vituo vya Afya ili vitoe huduma bora zaidi kwa wagonjwa na kuongeza ufanisi wa watoa huduma. Hii ni moja ya njia tunazosherehekea miaka 30 ya kukua pamoja na Watanzania,” alisema Bi. Marco.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa kituo hicho Dk. Elias Ndahani, aliishukuru benki hiyo kwa mchango huo, akisema vifaa hivyo vitasaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa. Msaada huu umekuja wakati mwafaka kwa sababu kituo chetu ni kipya hivyo umegusa kila eneo hasa upande ule wa upasuaji utasaidia sana kuokoa maisha ya kinamama wakati wa kujifungua, na hizi mashine za kusaidia kupumua zitasaidia pia kuokoa maisha ya watoto wakati wanapopata changamoto.
Nae mgeni rasmi Afisa Tarafa ya Kibamba Beatrice Mbawala kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Ubungo, Mhe. Albert Msando alisema “Kituo hiki cha Afya hakiwalengi wakazi wa Goba pekee bali na maeneo ya jirani, hivyo basi niwasihi mganga mkuu na wauguzi muweze kulinda vifaa hivi ili kunufaisha wakazi wa Goba”. alisema. Aliongeza kusema “Benki ya Stanbic imetoa vifaa hivi vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 25 ni kiasi kikubwa sana cha pesa, wangeweza kutoa hata mikopo wapate faida lakini wakaona waje kwa jamii ili wasaidie hudumu ya afya na benki hii sio tu wanasaidia huduma ya afya pia wanasaidia sekta ya elimu, mazingira. Nipende kuwashukuru uongozi wa benki ya Stanbic Tanzania kwa moyo huu wa kujitolea”. Alisema Beatrice
