TANZANIA YAJIPANGA KUZALISHA BIDHAA ZITOKANAZO NA MADINI NCHINI

▪️Ni maelekezo ya Mhe.Rais Samia ya uongezaji thamani madini nchini

▪️Waziri Mavunde akagua ujenzi wa kiwanda cha kusindika na kuyeyusha madini ya Nikeli na Shaba

▪️Kiwanda kuanza uzalishaji Februari,2026

▪️Wachimbaji wadogo wapata soko la uhakika wa kuuza malighafi kiwandani

▪️Mradi kugharimu Bilioni 37

Dodoma

Tanzania yaendelea kupiga hatua katika Mpango wa ujenzi wa viwanda vya uongezaji thamani madini kutokana na ujenzi wa kiwanda kipya cha usindikaji  na uyeyushaji madini ya Nikeli na Shaba kufikia asilimia 85 ya ujenzi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Mhe.Rais .Dkt.Samia Suluhu Hassan yanayoelekeza kuwa shughuli za uongezaji thamani madini kufanyika ndani ya nchi kabla ya kusafirishwa nje.

Hayo yameelezwa leo Novemba 21, 2025 na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde wakati anakagua kiwanda cha kusindika  na kuyeyusha madini ya Nikeli na Shaba kilichopo eneo la Mayamaya , Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.

Mhe.Mavunde amesema kuwa, kiwanda kitawasha mtambo wake wa kwanza wa uzalishaji ifikapo mwezi Februari, 2026 ambapo mtambo huo utachakata tani 300 za mashapo kwa siku.

Akielezea kuhusu gharama za uwekezaji katika kiwanda hicho, Mhe. Mavunde amesema kuwa uwekezaji huu ni mkubwa utakapo kamilika utagharimu shilingi bilioni 37, hivyo amewataka wachimbaji wadogo wa madini nchini  kutumia fursa hiyo ya soko la uhakika  kupeleka malighafi katika kiwanda. 

Akifafanua kuhusu malengo ya kujenga viwanda vya uchakataji na uongezaji thamani madini , Mhe.Mavunde amefafanua kuwa shabaha kubwa ni kuhakikisha Tanzania inakamilisha mnyororo wote wa thamani madini kuanzia uchimbaji mpaka uchakataji na uongezaji thamani ili kusafirisha nje ya nchi  bidhaa zitokanazo na rasilimali madini badala kusafirisha  madini ghafi  kama ilivyokuwa awali.

Kwa upande wake,  Mkuu wa Wilaya ya  Bahi Mhe. Joachimu Nyingo amesema kuwa,  anaipongeza Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupeleka wawekezaji wa madini mkoani Dodoma, jambo linalopelekea kufikia viwanda 9 vya uongezaji thamani madini.

Naye , msimamizi wa kiwanda hicho Hassan Ngaiza ameeleza juu ya faida mbalimbali za kiuchumi na kijamii zitaletwa na kiwanda hicho ikiwa pamoja na ajira zaidi ya 300 ambazo za kudumu na zisizo za kudumu, masoko  ya malighafi madini pamoja  na bidhaa nyingine.

Pamoja na mambo mengine, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Metali Tanzania Thobias Kente, ameushukuru uongozi wa kiwanda cha Zhong Zhou kwa juhudi kubwa inayofanya kuhakikisha kuwa  kiwanda kinakamilika kwa wakati, jambo ambalo litawezesha wachimbaji wadogo wa madini ya metali kupata soko la uhakika la madini ghafi wanayochimba nchini.