Tato wataka ubunifu katika kufikia malengo ya utalii nchini

Arusha. Chama cha Waendesha Utalii Tanzania (Tato) kimewataka wanachama wake kuzingatia ubunifu katika uendeshaji wa biashara ya utalii ili kukabiliana na changamoto za kisekta na kuchochea uchumi wake.

Kwa mujibu wa Serikali, kwa sasa Tanzania inatembelewa na watalii zaidi ya milioni 5.3 kwa mwaka na kuingiza mapato ya Dola za Marekani 4 bilioni huku ikilenga kufikia watalii milioni 8 ifikapo mwaka 2030.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 42 wa Tato uliofanyika Arusha Novemba 21, 2025, Mwenyekiti wa Tato, Wilbard Chambulo amesema sekta ya utalii inahitaji ubunifu wa kila wakati ili kuendana na mabadiliko ya mahitaji ya soko na teknolojia inayokua kila siku.

“Ubunifu tunaozungumzia hapa unalenga kutoa huduma za utalii zenye ubora wa hali ya juu na kuvutia kwa masoko ya ndani na kimataifa huku tukikazia pia utangazaji wa bidhaa zetu za utalii.

“Waendeshaji utalii hawawezi kuongeza mapato ya watalii bila ubunifu. Ni muhimu kuhakikisha wageni wanatumia muda mwingi kutembelea nchi yetu,” amesema Chambulo mbele ya wanachama zaidi ya 150 walioshiriki mkutano huo.

Ameongeza kuwa: “Badala ya siku mbili au tatu tu, watalii wanapaswa kufurahia ratiba ya siku tano hadi sita. Zaidi ya yote, tunapaswa kuepuka kuwafanyia haraka katika vivutio vikubwa; badala yake, tuwaelezee vivutio muhimu huku tukionyesha pia maeneo mengine ambayo bado hawajatembelea, ili kuhamasisha watalii kurudi Tanzania tena.”

Mjumbe wa Bodi ya Tato, Rahma Ally Adam, amesema kuwa Mkutano Mkuu unatoa jukwaa kwa wadau kushughulikia changamoto, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano kwa lengo la kukuza biashara ya utalii.

“Mkutano huu unawaleta pamoja wanachama wote wa Tato kujadili changamoto na mafanikio ya sekta ya utalii, kubadilishana mawazo juu ya namna ya kutoa huduma zinazoshindana kwenye masoko ya ndani na kimataifa, na kuimarisha uhusiano kati ya waendeshaji utalii na Serikali, kuhakikisha ukuaji wa sekta na kuzalisha mapato,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Precision Air, Patrick Mwanri amesema mchango wa miaka 30 wa shirika hilo katika sekta ya utalii ni mkubwa kwa kuhakikisha usafiri salama wa abiria wanaoingia na kutoka nchini.

“Tunashirikiana na Tato kutafuta njia za kuimarisha ushirikiano na kukuza Tanzania kama destination ya utalii ya kiwango cha juu. Kama nchi nyingine zinavyouza vivutio vyao kwa ufanisi, lazima tushirikiane katika mnyororo mzima wa thamani ya utalii,” amesema Mwanri.

“Leo, tumejadili changamoto zinazokabili sekta na jinsi tunavyoweza kushirikiana kuhakikisha ukuaji wake unaendelea. Precision Air inahudumia wadau wengi wanaosafiri mara kwa mara, kwa hivyo ni muhimu kuona sekta ikisonga vizuri.”

“Tunawaasa wadau wote kushirikiana, kuepuka ubinafsi, na kuwezeshana,” amebainisha.

Ametumia nafasi hiyo kuiomba Serikali itafakari upya kodi na ushuru unaolipishwa kwenye utalii, ikiwemo huduma za ndege, waendeshaji utalii na hoteli.

“Ada kubwa inaweza kuzuia watalii na kuathiri malengo yetu ya kufikia watalii milioni 8 ifikapo 2030 kwani tozo hizo huwa zinafaulishwa kwa watalii ambao wataona wachague pa kwenda,” amesema.

Mkuu wa Biashara wa NMB Bank, Alex Mgeni amesema dhamira ya taasisi hiyo ni kusaidia wadau wa utalii kifedha ili kusaidia sekta kufikia malengo yake.

“Tumeshiriki mkutano huu si tu kama wanachama halali bali pia kama mshirika muhimu wa kifedha kuunga mkono ukuaji wa sekta ya utalii Tanzania,” amesema Mgeni.

“NMB inaendelea kutoa suluhisho za kuimarisha shughuli za utalii, ikiwa ni pamoja na mikopo ya ununuzi wa magari ya kusafirisha watalii, ujenzi wa hoteli, na ujenzi wa mabanda na tents za malazi kwa wageni.

“Zaidi ya hayo, tumetoa ESME Business Debit Card, kadi inayowawezesha wafanyabiashara kuunganisha akaunti zao za biashara kwa malipo mtandaoni na POS, kadi hii inatoa huduma ya VIP lounges, bima ya mizigo na punguzo maalumu kwenye safari,” amebainisha.

Mgeni amewahimiza wafanyabiashara nchini kutumia huduma hizi kupitia matawi 240 ya NMB nchini, ikiwa ni pamoja na kufungua akaunti za biashara ili kufaidika na ATM na urahisi wa malipo wakati wa usafiri.