Usimamizi sahihi wa fedha watajwa kuimarisha uwajibikaji serikalini

Dodoma. Usimamizi makini wa masuala ya fedha umeelezwa kuwa nguzo muhimu katika kupunguza malalamiko, kuzuia mianya ya ubadhirifu na kuimarisha uwazi na uwajibikaji ndani ya taasisi za umma.

Hayo yamesemwa leo, Novemba 21, 2025, jijini Dodoma na Jaji Mstaafu Hamisa Kalombola, wakati akizindua Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Umma, kilichofanyika katika Makao Makuu ya Ofisi za Sekretarieti ya Maadili.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Jaji Kalombola amesema kuwa usimamizi sahihi wa fedha si tu ni sharti la kisheria, bali pia ni hatua muhimu katika kujenga taasisi zinazojitegemea, kuaminika na zinazojibu mahitaji ya wananchi.

“Usimamizi wa masuala ya fedha ni jambo muhimu sana linapofanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu kwani hii inatusaidia kupunguza malalamiko, migogoro na kudhibiti mianya ya ubadhirifu, sambamba na kujenga tabia ya uwazi na uwajibikaji wa pamoja.”

Aidha, amewahimiza wajumbe wa baraza hilo kushiriki kikamilifu katika kupitia taarifa za utekelezaji wa bajeti, kujadili na kutoa hoja zenye lengo la kuimarisha utendaji wa tume.

Wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Umma wakifuatilia Hotuba ya Jaji Mstaafu Hamisa Kalombola, katika  uzinduzi wa Kikao cha Baraza Jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha

“Ninawahimiza washiriki wote kutoa maoni, mapendekezo na changamoto zenu. Kila sauti ina thamani, na kila mchango una nafasi ya kuboresha mwelekeo wa taasisi yetu,” amesisitiza.

Hata hivyo, amesema kuwa uongozi wa Tume ya Utumishi wa Umma upo tayari kupokea mawazo, kujadili na kufanya maboresho pale inapohitajika ili kuhakikisha bajeti inakwenda sambamba na vipaumbele vya taasisi na matarajio ya wananchi wanaotegemea huduma zake.

Kikao hicho cha Baraza la Wafanyakazi kinatarajiwa kujadili mambo mbalimbali yahusuyo bajeti, utekelezaji wa majukumu ya tume na maboresho ya kimfumo katika kujenga utumishi wa umma wenye tija zaidi.