KABLA ya kuanza kwa mazoezi ya kikosi cha Yanga jioni ya leo, Ijumaa, Novemba 21, 2025, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex hapa Zanzibar, kocha mkuu, Pedro Goncalves raia wa Ureno amefanya kikao cha dharura na nyota watatu.
Kikao hicho kilichofanyika kwa takribani dakika moja kilimhusisha Pedro na mastaa Mudathir Yahya, Duke Abuya na Maxi Nzengeli.
Nyota hao ambao wamekuwa wakicheza kikosi cha kwanza, wanaunda safu ya kiungo ambapo Abuya na Mudathir ni viungo wa kati, wakati Maxi akicheza pembeni.
Mwanaspoti limeshuhudia kikao hicho kifupi kilichoanza mara baada ya kumalizika mazungumzo ya pamoja baina ya viongozi wa benchi la ufundi na wachezaji.
Wakati wachezaji wengine na maofisa wa Yanga wakitawanyika kuanza program za mazoezi, Pedro aliwabakisha viungo hao na kuzungumza nao kwa msisitizo.
Baada ya kikao hicho kumalizika, Pedro alimuita meneja, Walter Harrson na kuzungumza naye huku viungo hao wakiungana na kocha msaidizi, Patrick Mabedi kufanya mazoezi binafsi ya kuzunguka uwanja mizunguko mitatu, kisha kuungana na wenzao katika mazoezi ya jumla.
Yanga imefanya mazoezi ya mwisho Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kujiandaa na mechi ya kwanza Kundi B ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS FAR Rabat itayakayochezwa kesho Jumamosi, Novemba 22, 2025 uwanjani hapo.
Asubuhi ya leo katika mkutano na waandishi wahabari, Pedro amesema: “Kikosi changu ni kweli kina viungo wengi takribani nane ambao wote wapo vizuri, naamini wana uwezo mkubwa wa kupambana na wapinzani wetu kufanya vizuri hapo kesho. Tutaandaa mikakati ya kukabiliana nao ingawa hapa siwezi kuuza siri zangu.”
