DC Naano aagiza kukamatwa kwa wanaotatiza usambazaji wa mbegu za pamba

Maswa. Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano ameagiza Jeshi la Polisi kuwakamata viongozi wote wa Vyama vya Msingi (Amcos) wanaotuhumiwa kuhujumu usambazaji wa mbegu za pamba kwa msimu wa kilimo 2025/2026.

Agizo hilo limetolewa Novemba 21,2025  wakati serikali wilayani Maswa mkoani Simiyu, ikizindua rasmi msimu mpya wa kilimo cha zao la pamba, huku wakulima wakilalamikia upungufu mkubwa wa mbegu licha ya Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) kusambaza kilo 1,500,000.

Akizungumza katika kijiji cha Dodoma kilichoko Kata ya Mwamashimba wilayani humo amesema serikali haitavumilia wizi wa mbegu za pamba unaofanywa na baadhi ya viongozi wa Amcos katika musimu huu wa kilimo.

Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dk Vicent Naano akizungumza wakati wa kufungua musimu wa kilimo cha pamba mwaka 2025/2026 wilayani humo katika kijiji cha Dodoma.Picha na Samwel Mwanga

“Kila jioni Mratibu wa pamba wa wilaya nipate taarifa ya Amcos iliyofanya hujuma. Wote wakamatwe, hakuna kuachiwa. Wizi kwenye Amcos hatutauvumilia,” amesema.

Dk Naano ameonya kuwa Serikali haitavumilia uendelevu wa vitendo vya wizi na udanganyifu kama vilivyowahi kujitokeza misimu iliyopita, ikiwemo kuibia wakulima kupitia mizani.

Imeelezwa kuwa mahitaji halisi ya mbegu kwa wilaya hiyo ni kilo 2,021,900, hivyo kuacha upungufu wa kilo 521,900 ambao umewafanya wakulima wengi kukosa mbegu za kuanzisha kilimo kwa wakati.

Mkulima wa kijiji cha Dodoma Maduhu Jilala, amesema kuwa upungufu na ucheleweshaji wa mbegu umekuwa ukirudisha nyuma uzalishaji wa pamba kila msimu.

“Mbegu zilizogawiwa ni chache. Tumepokea tani 15 kwa wakulima 411, lakini kijiji kina kaya 900. Wakulima wengi hawajapata mbegu, tunaomba tusaidiwe kuongezewa haraka,” amesema.

Kwa upande wake, Judith Fabian wa kijiji cha Buyubi alisema baadhi ya wakulima wanakosa mbegu kutokana na kukwama katika mfumo wa usajili unaohitaji kitambulisho cha taifa.

“Wakulima wengi majina hayapo kwenye orodha kwa sababu hawana vitambulisho. Hali hii inaturudisha nyuma,” amesema.

Mkaguzi wa TCB wilayani Maswa, Ally Mabrouk, alikiri kuwepo kwa upungufu wa mbegu na kubainisha kuwa baadhi ya viongozi wa Amcos wamekuwa wakiuza kinyemela kwa wakulima wa maeneo ya jirani.

Sehemu ya wakulima waliohudhuria siku ya uzinduzi wa musimu wa kilimo cha zao la pamba wa mwaka 2025/2026 katika wilaya ya Maswa katika kijiji cha Buyubi.Picha na Samwel Mwanga

“Tunapopeleka mbegu kwenye Amcos tunategemea zigawiwe kwa wakulima. Lakini baadhi ya viongozi wanauza kwa vijiji vya mpakani na kuwaacha wakulima wao bila mbegu. Hii inawanyonya wakulima,” amesema.

Aliongeza kwa kueleza kuwa tathmini inaendelea kufanywa ili kuhakikisha vijiji vyote vilivyo na upungufu vinapatiwa mbegu kwa wakati.

Afisa Kilimo wa Wilaya ya Maswa, Gimu Mabula amesema wilaya hiyo inalenga kulima hekta 40,438 na kuzalisha tani 40,438 za pamba msimu huu.

“Tunawapatia wakulima elimu ya kilimo bora na kuhakikisha pembejeo zinawafikia kwa wakati. Mbegu zinatolewa kwa mkopo kwa Sh1,400 kwa kilo, sawa na Sh24,000 kwa mfuko wa kilo 20 unaotosheleza ekari mbili,” amesema.

Kwa sasa, ugawaji wa mbegu unaendelea katika vijiji vyote vya wilaya ya Maswa huku serikali ikisisitiza usimamizi madhubuti ili kuhakikisha mbegu zinawafikia walengwa na kuongeza tija ya uzalishaji wa zao hilo muhimu kwa uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.