Simanjiro. Jumla ya madiwani wateule 10 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamejaza fomu za kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, huku wengine saba wakijitokeza kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Baraka Kanunga, hatashiriki katika kinyang’anyiro hicho baada ya kupoteza katika kura za maoni za CCM kwa mpinzani wake katika nafasi ya udiwani wa Kata ya Komolo, Saning’o Somi.
Akizungumza Novemba 21, 2025, Katibu wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Igembya Wambura amethibitisha kuwa wagombea hao wamewasilisha fomu za kuomba uteuzi kwa nafasi hizo, hatua inayoashiria mchakato wa uchaguzi wa uongozi wa halmashauri kuingia katika hatua muhimu.
Wambura amewataja madiwani wateule walioomba nafasi ya uenyekiti kata zao kwenye mabano ni Albert Msole (Ngorika), Jackson Ole Materi (Terrat), Taiko Laizer (Naisinyai), Loth Yamat (Edonyongijape) na Ezekiel Lesenga (Loiborsiret).
Amewataja madiwani wateule wengine waliojaza fomu za kuomba uenyekiti ni Soningo Somi (Komolo), Kaleiya Mollel (Msitu wa Tembo), Yohana Shinini (Emboreet) Elibariki Mollel (Orkesumet) na Zakayo Michael (Kitwai).
Wambura amesema baadhi ya waliochukua fomu ya kugombea makamu mwenyekiti na kata zao kwenye mabano ni Marco Munga (Naberera), Julius Lemboi (Shambarai), Mwanjaa Jacob (viti maalum), Rehema Laizer (viti maalum) na Elibariki Mollel (Orkesumet).
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya pamoja na meya wa mji au jiji hutumikia nafasi zao kwa kipindi cha miaka mitano, huku makamu mwenyekiti akihudumu kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa mujibu wa utaratibu wa ndani wa halmashauri.
Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro ina jumla ya kata 18, ambazo zote zimepata madiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Simanjiro wamezitaka kamati za uteuzi kutumia hekima na busara katika mchakato wa kupendekeza majina ya wagombea, wakisisitiza umuhimu wa kurejesha majina madhubuti hata kama ni mmoja au watatu watakaoweza kuongoza halmashauri hiyo kwa ufanisi.
Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, John Steven, amesema kwa sasa Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya, anahudumu kama Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, hivyo mwenyekiti ajaye anapaswa kwenda sambamba na kasi yake ya uwajibikaji.
“Tunahitaji Mwenyekiti mwenye uwezo mkubwa, uzoefu na elimu ya kutosha ili kuepuka migogoro isiyo na tija na kuzingatia jambo moja tu maendeleo,” amesema Steven.
Naye mkazi wa Kata ya Loiborsiret, Neema Mollel, amesema anatarajia vikao vya CCM ngazi ya wilaya, mkoa na taifa vitapitisha majina sahihi ya wagombea kulingana na sifa walizonazo.
Amesema wagombea wana uwezo tofauti, hivyo madiwani waliowahi kuhudumu, wanaoonyesha uadilifu, nidhamu na rekodi nzuri ya utendaji, wanapaswa kupewa kipaumbele katika mapendekezo yao ili kugombea nafasi hiyo kupitia CCM.
