Hatima umeya, uenyekiti mikononi mwa kamati za siasa wilaya, mikoa

Dar/Dodoma. Uamuzi wa majina matatu kati ya kadhaa waliochukua fomu kuomba ridhaa ya umeya na naibu meya wa manispaa na majiji iko mikononi mwa vikao vya Kamati za Siasa za mikoa na wilaya za Chama cha Mapinduzi (CCM).

Hiyo ni baada ya leo saa 10 alasiri, kufungwa kwa dirisha la uchukuaji na urejeshaji fomu za kuomba nafasi hiyo na leo Novemba 21, 2025, na kesho vinaanza vikao vya kamati za siasa za wilaya nchi nzima kuchambua na kupendekeza majina kwa vikao vya juu.

Vikao hivyo ngazi ya wilaya vitafuatiwa na vikao vya kamati za siasa za mikoa Novemba 23, 2025 ambavyo navyo vitafanya kazi ileile ya kuchambua na kupendekeza majina ya waliochukua fomu kwa vikao vya juu.

Vikao hivyo ndivyo vitakavyoamua majina matatu yatakayopelekwa katika vikao vya kitaifa kwa ajili ya mchujo, kisha kamati za madiwani zitakazopiga kura na kutoka na jina moja litakaloingia kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi.

Tofauti na miaka mingine, mchuano wa umeya mwaka huu, unaonekana kuwakutanisha mameya wanaotetea nafasi zao na waliokuwa wasaidizi wao, yaani naibu mameya wastaafu, kadhalika wenyeviti wa halmashauri.

Siyo hivyo tu, katika kinyang’anyiro hicho cha mwaka huu, kumeshuhudiwa idadi kubwa ya madiwani waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ya umeya.

Ratiba ya vikao vya uteuzi

Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya CCM, vikao vya kamati za siasa za wilaya vitafanyika Novemba 22, kuchambua na kupendekeza majina kwa mamlaka za juu.

Hatua hiyo, itafuatiwa na kikao cha kamati za siasa za mikoa nchi nzima, zitakazoketi Novemba 23. Zenyewe pia zitatoa mapendekezo yao kwa majina matatu kwa vikao vya juu.

Vikao hivyo vitafuatiwa na Sekretarieti ya Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar ambayo pia itafanya mchujo wa majina kwa upande wa visiwa hivyo.

Novemba 25, chanzo hicho kimeeleza kwamba kitafanyika kikao cha Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar na itakamilisha mapendekezo yake ya majina ya waliochukua fomu.

Novemba 27 na 28, chanzo hicho, pia, kimeeleza kuwa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM, itaketi jijini Dodoma kufanya uchambuzi wa majina nchi nzima.

Baada ya sekretarieti, itafuatiwa na Kamati Kuu itakayoketi Novemba 29, 2025 kwa ajili ya kufanya uteuzi wa wagombea kati ya majina yaliyopendekezwa.

Baada ya uteuzi, Novemba 30, 2025 vitafanyika vikao vya kamati za madiwani wa CCM katika halmashauri za miji na wilaya kuwatambua waliopitishwa.

Siku hiyo hiyo, amesema zitapigwa kura kupata jina moja kati ya yaliyopendekezwa, litakalokwenda kushindana katika kinyang’anyiro cha uchaguzi rasmi wa meya.

Akizungumzia kinyang’anyiro hicho katika Wilaya ya Ubungo, Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Henry Mwenge amesema uchukuaji na urejeshaji fomu hizo, utatakamilika saa 10 jioni ya Novemba 21, 2025.

Hadi alipokuwa anazungumza na Mwananchi, saa 6:20 mchana, Mwenge amesema tayari wanachama tisa wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania umeya huku watatu wakijitokeza kuwania unaibu meya.

“Ni vigumu kuweka hadharani majina yao, lakini kwa sasa nachoweza kukwambia ni idadi ya waliochukua fomu. Tunaogopa kutaja majina kwa sababu za kiusalama na kiitifaki,” amesema.

Mmoja wa waliochukua fomu kuwania nafasi hiyo wilayani Ilala, amesema katika Wilaya ya Ilala, madiwani 10 wamejitokeza kuwania nafasi hiyo na miongoni mwao wapo watu mashuhuri.

Kwa sababu utaratibu wa chama hicho ni vikao, amesema hana mashaka kwamba vitafanyika na kutoa nafasi kwa wenye sifa stahiki na wanaofaa kwenda hatua zinazofuata.

“Mwisho wa siku chama kina mifumo yake na vikao ndivyo vitakavyoteuwa majina na kisha watapigiwa kura na mabaraza ya madiwani,” amesema.

Hata hivyo, amesema katika wilaya hiyo huenda kukawa na mchuano mkali kati ya meya anayemaliza muda wake, Omar Kumbilamoto dhidi ya sura mpya zilizojitokeza kuwania nafasi hiyo.

Amesema meya huyo mstaafu naye atachuana na aliyekuwa msaidizi wake diwani wa Ilala, Saady Khimji ambaye pia amechukua fomu kuwania nafasi hiyo.

Alipotafutwa kuzungumzia mchakato huo, Kumbilamoto amesema yupo katika harakati za kwenda kuchukua fomu hiyo ili ajitose kuomba ridhaa ya kutetea nafasi yake.

Kwa upande wa Wilaya ya Kinondoni, Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Jacob Siayi amesema hadi muda anazungumza na Mwananchi saa 5:30 asubuhi, jumla ya madiwani saba walijitokeza kuchukua fomu.

Idadi ya Madiwani waliojitokeza kuwa nafasi za Meya na Wenyeviti wa Halmashauri za Wilaya umeleta picha ya ushindani katika nafasi hizo maeneo mengi nchini.

Madiwani wenye ushawishi na uwezo wa kiuchumi baadhi yao wamechukua fomu hizo katika uchaguzi unaotarakia kufanyika hivi karibuni ndani ya vyama.

Kwa upande wao CCM leo Novemba 21,2025 walifungua pazia kwenye wenye nia ya kugombea umeya na naibu meya kwa majiji na manispaa na kwa halmashauri ni wenyeviti na makamu wenyeviti.

Baadhi ya madiwani wenye ushawishi na uwezo wa kiuchumi wamechukua fomu hizo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni ndani ya vyama.

Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa David Mwamfupe amechukua fomu leo ambapo atapambana na ushindani mkali kutoka kwa Kamuli Gombo (Ipagala), Theobas Maina (Ntyuka) na diwani Sadick Mponyamili wa Kata ya Iyumbu huku ikielezwa wapo na wengine waliochukua fomu kuomba nafasi hiyo.

Hata hivyo, Profesa Mwamfupe amekuwa na bahati ya mtende ndani ya CCM kwani mara kadhaa kwenye chaguzi zilizopita, chama hurudisha jina lake akiwa mgombea pekee baada ya kuwaondoa wengine.

Leo, amesema wingi wa waliogombea ni kipimo cha demokrasia akisisitiza kuwa chama kitatenda haki na mwisho madiwani wataamua nani wanataka kusafiri naye kwa miaka mitano.

Kwa upande wake, mwenyekiti aliyedumu muda mrefu kuliko wote katika Mkoa wa Dodoma, White Zuberi wa Kongwa, amepata wapinzani akiwemo diwani wa kata jirani yake, Elisha Kuta (Ugogoni).

Mwingine anayekitaka kiti hicho ni Diwani wa Kata ya Songambele, Peter Sadoki ambao inaelezwa kuwatakuwa na ushindani mkali kwa watatu hao.

Mwenyekiti wa Wilaya ya Mpwapwa aliyemaliza muda wake, George Fuime amesema hakuchukua fomu ya nafasi hiyo akitaja sababu kwamba ni zamu ya wenzao wa jimbo la Kibakwe.

Halmashauri ya Mpwapwa ina majimbo mawili ya Mpwapwa na Kibakwe na Fuime ni Diwani wa Kata ya Mpwapwa Mjini. Kwa sasa waliogombea ni aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Richard Mapondwa (Luhundwa) na Kayanda Mwanike wa Kata ya Chipogolo wote wanatoka Jimbo la Kibakwe.

Hadi leo asubuhi Diwani wa Lamaiti katika Wilaya ya Bahi, Donald Mejeti hakuwa amechukua fomu ya kuomba kutetea kiti chake na alipoulizwa alisema bado anatafakari.

Katibu wa CCM Wilaya ya Chamwino, Ibrahim Mpwapwa amesema madiwani wateule sita walikuwa wamechukua fomu kuomba nafasi ya mwenyekiti na wanne waliomba kiti cha makamu.

Mpwapwa amesema miongoni mwa walioomba nafasi ya Mwenyekiti, ni aliyekuwa makamu mwenyekiti kipindi kilichopita na Diwani wa Kata ya Buigiri Keneth Yindi.

“Kwa nafasi ya mwenyekiti amechomoza mwanamke mmoja anaitwa Dinna Meda kutoka Kata ya Makang’wa na nakamu yupo mwanamke mmoja, ila tusubiri muda ufike ndiyo tutajua,” amesema Mpwapwa.

Akizungumzia mchujo wa wagombea, amesema kwa mujibu wa ratiba waliyopokea kutoka Makao makuu, Novemba 22, 2025 nchi nzima kamati za siasa zinakutana na Jumapili ya Novemba 23, 2025 itakuwa ni kamati za siasa mikoa ndipo watapeleka vikao vya juu.

Aliyekuwa Naibu Meya wa Manispaa ya Singida, Ibrahim Murua amechukua fomu katika kiti ambacho kiko wazi kwani aliyekuwa meya kwa sasa ndiye Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini.

Kwenye Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Diwani wa Kata ya Dung’unyi, Gasper Silvery ndiye aliyejitokeza hadharani kueleza kwamba amechukua fomu ingawa wapo na wengine.

Imeandikwa na Bakari Kiango, Juma Issihaka na Habel Chidawali