Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amefanya uteuzi na kubadilisha makatibu wakuu wa wizara nane, pamoja na naibu makatibu wakuu wa wizara tano.
Miongoni mwa walioteuliwa wamo waliokuwa wakuu wa mikoa na watendaji wakuu wa taasisi za Serikali.
Katika uteuzi huo, makatibu wakuu wa wizara tisa wameendelea kusalia walipokuwa.
Wateule hao wataapishwa Jumamosi, Novemba 22, 2025 Ikulu Zanzibar, kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa Novemba 20, 2025 na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Zena Said.
Taarifa hiyo imesema aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mattar Zahor Masoud ameteuliwa kuwa katibu mkuu Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo.
Uteuzi huo unaifanya mikoa mitatu sasa kutokuwa na wakuu wake, baada ya wawili kuwa makatibu wakuu na mmoja waziri.
Hii ni baada ya Salama Mbarouk Khatib, aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, kuteuliwa kuwa katibu mkuu Waziri wa Vijana, Ajira na Uwekezaji.
Pia Dk Mwinyi Novemba 8 alimteua Idrissa Kitwana Mustafa, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, kuwa Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ.
Kwenye uteuzi huo wa jana, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk Rahma Salim Mahfoudh ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, huku Saleh Mohamed Juma, akiteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo. Saleh alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Serikali wa huduma za matrekta na zana nyingine za kilimo.
“Ali Said Bakari ameteuliwa kuwa katibu mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, kabla ya hapo alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe,” inaeleza taarifa hiyo.
Rais Mwinyi amemuhamisha Fatma Mabrouk Khamis kutoka Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda kwenda Wizara ya Mawasiliano, Tekenolojia ya Habari na Ubunifu.
Khamis Suleiman Mwalimu amehamishiwa Wizara ya Kazi na Uwekezaji akitokea Wizara ya Ofisi ya Rais, Kazi Uchumi na Uwekezaji, huku Dk Habiba Hassan Omar akihamishiwa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda akitokea Wizara ya Ujenzi, Mawaliano na Uchukuzi.
Katika taarifa hiyo, Mohamed Dhamir Kombo ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kutoka nafasi ya Mkurugenzi Idara ya Kilimo na Uhakiki wa Chakula.
Amos John Enock, ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kabla ya uteuzi huo alikuwa Ofisa Elimu Mkoa wa Mjini Magharibi.
Rashid Ali Salum amehamishwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kazi na Uwekezaji, awali alishika wadhifa huo katika Wizara ya Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji.
Makame Machano Haji, ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, akitokea Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi.
“Khalid Masoud Waziri ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Vijana, Ajira na Uwekezaji akitokea Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali,” inaeleza taarifa.
Makatibu waliobaki kwenye nafasi zao
Mansura Mosi Kassim, amebakia kwenye nafasi yake ya Katibu Mkuu Wizara ya Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, huku Saleh Juma Mussa, akisalia Ofisi ya Rais Ikulu.
Issa Mahfoudh Haji, amebakia kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Tawala Za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, huku Joseph John Kilanga akiendelea na Wizara ya Maji, Nishati na Madini.
Islam Seif Salum anabaki kuwa katibu mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi na Mariam Juma Sadalla akiendelea na Wizara ya Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais.
Khadija Khamis Rajabu anasalia Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi sawa na Khamis Abdulla Said, anayeendelea kuhudumu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali. Mwingine ni Dk Mngereza Miraji Mzee, anayesalia Wizara ya Afya.
Omar Haji Gora na Mzee Ali Haji wanaendelea kuhudumu nafasi ya naibu katibu mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, huku Aboud Hassan Mwinyi akiendelea Wizara ya Fedha na Mipango.
Mwanajuma Majidi Abdalla anaendelea kuhudumu Wizara ya Maji, Nishati na Madini sawa na Mikidad Mbarouk Mzee katika Wizara ya Tamisemi.
Salhina Mwita Ameir anaendelea na wadhifa huo Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na Dk Mwanakhamis Adam Ameir amebakia katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.
Muhaza Gharib Juma amebaki Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi na Zahor Kassim Mohamed akiendelea kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi
Khatib Mwadin Khatib ameendelea kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto.
Wakizungumza na Mwananchi kuhusu uteuzi huo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa na utawala bora, wamesema kuna mchanganyiko ambao huenda Rais ameona kasi anayotaka kwenda nayo ndio wataiweza.
Mchanbuzi wa siasa Zanzibar, Ali Makame amesema uteuzi ni mamlaka ya Rais, kwa hiyo yeye ndiye anajua watu wanaoweza kufanya kazi katika viwango anavyotaka.
“Wapo ambao tunawafahamu walikuwa watendaji wazuri katika nafasi walizokuwa nazo, kwa hiyo kuwekwa katika nafasi za ukatibu mkuu ni dhahiri watakwenda kuleta mabadiliko kwenye wizara,” amesema na kuongeza:
“Ukiangalia utaona kuna mchanganyiko mzuri tuseme nusu kwa nusu, waliobaki na walioteuliwa hapa ni kwenda kubadilishana uzoefu.”
Kwa upande wake, Burhan Haji amesema uteuzi huo umelenga kuzingatia kasi ambayo ameitaja baada ya kuingia tena madarakani muhula wa pili.
Hata hivyo, amesema kuna kazi kubwa ipo mbele ya wateule hao ikizingatiwa kauli ya Rais kwamba anataka kasi kubwa zaidi ya ile iliyokuwapo awali.
“Ni mabadiliko ambayo nadhani yanalenga kuleta maendeleo zaidi, unaona kuna wakuu wa mikoa ambao kimsimgi wamefanya vizuri katika mikoa yao sasa amewapa wakawe watendaji wakuu wa wizara, hii inaonyesha jinsi mkuu wa nchi anavyotaka kuona matokeo,” amesema.
