MSAMA ATOA KAULI NZITI AKIWASIHI GEN-Z, VIONGOZI WA DINI


 ::::::::::

MKURUGENZI wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama amesema kilichotokea Oktoba 29, kisijirudie na watanzania wote tuseme inatosha kwani sio utamaduni wetu

Msama amesema hayo leo wakati akitoa maoni yake kuhusu tume iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuchunguza matukio ya vurugu za Oktoba 29, siku ya uchaguzi mkuu mwaka huu.

Tume hiyo inayoogozwa na Jaji Mkuu Mstaafu, Othoman Chande, ilizinduliwa na Rais Samia, katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, mjini Dodoma.

Vurugu hizo ambazo hadi leo lengo lake hazijulikani, zimesababisha vifo, uharibifu wa miundombinu, mali za Serikali na watu binafsi . 

Msama ambaye alikuwa mgombea Ubunge jimbo la Ukonga (CCM), alisema huu sio muda wa kunyoshena kidole kwamba nani alikosea na nani alikuwa sahihi bali ni wakati wa kutafakari na kusema imetosha.

Kwa mujibu wa Msama, Rais Samia anastaili pongezi kwa hatua anazochukua kwani ameshatoka hadharani  kutoa pole kwa wafiwa, majeruhi, wananchi na wafanyabashara waliopoteza mali zao na ameunda tume kuchunguza matukio hayo ya Oktoba 29

“Kila mmoja ameona kilichotokea Oktoba 29, mimi naamini kila mtu ameona tulipokosea, vijana walioandamana na kuleta vurugu, wamejifunza kitu, viongozi wetu wamejifunza kitu, sisi wananchi na wazazi, tumejifunza tulipokosea. Sasa ni wakati wa kusema inatosha, yaliyopita, yasijirudie,” alisema Msama.                                                     

Akizungumzia tishio la vijana kutaka kufanya maandamano mengine Desemba 9, Msama alisema hatua hiyo inapaswa kupingwa na kila Mtanzania aliyeona matukio na hasara ya vurugu za Oktoba 29.

Alisema maandamano hayo hayana tija kwa taifa kwani Rais ameshapatika, tayari ameunda serikali yake, ameunda tume huru ya uchunguzi itakayo kuja na mapendekezo yatakayopelekwa kwenye tume ya maridhiano ili  kuzuia matukio hayo ya Oktoba 29, yasijirudie.

” Nawakumbusha vijana kutambua kwamba uchaguzi umepita na Rais amepatikana, vurugu zozote haziwezi kubadilisha matokeo na hazikubaliki. Tumwache Rais afanyekazi, tuiache tume ifanyekazi yake ili tupate suluhu ya kudumu kuhakikisha Tanzania inaendelea kubaki kuwa kisiwa cha amani na utulivu,” alisema Msama.

Msama pia aliwataka viongozi wa dini kuwa makini na kauli zao kwani zinaweza kuligawa taifa badala yake waongoze ibada na sala za kulionbea taifa.

Kwa mujibu wa Rais Samia, matokeo ya uchunguzi wa tume hiyo iliyopewa miezi mitatu, yatasaidia taifa kuingia kwenye meza ya maridhiano.

 Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa tume hiyo huru ya uchunguzi, Rais Samiq, ameitaka  kuchunguza matukio ya Uvunjifu wa Amani ya Uchaguzi Mkuu wa 2025. 

Alisema tume hiyo inapaswa  kuchunguza kwa kina mchango wa vyama vya siasa, asasi za kiraia (NGOs) za ndani na nje, pamoja na tuhuma za vijana kulipwa fedha kabla ya kuingia mitaani.

Rais Samia ameitaka Tume hiyo kutazama sura nzima ya mgogoro, ikiwemo mitazamo, tamko na hatua za wadau wote.

Amesema madai haya, iwapo ni ya kweli, yana uzito ambao unahitaji kuchunguzwa kwa undani ili taifa lipate majibu sahihi na hatua stahiki zichukuliwe.

Rais amesisitiza kuwa hata kama kulikuwa na changamoto za kisiasa kati ya vyama, Tume ya Uchaguzi, Msajili wa Vyama au Serikali, haipaswi kufikia hatua ya vurugu, uharibifu na vifo.

Rais pia ametaka tume ichunguze kauli zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya makundi wakati wa vurugu, ikiwemo madai ya kutaka Tanzania kufuata mkondo uliotokea Madagascar.

Ends