Moshi. Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillus Wambura amewataka wahitimu wa mafunzo ya jeshi hilo kuepuka utendaji wa mazoea, huku akiwahimiza Watanzania kuimarisha upendo, umoja na mshikamano na kutogawanyika kwa namna yoyote ile ya kisiasa na kidini.
IGP Wambura amewataka wahitimu hao kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi, akieleza kazi ya kulinda raia na mali zao ni jukumu la kipekee duniani linalohitaji uzalendo wa hali ya juu, utii, nidhamu na ujasiri ili kutekelezwa kwa ufanisi.
Amesema hayo leo Novemba 21, 2025 alipofunga mafunzo ya awali katika Shule ya Polisi Tanzania, Moshi mkoani Kilimanjaro. Jumla ya askari 4,782 wamehitimu mafunzo hayo, huku 217 wakishindwa kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwamo utovu wa nidhamu na maadili.
Amewapongeza wakufunzi na mkuu wa shule kwa kuhakikisha askari wanapata mafunzo yanayokidhi vigezo vya ubora unaohitajika kitaifa na kimataifa pia wahitimu kwa juhudi zao katika mafunzo yaliyodumu kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Amesema mafunzo ya uaskari yanahitaji nidhamu na uvumilivu wa hali ya juu katika kutekeleza majukumu ya kulitumikia Taifa.
“Nimesikia kuna baadhi yenu walifukuzwa kwa sababu mbalimbali ikiwemo utovu wa nidhamu, hivyo ninyi ambao mnahitimu leo ni dhahiri mmeonyesha nidhamu ya hali ya juu,” amesema na kuongeza:
“Askari mliohitimu, kazi ya kulinda raia na mali zao popote pale duniani, ina umuhimu wa kipekee, jukumu hili ni zito linalohitaji uzalendo wa hali ya juu, kutii, nidhamu na ujasiri.”
Amewataka kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi na za kimataifa, huku wakijiepusha na utendaji wa kimazoe.
Awali, Mkuu wa Shule ya Polisi Tanzania, Moshi (TPS), Kamishna Ramadhani Mungi, amesema mwaka 2024 walipokea wanafunzi askari 4,999 na mpaka leo Novemba 21, 2025 wamehitimu 4,782 baada ya 217 kufukuzwa kutoka na changamoto mbalimbali zikiwamo za utovu wa nidhamu na maadili na uwezo mdogo wa kujifunza.
Kwa upande wa wananchi, IGP Wambura amesema: “Nitoe rai kwa wananchi kuendelea kuimarisha upendo, umoja na ushirikiano na jeshi letu la Polisi kwa masilahi ya Taifa letu, tusikubali kugawanyika kutokana na sababu zozote zile iwe ya kisiasa, kidini au rasilimali.”
“Tuendelee kutunza tunu yetu ya usalama na amani ya nchi yetu iliyodumu takribani kwa kipindi cha miongo sita sasa tangu tupate uhuru na tushirikiane wote tuhakikishe tunakuwa salama kwa wakati wote,” amesema.
Wakari huohuo, Jeshi la Polisi limetoa tahadhari kuhusu kuongezeka kwa kauli za uchochezi zinazoweza kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu wa Taifa.
Katika taarifa kwa umma, jeshi hilo limesema linafuatilia kwa ukaribu mwenendo wa hali ya usalama nchini na litaendelea kuchukua hatua stahiki dhidi ya mtu yeyote au kundi litakalobainika kukiuka sheria kwa kutoa kauli zenye mwelekeo wa kuchochea vurugu au migawanyiko katika jamii.
Onyo hilo limetolewa wakati ambao kumekuwapo mfululizo wa matamko kutoka kwa baadhi ya makundi na watu binafsi kutokana na vurugu zilizotokea wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, matamko ambayo yameibua mjadala na misimamo tofauti katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika taarifa iliyotolewa leo Ijumaa, Novemba 21, 2025 na Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nchini jijini Dodoma, limeeleza limebaini uwepo wa baadhi ya watu wanaotumia majukwaa mbalimbali ya mawasiliano kutoa kauli ambazo zinaweza kuchochea mgawanyiko na kuathiri mshikamano wa jamii.
Jeshi la Polisi limesema matamshi ya kuendeleza chuki, kuhamasisha migawanyiko au kuibua hisia zinazoweza kusababisha uvunjifu wa amani ni kinyume cha sheria na ni tishio kubwa kwa usalama na utulivu wa nchi.
Vilevile, limesisitiza kuwa halitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mtu yeyote atakayejihusisha na matumizi ya lugha iwe laini au kali yenye viashiria vya uchochezi, likibainisha kuwa hatua hizo ni muhimu katika kudhibiti chuki na kuzuia vurugu ambazo zina madhara makubwa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
“Tutaendelea kufanya kazi kwa umakini ili kuhakikisha amani inaendelea kutawala, hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inahitaji maridhiano ya kitaifa kurejesha utulivu. Ikizuka vurugu, athari zake ni pana na humgusa kila mwananchi katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kiusalama,” imesema taarifa hiyo.
IGP Wambura amewataka askari kushirikiana na jamii, akieleza yapo matukio wanapaswa kushirikiana ili kuzuia, kupambana nayo na kuyatafutia ufumbuzi.
“Napenda niwashirikishe changamoto mtakazokutana nazo kwenye jamii hivi sasa, ikiwemo matishio ya ugaidi, uharamia, dawa za kulevya, usafirishaji haramu wa binadamu pamoja na uhamiaji haramu. Hizo ni baadhi tu ya changamoto za kiusualama mtakazokutana nazo kwenye mikoa muendako,” amesema.
Amewaeleza wanahitaji ushirikiano wa dhati na wa ukaribu kutoka kwa wananachi ili kuzuia na kupambana na makosa hayo.
“Nitoe wito kwa wananachi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi, kutoa taarifa za uhalifu ili tuendelee kuwa salama. Kumbukeni usalama ni nguzo muhimu ya maendeleo katika nyanja zote za maisha ya binadamu na bila usalama hakuna maendeleo yanayopatikana,” amesema.
Vilevile, amewataka askari kulinda afya zao ikiwamo maambukizi ya virusi vya Ukimwi ili kulitumikia Taifa wakiwa na afya njema.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, akitoa salamu za mkoa amesema upo salama na utaendelea kuwa salama wakati wote.