Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Bandari Dar es Salaam, Balozi Ernest Mangu ametoa maagizo matano kwa Chuo cha Bandari na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), yakiwemo kukamilisha uwekezaji katika miundombinu ya kisasa ya kujifunzia na kufundishia.
Lengo ni kuhakikisha chuo hicho kinakuwa kitovu cha umahiri na ubunifu katika sekta ya bandari, na hivyo kutoa wataalamu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya tasnia na kuimarisha ushindani wake kimataifa.
Balozi Mangu, aliyewahi kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), ametoa maagizo muhimu kwa Chuo cha Bandari Dar es Salaam leo Novemba 21, 2025, wakati wa Mahafali ya 24 ya chuo hicho.
Katika mahafali hayo, wahitimu 757 (wanaume 374 na wanawake 384) walitunukiwa vyeti vya ngazi ya stashahada na astashada.
Akihutubia kama mgeni rasmi, Balozi Mangu amesema kuwa ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya kujifunzia na kufundishia lazima ukamilike ndani ya miaka mitatu ijayo, yaani kabla ya mwisho wa mwaka 2028.
Balozi Mangu amesema uwekezaji huo utakuwa nguzo muhimu ya kukifanya chuo hicho kuwa kitovu cha mageuzi ya sekta ya bandari.
Pia, amehimiza juhudi za kupata ardhi katika eneo la Pemba Mnazi, Kigamboni, ili kuweka miundombinu zaidi ya mafunzo na kuimarisha uwezo wa chuo kutoa mafunzo bora na yenye ushindani wa kimataifa.
“Ninaelekeza Menejimenti ya TPA na Chuo kuendeleza jitihada za kupata ardhi katika eneo la Pemba Mnazi, Kigamboni, ili kuiwezesha taasisi kuwekeza katika miundombinu wezeshi ya kufundishia na kupanua huduma zake. Hatua hii itakiwezesha Chuo kuakisi ukuaji wa sekta na kufikia viwango vya kikanda.”
Pia, Balozi Mangu ameeleekeza kuanzishwa kwa Makumbusho ya Bandari ya kidijitali na kisasa itakayohifadhi kumbukumbu, historia, nyaraka na rekodi za maendeleo ya bandari nchini na makumbusho hayo yatakuwa rejea kuu kwa watafiti, wanafunzi na vizazi vijavyo kuhusu safari ya sekta ya bandari ilipotoka, ilipo na inakoelekea.
Agizo lingine, Balozi Mangu ameitaka TPA iharakishe mchakato wa kuhuisha muundo wake ili kuwezesha kuanzishwa kwa Kitengo cha Utafiti na Uendelezaji Biashara.
“Kitengo hicho kitashirikisha wataalamu wa Chuo cha Bandari kufanya tafiti za kiuchumi, uwekezaji, masoko, changamoto za kiforodha na masuala mengine muhimu ili kupunguza vikwazo vinavyoathiri utendaji wa sekta ya uchukuzi na bandari,”amesema.
Balozi Mangu amehitimisha maagizo kwa kutoa wito kwa TPA na Chuo kuendeleza juhudi za kuwawezesha wakufunzi kupata elimu ya juu ndani na nje ya nchi ili kuongeza uwezo wa kufundisha masomo ya kisasa ya uendeshaji wa bandari.
Amesema bila wakufunzi wenye ujuzi wa kiulimwengu, chuo hakiwezi kufikia hadhi ya kuwa eneo la umahiri linalotegemewa na sekta.
Awali, Mkuu wa Chuo hicho, Dk Lufunyo Hussein, amesema taasisi hiyo inaendelea kufanya maboresho makubwa ili kuhakikisha huduma zake zinakidhi ubora wa kitaifa na kimataifa.
Dk Hussein, amesema wanaimarisha mfumo wa taarifa za wanafunzi ili ulingane na mifumo ya taasisi nyingine, na kwamba majadiliano ya ushirikiano na vyuo vya nje ikiwamo Oman na Nigeria yanaendelea ili kubadilishana uzoefu na ujuzi.
Amesema wanazidi kuimarisha ushirikiano na wawekezaji katika bandari mbalimbali nchini, hatua ambayo itawawezesha wanafunzi na wakufunzi kujifunza teknolojia za kisasa zinazotumika katika bandari za kimataifa.
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa katika salamu zake kwenye mahafali hayo amesisistiza kuwa TPA inaendelea kufanya mageuzi makubwa ya kukiboresha Chuo cha Bandari ili kiwe taasisi ya kimataifa inayojengwa juu ya ubora, teknolojia ya kisasa na wataalamu wabobezi.
Mbossa amesema kuwa uwekezaji uliofanywa na TPA ikiwemo ununuzi wa mitambo ya kisasa ya kufundishia yenye thamani ya Sh3.5 bilioni inaonesha dhamira ya dhati ya kuliongezea chuo uwezo wa kutoa mafunzo ya vitendo na ya kiwango cha juu kwa watumishi na wanafunzi.
“TPA tutaendelea kukiboresha Chuo cha Bandari kwa kukipatia miundombinu ya kisasa, vifaa vya kufundishia, mifumo ya Tehama na wataalamu wabobezi ili kiendane na kasi ya mageuzi katika sekta ya bandari,” amesema
