Vijana 35 Watanzania wapata ujuzi kubadili taka kuwa bidhaa, wachekelea

Dar es Salaam. Wakati wewe ukitupa au ukizitazama taka kama chupa za plastiki, vifuu vya nazi, mabaki ya vitambaa au visoda zikiwa barabarani na kuona hazina thamani basi utakuwa unajidanganya.

Mbali na hizo pia karatasi ngumu kama zile za kalenda, vyote jumla zinauwezo wa kubadilishwa na kuwa bidhaa zenye kuvutia kama bangili, mauwa na mapambo mbalimbali ya nyumba na ofisi.

Watu wengi huzitazama taka kwa jicho la uchafu, lakini bila kufahamu taka hizo zinauwezo wa kuwa kitega uchumi ikiwemo kutumiwa na wajasiriamali.

Hayo yanadhihilishwa na vijana 35 wa kitanzania waliopo vyuoni na wengine nje ya mfumo wa elimu ambao wamepata mafunzo ya kuzalisha bidhaa zitokanazo na taka kupitia mradi wa mafunzo wa Uchumi Rejeshi (circular economy) wa Taasisi ya Utu na Mazingira (Hudefo), ulioanza Julai mwaka huu.

Wakizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Novemba 21, 2025 katika hafla ya ufungaji wa mradi huo wameeleza furaha yao kwa kupata ujuzi huo mpya utakao wasaidia katika maisha huku wakiahidi kuwapatia elimu hiyo na wenzao pamoja na jamii kwa ujumla.

Pendo Moffat aliyepata mafunzo katika mradi huo amesema ameweza kutengeneza bangili zitokanazo na vifuu vya nazi na taka za karatasi, pia kutengeneza mikeka ya mezani (table mats) akisema bidhaa hizo zinatumika hotelini na kuvutia watalii.

“Tunaweza kutengeneza vitu vyote hivi kwa kutumia vifaa kama msasa, sindano, gundi na rangi kama kijana ninayo furaha kwani ujuzi ni bora zaidi,” amesema.

Akieleza zaidi Pendo amesema utengenezaji wa bidhaa hizo ni fursa mpya kwa kuwa kuna watu waliopo mtaani hasa kina mama na hawana cha kufanya hivyo watapa elimu hiyo.

Prisca Mlangwa kupitia uchumi rejeshi amesema ameweza kujifunza kutumia taka za plastiki kama chupa kuzibadilisha kutengeneza bidhaa mbalimbali kama mauwa ya urembo.

Amesema kupitia chupa hizo za plastiki kwa sasa wameweza kutengeneza bidhaa hizo zenye kuvutia zinazoweza kuuza ndani hata nje ya nchi.

“Tunaijulisha jamii kwamba kuna vitu visivyofikiriwa kama taka vinaweza kugeuzwa kuwa thamani kwa bajeti ndogo na kisha maisha yakaendelea,” amesema.

Amesema hata mtu wa kawaida anaweza akakusanya taka akatengeneza bidhaa akapeleka kwenye maonesho kama Sabasaba au Nanenane kutangaza kile anachokifanya.

Kwa upande wake, Juma Hassan amesema yeye na kundi lake kati ya makundi manne yaliyogawanywa katika vijana hao 35 wao waliamua kutoa elimu ya ujuzi huo hasa kwa vijana na wanawake.

“Uchumi Rejeshi unamaanisha taka zinatumika kutengeneza bidhaa na si kutupwa kama ilivyozoeleka,” amesema.

Kiongozi wa mradi huo wa Uchumi Rejeshi, Theresia Mushi amesema mradi umefanikiwa kutokana na ushiriki na matarajio waliyoweka.

“Tulikuja na wazo la kuzipa uhai tena taka kama za nguo vitenge, kanga chupa ili kutengeneza bidhaa. Tukatafuta vijana tukawapa mafuzo ambayo mwazo walikuwa wakisoma mtandaoni kisha tukaanza kukutana,” amesema.

Amesema bidhaa zote zilizofundishwa na kutengenezwa zinafika 150 ikiwemo pochi, bangili, mauwa ya plastiki, mikeka ya mezani, vishikiria funguo (key holders) na nyingine nyingi.

“Bidhaa nyingine zimepelekwa kwenye Mkutano wa 30 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) unaofanyika nchini Brazil,” amebainisha.

Amesema mradi huo hauishii kwa vijana hao bali ujuzi huo utapelekwa kwa kina mama na vijana wengine ili watengeneze bidhaa mbalimbali ikiwa ni kusudi la Hudefo.