Wajasiriamali wafichua siri ya tiba kwenye maua

Morogoro. Wajasiriamali wa bidhaa za maua katika Maonesho ya Biashara ya Morogoro wamesema kuwa, licha ya maua kutambulika zaidi kama mapambo ya nyumba, bustani na hoteli, yana pia manufaa makubwa kiafya ambayo sehemu kubwa ya jamii bado haijayafahamu vya kutosha.

Akizungumza na Mwananchi leo, Novemba 21, 2025, mjini hapa, mjasiriamali wa maua na mimea tiba, Neema Katendele, amesema maua yana thamani inayozidi uzuri wake wa nje, kwani baadhi ya aina hutumika kama tiba asilia kwa magonjwa mbalimbali ya binadamu.

Neema amebainisha kuwa maua yanapohifadhiwa na kutunzwa vizuri yana uwezo wa kuboresha ubora wa hewa ndani ya nyumba, kutuliza mazingira, kupunguza mfadhaiko na kuongeza ustawi wa kimwili na kiakili.

Ameongeza kuwa baadhi ya maua husaidia kupunguza au kutibu matatizo kama vidonda vya tumbo, presha ya kupanda na kushuka, matatizo ya masikio, pamoja na kuondoa msongo wa mawazo.

“Maua yana faida nyingi kwa afya ya binadamu. Hasa maua ya msharifu, ‘rosemary’ na mchaichai. Msharifu hutibu vidonda vya tumbo na kisukari, ‘rosemary’ hutibu presha, na mchaichai hutibu uchovu wa mwili,” amesema Neema.

Mjasiriamali mwingine wa maua, Idda Maro, ameeleza kuwa tabia za maua zinatofautiana kulingana na mazingira yao ya ukuaji.

Baadhi hupenda jua muda wote, wengine kivuli au mchanganyiko wa yote mawili, ili kuleta mafanikio ya kipekee.

“Maua huleta nuru, furaha, upendo, na utulivu katika nyumba. Watu wanaoishi katika maeneo yenye maua huiga tabia ya kuvutia na kupata mazingira bora,” amesema Idda.

Naye Meneja wa Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA) Mkoa wa Morogoro, Dustan Mziwanda, amesema kuwa maonesho hayo ni fursa ya kipekee kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wa mkoa huo kuonyesha ubunifu na bidhaa zao.

“Leo tumeanza kugawa mabanda kwa wajasiriamali waliothibitisha kushiriki. Kesho (Novemba 22, 2025) tutakamilisha zoezi la ugawaji mabanda. Wajasiriamali wataanza shughuli zao za kutangaza biashara na kutoa elimu kwa wananchi,” amesema Mziwanda.