MABAO mawili ya nyota wa Namungo, Jacob Masawe dakika ya 75 na Cyprian Kipenye dakika ya 82, yametosha kuipatia ushindi timu hiyo wa 2-0, dhidi ya Dodoma Jiji, katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa leo Novemba 21, 2025 kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.
Katika mechi hiyo, ilishuhudiwa wachezaji waliotokea benchi wakiamua ushindi kwa Namungo, akianza Masawe aliyeingia dakika ya 59, akichukua nafasi ya Lucas Kikoti huku kwa upande wa Kipenye akiingia dakika ya 73, akipishwa na Hashim Manyanya.
Namungo iliyocheza mechi ya saba hadi sasa, huu ni ushindi wa pili kwa kikosi hicho chini ya Kocha, Juma Mgunda, tangu mara ya mwisho ilipoifunga Tanzania Prisons bao 1-0, Septemba 21, 2025, ikitoka sare tatu na kuchapwa mbili.
Kwa upande wa Dodoma Jiji, hiki kinakuwa ni kipigo
cha nne msimu huu hadi sasa katika Ligi Kuu, baada ya kutoka sare mara mbili na kushinda moja tu kwa mabao 2-0, dhidi ya Coastal Union, kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, Septemba 27, 2025.
Mechi ya mwisho kabla ya hii iliyopigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa, timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2, Februari 9, 2025, ambapo Namungo ilifunga kupitia Pius Buswita na Erasto Nyoni, huku ya Dodoma yakifungwa na Paul Peter na Apollo Otieno.
Kipigo cha leo ni mwendelezo mbaya wa Dodoma Jiji katika Ligi Kuu Bara msimu huu, baada ya mechi ya mwisho kupokwa pointi tatu na mabao matatu pia dhidi ya kikosi cha Pamba Jiji, Oktoba 25, 2025, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Sababu za Dodoma kupokwa pointi tatu na mabao matatu ni kutokana na mechi hiyo kushindwa kumalizika na kusimama dakika ya 6, baada ya kutokea kwa hitilafu ya umeme huku, wenyeji Dodoma ikiongoza kwa bao 1-0, lililofungwa na, Benno Ngassa.
Hata hivyo, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi Kuu Bara katika kikao chake cha Oktoba 27, 2025, kilitoa uamuzi wa kuipa Pamba Jiji ushindi wa mabao 3-0 na pointi tatu, kwa kosa la Dodoma Jiji kushindwa kuandaa mechi hiyo kikamilifu.
Sababu ya Dodoma Jiji kupokwa ushindi huo ni kutokana na kutofanya juhudi zozote za kurejesha mwanga kwenye Uwanja wa Jamhuri hivyo, kusababisha mechi hiyo kuvurugika, huku adhabu ikitolewa kwa kuzingatia kanuni ya 32:3 ya Ligi Kuu Bara.
Kutokana na adhabu hiyo na kwa mujibu wa kanuni ya 32:3 ya Ligi Kuu Bara kuhusu kuvuruga mechi, bao la mshambuliaji huyo nyota wa Dodoma Jiji, Benno Ngassa alilolifunga lilifutwa rasmi katika orodha ya mabao yake na ya timu anayoichezea pia.