Petro de Luanda yaipiga mkwara Simba

KOCHA Mkuu wa Petro de Luanda ya Angola raia wa Hispania, Franc Artiga, amesema licha ya kucheza na Simba kwa mara ya kwanza lakini haihofii wakati timu hizo zitakapokutana kesho katika mechi ya kwanza ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Artiga amesema anatambua mechi ya kesho itakuwa ni ngumu kutokana na rekodi za Simba inapocheza nyumbani, Ingawa wao wamekuja kucheza mpira kwa kufurahia zaidi.

“Sio rahisi unapocheza mechi za aina hii hasa kucheza na Simba ambayo ni kweli ina rekodi nzuri ikiwa nyumbani, licha ya yote ila tumekuja kucheza kwa tahadhari lakini kuonyesha mpira pia mzuri,” amesema Artiga.

Aidha, Artiga amesema katika mechi ya kesho atawakosa wachezaji watatu muhimu wa kikosi hicho, japo itakuwa ni nafasi nzuri kwa wengine kuchukua nafasi zao.

“Tutawakosa wachezaji, Pedro Aparicio, Macaiabo na Matheus Costa, ni pigo kwetu kwa sababu unapokuwa katika hatua hii unahitaji kuona nyota wote wakiwa katika hali nzuri ya kiakili na kimwili,” amesema Artiga.

Kwa upande wa nyota wa kikosi hicho, Hugo Marques, amesema licha ya kuona mechi kadhaa za Simba, ila ni ngumu kuzifanyia tathimini kwa sababu hatua hii ni ngumu na tofauti.

“Nawajua baadhi ya wachezaji wa Simba, akiwemo Neo Maema kwa sababu nimecheza naye kule Afrika ya Kusini, ila kwa niaba ya wenzangu sisi tumekuja Tanzania kushindana,” amesema Hugo.

Nyota huyo amesema, licha ya kesho kucheza na Simba kwa mara ya kwanza, ila ni miongoni mwa timu anazozifahamu vizuri hapa Tanzania kutokana na rekodi zake ikiwemo na Yanga.

“Tuna wachezaji wazoefu wa mashindano haya hivyo, kama nilivyosema mwanzo itakuwa ni mechi ngumu lakini tutaonyesha ubora na uzoefu tulionao,” amesema.

Hugo amesema miongoni mwa ubora ambao Simba inao kutokana na baadhi ya mechi walizozifuatilia ni pamoja na mipira ya kutenga (Set Pieces), ingawa wamejipanga ili kuhakikisha wanaanza vyema mashindano hayo makubwa Afrika.

Petro ilifika hatua ya makundi ikianza kwa kuitoa Cercle de Joachim ya Mauritania raundi ya awali kwa jumla ya mabao 6-0, huku raundi ya pili ikakutana na Stade d’ Abidjan ya Ivory Coast na kuiondosha kwa jumla ya mabao 4-0, Hivyo, kufuzu makundi.