KOCHA wa Simba, Selemani Matola na mchezaji wa timu hiyo, Joshua Mutale wamefichua siri itakayowabeba msimu huu katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku malengo makubwa yakiwa ni kufika nusu fainali.
Matola na Mutale wamezungumza hayo jijini Dar es Salaam, wakati timu hiyo ikijiandaa kwa ajili ya mechi ya kwanza ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya Petro de Luanda ya Angola, itakayopigwa kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Akizungumzia maandalizi ya mechi hiyo, Matola amesema licha ya kutowahi kukutana na Petro, lakini ni timu nzuri na yenye rekodi bora katika michuano hii, hivyo, wamejipanga kwa ajili ya changamoto mpya kesho.
“Malengo yetu msimu huu ni kufika nusu fainali lakini haitokuwa rahisi kwa sababu ya ushindani wa timu tulizonazo, naamini silaha yetu muhimu ni kutumia vyema mechi za nyumbani na hiyo ndio njia pekee na bora itakayotubeba kufanikisha hilo,” amesema Matola.
Pia, Matola amesema kuwakosa wachezaji wawili muhimu wa timu hiyo, kipa, Moussa Camara na beki wa kati, Abdulrazack Hamza ambao ni majeruhi ni pigo kubwa kwa kikosi hicho, ingawa maandalizi kiujumla ya timu hiyo yamekamilika na yako vizuri.
“Hatua tuliyofikia hakuna mechi nyepesi, tunawachulia wapinzani wetu kwa uzito mkubwa kwa sababu ni timu yenye rekodi nzuri katika michuano ya Afrika na kila mmoja wetu analijua hilo.”
Kwa upande wake, Mutale amesema wachezaji wako tayari kwa ajili ya mechi ya kesho, kwani malengo ni kuhakikisha wanaanza vyema hatua ya makundi.
“Sisi kama wachezaji tuko tayari kwa hii changamoto nyingine, tutajitoa kwa niaba ya kila aliyekuwa nyuma yetu, hasa mashabiki zetu ambao wamekuwa nasi katika kila hatua,” amesema Mutale.
Simba iliyo kundi D la michuano hiyo, itapambana na Petro de Luanda kesho kuanzia saa 10:00 jioni Kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku timu nyingine zinazounda kundi hilo ni Esperance de Tunis ya Tunisia na Stade Malien ya Mali.
Simba ilifika makundi baada ya kuitoa Gaborone United ya Botswana hatua ya awali kwa jumla ya mabao 2-1, kisha kukutana na Nsingizini Hotspurs ya Eswatini na kuitoa pia kwa jumla ya 3-0.