UHONDO wa Ligi Kuu Bara unaendelea tena leo kwa mechi mbili kupigwa, ambapo TRA United zamani Tabora United itacheza na maafande wa Tanzania Prisons, huku Mashujaa ikiwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma kucheza na Mbeya City.
TRA United itakayokuwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora kuanzia saa 8:00 mchana, inasaka ushindi wa kwanza msimu huu wa Ligi Kuu, baada ya kikosi hicho kulazimishwa sare mechi zote tatu mfululizo ilizocheza.
Timu hiyo ilianza msimu huu kwa sare ya kufungana mabao 2-2 na Dodoma Jiji, kisha suluhu dhidi ya Pamba Jiji na Mashujaa, huku maafande wa Prisons ikishinda mechi mbili na kuchapwa pia miwili kati ya minne iliyocheza hadi sasa.
Mechi ya mwisho iliyopigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ambayo timu hizo zilikutana iliisha kwa suluhu, Septemba 14, 2024 huku ile ya marudiano iliyopigwa jijini Mbeya, Februari 21, 2025, zilitoka sare ya kufungana bao 1-1.
Kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma wenyeji Mashujaa wataikaribisha Mbeya City kuanzia saa 10:15 jioni, huku mechi hiyo ikiwa ni ya kisasi, kwani inakumbukwa ndio iliyoishusha daraja timu hiyo ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Mechi hiyo inasubiriwa kwa hamu kwani itakuwa ya kisasi kwa Mbeya City, kwani msimu wa 2022-2023, ilishushwa daraja hadi Ligi ya Championship kabla ya kurejea tena msimu huu, wakati zilipokutana katika ‘play-offs’ za kuisaka tiketi ya Ligi Kuu.
Katika mechi hiyo, Mashujaa ilishinda kwa jumla ya mabao 4-1 na kupanda Ligi Kuu, huku Mbeya City ikishuka rasmi daraja kabla ya kurejea tena msimu huu, baada ya maafande kushinda mabao 3-1, Juni 19, 2023, kisha tena bao 1-0, Juni 24, 2023.
Kocha wa Mashujaa, Salum Mayanga aliyewahi pia kuifundisha Mbeya City ikiwa Ligi ya Championship, amesema licha ya mechi hiyo kubeba kumbukumbu za kuvutia, itakuwa ni ngumu sana kwa sababu ya ubora wa wapinzani hasa eneo la ushambuliaji.
“Mechi zenye kumbukumbu nzuri au mbaya huwa zinaongeza sana ushindani kwa timu zote hasa zinapokutana, hii pia ni mojawapo kwa sababu zina wachezaji wanaofahamiana, hivyo, tumejipanga vizuri nyumbani kwa changamoto hiyo,” amesema kocha Mayanga.
Kwa upande wa kocha wa Mbeya City, Malale Hamsini, amesema utulivu wa wachezaji wa timu hiyo katika kumalizia nafasi za kufunga ndio changamoto kubwa, japo baada ya mapumziko mafupi amefanyia kazi ili kutengeneza kikosi bora cha ushindani.