Simanjiro. Mjane Sion Mathayo amerejeshewa nyumba iliyokuwa dhamana ya deni la Sh11 milioni baada ya Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Fakii Lulandala kufanikisha kupata fedha za kulipa deni hilo.
Nyumba hiyo iliyorejeshwa kwa mjane Sion Mathayo, mkazi wa kitongoji cha Mkumbi mji mdogo wa Orkesumet iliwekwa rehani na mume wake dereva bodaboda, Mohamed Ally (Mang’ati) aliyeuawa hivi karibuni.
Dereva bodaboda, Mohamed Ally (Mang’ati), ambaye aliweka nyumba yake rehani ili kufidia deni, aliuawa kwa kuteketezwa kwa moto baada ya kumwagiwa petroli na watu wawili akiwa na pikipiki yake mnamo Oktoba 2025.
Alipata majeraha makubwa na alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Lulandala, akizungumza wakati wa kumkabidhi mjane huyo hati ya umiliki wa nyumba jana, amesema kuwa wadau mbalimbali wamejitokeza kuchangia na kulipa deni hilo ili kuhakikisha anaendelea kuishi katika nyumba hiyo pamoja na mtoto wake, kufuatia kuuawa kwa mumewe.
“Mume wake aliweka rehani nyumba yao kwa Sh11 milioni ili alipe deni analodaiwa kisha akachomwa moto na kufa, hivyo nikazungumza na wadau ili tulipe fedha hizo na mjane aendelee kuishi hapo,” amesema Lulandala.
Amesema watu mbalimbali wamechangia fedha hizo hadi kupatikana kwake ikiwemo ofisi yake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki James Ole Millya na wadau wengine wa maendeleo.
“Nawapongeza wote waliochangia kwa namna moja au nyingine kuhakikisha mjane anaendelea kuishi kwenye nyumba yao kwani deni ndilo limesababisha yote kutokea,” amesema Lulandala.
Kwa upande wake mjane huyo, Sion Mathayo amemshukuru mkuu wa wilaya hiyo kwa kufanikisha kulipa deni na kupata nyumba hiyo ambayo mume wake aliiuza ili kufidia deni kabla hajauawa.
“Namshukuru Mungu kwa tukio hili la DC wetu Lulandala kusimamia kupatikana kwa fedha hizo na sisi kuendelea kuishi katika nyumba yetu ambayo marehemu mume wangu aliiuza ili afidie deni alilokuwa anadaiwa,” amesema Sion.
Amesema kwamba, licha ya kumpoteza mume wake aliyeuawa, amepata faraja kuona kuwa yeye na mtoto wake wataendelea kuishi katika nyumba yao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Madereva wa Bodaboda wa mji mdogo wa Orkesumet, Joshua Kishumuu, amesema kitendo cha Mkuu wa Wilaya kurejesha nyumba hiyo kwa mjane ni cha kupongezwa sana.
“Tunamshukuru DC wetu mwalimu Lulandala kwa kusimama kidete kwani nyumba ilishauzwa na mjane angeteseka, ila hivi sasa ataendelea kuishi hapo tofauti na awali kwani alikata tamaa,” amesema Kishumuu.
Mmoja wa wakazi wa Orkesumet, Enot Paul, amesema kuwa ni jambo jema kuona mjane huyo anaendelea kuishi katika nyumba yake, kwani vinginevyo angekumbwa na misukosuko miwili kwa wakati mmoja kupoteza mume wake na pia kukosa makazi.
“Ni tukio zuri la mjane kupata msaada huu kwani mume wake alikuwa dereva bodaboda kisha akauawa na pia akatakiwa kuondoka kwenye nyumba anavyoishi ila sasa amefarijika,” amesema.