Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dodoma, imemhukumu kifungo cha miaka minne jela aliyekuwa askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jonathan Huzi, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua bila kukusudia aliyekuwa mpenzi wake, Veronica Michael.
Huzi alishtakiwa kwa kosa la mauaji ya bila kukusudia kinyume cha kifungu cha 195 na 198 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Jaji Evaristo Longopa, aliyesikiliza shauri hilo alitoa hukumu hiyo Novemba 19, 2025 na nakala yake kupakiwa kwenye mtandao wa mahakama siku hiyo.
Tukio la mauaji lilifanyika Oktoba 10, 2014 katika Mtaa wa Majengo wilayani Manyoni, mkoani Singida.
Ilielezwa mahakamani kuwa mshtakiwa na Veronica walikuwa wapenzi na kwamba usiku wa tukio hilo, Lelo Shio akiwa usingizini alimsikia Veronica akigombana na mpenzi wake huyo.
Ilielezwa Shio alipojaribu kutoka nje kwenda kumwokoa alibaini mlango wake ulikuwa umefungwa kwa nje.
Alipotaka kuufungua alisikika mshitakiwa akisema: “Mimi ndiye nimekufungia mlango hadi nikamilishe kazi yangu ndipo nitakufungulia na ole wako upige kelele sasa…” Baada ya dakika 10 alisikika mshitakiwa akisema: “Nakufungulia mlango utaukuta mzoga wako hapa…”
Shio alieleza mahakama kuwa alipofungua mlango alimuona mshtakiwa akikimbia kutoka eneo hilo na alipofika karibu na eneo la tukio alimuona Veronica akiwa na majeraha mwilini, ikiwemo sehemu za siri, huku ulimi ukiwa nje.
Tukio hilo liliripotiwa Kituo cha Polisi Manyoni na majeruhi alipelekwa Hospitali ya Wilaya Manyoni kwa matibabu ambako Oktoba 21, 2014 alifariki dunia.
Uchunguzi wa kitabibu ulibaini chanzo cha kifo chake ni kutokwa damu nyingi.
Mshtakiwa alikamatwa Oktoba 10, 2023 na alihojiwa na polisi, baadaye akapelekwa kwa mlinzi wa amani ambako kwa maelezo ya onyo alikiri kumuua Veronica.
Alipotiwa hatiani kwa kukiri kuwa na hatia, wakili wa serikali alieleza mshtakiwa hana rekodi za uhalifu za kabla ya tukio hilo, akaomba adhabu kali itolewe kwa sababu ya silaha zilizotumika kuua kwa kumchoma mwathirika wa tukio hilo sehemu mbalimbali za mwili na kusababisha majeraha mengi kifuani, mikononi na sehemu za siri.
Alieleza silaha ya kuua ilielekezwa kwenye maeneo nyeti ya mwili ambayo ni hatarishi, mshtakiwa alishindwa kumhudumia mwathirika wa tukio hilo na badala yake alikimbia, huku akimwacha Veronica akiugulia maumivu kutokana na majeraha aliyoyapata kwa sababu ya ugomvi baina yao.
Aliiomba mahakama kumhukumu adhabu kali ili kutoa hadhari kwa jamii kutojichukulia sheria mkononi.
Kwa upande wake, wakili wa utetezi, aliomba mahakama kumpunguzia mshtakiwa adhabu kwani hana rekodi za uhalifu na hilo lilikua kosa lake la kwanza.
Kifo hicho alisema kilitokea kwa sababu ya mapigano kati yao ambapo utumiaji wa kitu chenye ncha kali kilikuwa katika mapigano bila nia yoyote ya kuua.
Alieleza mshtakiwa alikuwa na ushirikiano na vyombo vya sheria kwani alikiri kosa, hivyo kulinda rasilimali za Serikali.
Alidai mahakamani kuwa mshtakiwa aliyetiwa hatiani anajutia matendo yake kwani alimpoteza mpenzi wake na amepata funzo kwa miaka miwili aliyokaa rumande, anategemewa na wazazi wake wawili, ana watoto watatu wanaohitaji malezi na matunzo.
Sababu nyingine zilikuwa ni kuwa, mshtakiwa amepata shinikizo la chini la damu kwa kumpoteza mpenzi wake na ajira kama askari wa JWTZ alikokuwa akifanya kazi kabla ya tukio hilo na kuhitimisha kwa kuomba mahakama kupunguza adhabu.
Jaji Longopa amesema mahakama imezingatia kwa umakini namna kosa lilifanyika na mazingira yote na kupima kwa kuzingatia uzito baada ya kusikiliza hoja za pande zote.
Amesema ni dhahiri kutokana na taarifa zilizowasilishwa kwamba, kulikuwa na ugomvi kati ya mshtakiwa na Veronica na mshtakiwa alitumia silaha kwa kumchoma na kumjeruhi, majeraha yaliyosababisha kifo chake.
“Katika mazingira ya jambo hilo, pamoja na mazingira yote ya tukio hilo, nimeridhika kwamba mauaji hayo yanachukuliwa kuwa mauaji ya kiwango cha kati katika kiwango cha kuua bila kukusudia. Sababu ya kufikiria kuwa ni mauaji ya katikati yanatokea kwa kutumia silaha mbaya dhidi ya marehemu,” amesema na kuongeza:
“Kuchomwa visu na kusababisha majeraha mengi katika sehemu mbalimbali za mwili zikiwemo maeneo nyeti. Kutokana na hali hiyo, hatua ya kuanzia itakuwa kifungo cha miaka saba jela.”
Baada ya kumpunguzia adhabu, amemhukumu kifungo cha miaka minne jela na kueleza kuwa muda huo utamtosha kujirekebisha.