Wapakistan saba washikiliwa Songwe kwa kukiuka masharti ya viza

Songwe. Idara ya Uhamiaji mkoani Songwe inawashikilia raia saba wa Pakistan kwa tuhuma za kukiuka masharti ya viza walizopewa walipoingia nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Novemba 22, 2025, Kaimu Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Songwe, Mrakibu wa Uhamiaji Rose Magesa, amesema watuhumiwa hao ni miongoni mwa raia tisa wa Pakistan waliokamatwa Novemba 18, 2025, katika msako maalumu uliofanyika mjini Tunduma, Wilaya ya Momba.

Magesa amesema masharti ya viza zao yalielekeza waelekee jijini Dar es Salaam, eneo la Mbweni, kwa ajili ya shughuli za matembezi.

Hata hivyo, waliondoka na kufika mkoani Songwe kwa shughuli ambazo hazikuainishwa katika masharti yao.

Aidha, raia wengine wawili wa Pakistan walikamatwa kwa kosa la kuingia nchini bila vibali halali.

Magesa amewataja waliokiuka masharti ya viza pamoja na namba zao za pasipoti kwenye mabano ni Khizar Hayat (JJ6171151), Muhammad Rehman Rasheed (GU9842383), Muhammad Raza (YB9899821), Araiz Chand (YB9899821), Ahmed Ali (TF1832401), Aqib Javed (GH8676622) na Mubashar Ali (YF796162).

Amesema watuhumiwa hao wanatarajiwa kusafirishwa kwenda Dar es Salaam kwa uchunguzi zaidi mara baada ya mahojiano ya awali kukamilika.

Katika hatua nyingine idara hiyo ilieleza kuwa katika operesheni maalumu iliyofanyika kuanzia Oktoba 29 hadi Novemba 21, 2025 katika maeneo mbalimbali ya mpakani Tunduma ilifanikiwa kunasa wahamiaji wengine haramu 31 wote wakiwa ni kutoka nchini Ethiopia.