Dk Mwinyi: Utaratibu wa kusubiri faili ofisini umepitwa na wakati

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amesema sasa si muda wa watendaji wakuu wa Serikali kukaa ofisini kusubiri kuletewa mafaili, badala yake wawafuate wananchi kutatua changamoto zao huko walipo.

Amesema hayo leo Jumamosi Novemba 22, 2025 baada ya kuwaapisha makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu aliowateua juzi, kwenye hafla iliyofanyika viwanja vya Ikulu, Zanzibar.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano Ikulu, imemnukuu Dk Mwinyi akisema Serikali haitavumilia mtendaji anayeshindwa kwenda maeneo yenye matatizo, kwani imezoeleka mara nyingi watu hukaa ofisini kusubiri mafaili bila ya kutoka nje.

Amesema utaratibu wa kusubiri mafaili ofisini umepitwa na wakati na uongozi wa sasa unahitaji watumishi wenye kasi, ubunifu na utayari wa kuwasikiliza wananchi moja kwa moja.

“Kuna tabia ya watu kukaa ofisini wakisubiri mafaili waletewe, huo si utendaji tunaoutaka katika awamu hii, tunahitaji viongozi wanaotembea, wanaofuatilia na wanaotatua changamoto kwenye maeneo husika,” amesema.

Dk Mwinyi amesema ipo mifano ya matatizo madogo lakini yanakaa muda mrefu bila ya kupatiwa ufumbuzi kutokana na watendaji kukaa ofisini.

“Nadhani itoshe sasa, kwani wananchi wa nchi hii wana matarajio makubwa na sisi. Mimi nitakuwa mmoja katika kuhakikisha yeyote yule ambaye hatekelezi majukumu yake, basi anatupisha kwani lengo letu ni kuona yale tuliyoahidi yanatimia,” amesema.

Amewasisitiza watendaji kutumia nafasi walizopewa kuboresha utoaji huduma kwa umma, sambamba na kuongeza uwajibikaji katika taasisi zao.

Ameahidi kufanya kikao kazi na watendaji wote aliowateua na wale wa zamani, wakiwamo mawaziri kuzungumzia matarajio yake katika utekelezaji wa shughuli za Serikali wanapoanza awamu ya pili ya utendaji wake.

Dk Mwinyi amesema vitendea kazi vikuu kwa awamu ya pili ya Serikali ya awamu ya nane ni vitano, ikiwamo ilani ya CCM ya uchaguzi ya mwaka 2025/2030.

Amesema ni lazima kila mtu aangalie sekta yake inasemaje katika ilani na kupanga mpango kazi wa kuhakikisha inatekelezwa kwa asilimia 100.

Nyenzo ya pili, amesema ni kuisoma hotuba aliyoitoa akizindua Baraza la 11 la Wawakilishi, kwa kuwa kuna maeneo mengi ambayo amezungumza na yote yanataka utekelezaji, zikiwa ni ahadi alizotoa.

Dk Mwinyi amesema ahadi alizotoa kipindi cha kampeni kwa wananchi ni nyenzo ya tatu, akieleza ofisi yake itatoa orodha ya ahadi hizo na kila taasisi na wizara inapaswa kuangalia maono yake kwa madhumuni ya kujipanga na kutekeleza kwa muda mfupi iwezekanavyo.

Nyenzo ya nne ni Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar na ya tano ni Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050, hivyo wakijipanga vizuri katika utekelezaji wa maeneo hayo, hana shaka kwamba watakidhi matakwa ya wananchi ambayo waliyasema sana kipindi cha kampeni.

“Kwangu mimi zile ni ahadi na muungwana akiahidi anatekeleza, hivyo ninyi ndio watendaji na mnatambua majukumu yenu katika wizara na maofisa masuuli katika wizara zenu,” amesema.

Vilevile, amekemea makundi ndani ya wizara akisema kwa uwepo wake kwenye taasisi za umma hawataweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Amewataka kuhakikisha wanayaondoa makundi hayo na kushirikiana kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi.

“Niwatake kama watawala katika wizara hakikisheni mnaondoa makundi, watu wote wanakuwa wamoja na mnafanya kazi waliyotukabidhi wananchi,” amesema.


Pia amesisitiza kuhusu ukusanyaji wa mapato katika wizara zao na kuzingatia matumizi vyema, akieleza bado kuna changamoto ya ukusanyaji hafifu wa mapato na uwepo wa matumizi makubwa ambayo hayana sababu za msingi.

Baadhi ya walioapishwa wameeleza hawatamwangusha Rais, bali wanakwenda kufanya kazi za kuleta matokeo chanya.

“Tunakwenda kufanya kazi kama yalivyo mategemeo ya mheshimiwa Rais, kama ambavyo amesema si muda wa kukaa ofisini, bali ni kwenda kutatua changamoto za wananchi,” amesema Fatma Mabrouk Khamis, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi na Uwekezaji.

Wakati huohuo, Dk Mwinyi amekutana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi, aliyefika Ikulu kujitambulisha leo Novemba 22, 2025.

Dk Mwinyi amempongeza kwa kushika wadhifa huo na kumhakikishia ushirikiano katika utekelezaji wa masuala yanayohusu Muungano.

Amesema mafanikio makubwa yamefikiwa katika kuzipatia ufumbuzi changamoto nyingi zilizokuwepo awali, hivyo juhudi zinapaswa kuendelezwa ili kuimarisha Muungano kwa masilahi ya pande zote mbili.

Dk Nchimbi amempongeza Dk Mwinyi kwa ushindi mkubwa wa kuchaguliwa tena kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Ameeleza matumaini yake ya kuiona Zanzibar ikifanya maendeleo katika miaka mitano ijayo.

Akizungumzia Muungano, ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendeleza dhamira thabiti ya kuufanya Muungano kuwa imara zaidi.