BEKI wa JKT Tanzania, David Bryson ameutaja msimu wa 2025/26 ni dume kutokana na ushindani uliopo, huku akiwatahadharisha wapinzani wao, wanaitaka tano bora ya Ligi Kuu Bara, hivyo watarajie ushindani.
Bryson amesema hayo baada ya kucheza dakika 90 dhidi ya KMC na kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa bao 1-0 na kupata ushindi wa pili ugenini baada ya awali kufanya hivyo dhidi ya Coastal Union.
Akizungumza na Mwanaspoti, Bryson alisema ubora wa Ligi Kuu unaendelea kupanda msimu hadi msimu kutokana na ushindani unaoendelea hasa huu ambao ameutaja kuwa bora na hakuna mteremko.
“Hakuna ubishi ubora wa ligi yetu unaendelea kupaa, uwekezaji mkubwa uliofanywa na wawekezaji kwenye klabu ndiyo chachu ya ushindani uliopo. Hakuna timu ambayo ipo kwa ajili ya kugawa pointi, jasho lako ndiyo litaisaidia timu kupata matokeo,” alisema na kuongeza:
“Sijaanza vizuri msimu, lakini nashuhudia ubora kutoka kwa wapinzani. Nimepata nafasi ya kucheza dakika 90 dhidi ya KMC mchezo haukuwa rahisi licha ya timu hiyo kuwa sehemu ya timu zilizogawa pointi nyingi msimu huu kwa wapinzani, lakini walitupa dakika 90 bora na ngumu.”
Bryson ambaye hakuwa sehemu ya mchezo timu yake ilipochapwa mabao 2-1 kutoka kwa Simba kwenye uwanja wao wa nyumbani, alisema msimu huu ni dume na changamoto ya ushindani inayoonyeshwa ni sehemu ya ubora wa ligi na kujengwa kwa timu bora ya taifa.
“Ubora wa timu zote 16 za ligi unatoa chachu ya ushindani kwa wachezaji binafsi pia kwani kila mchezaji anataka namba ya kucheza kikosi cha kwanza kwa kufanya kilicho bora kila anapopata nafasi hii inatoa picha nzuri kwetu wachezaji pia kukuza ubora wetu ambao utakuwa chachu kwenye timu zetu za taifa.”