Dodoma. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka Watanzania kuongeza umakini wakati ambao inaendelea kuongeza juhudi za kukabiliana na usambazaji wa fedha bandia.
Hilo linasemwa wakati ambao sheria inaweka wazi kuwa mtu atakayekutwa na fedha bandia adhabu yake ni kifungo cha maisha.
Ofisa mwandamizi wa Benki Kuu, Atufigwegwe Mwakabalula amesema kuwa watengenezaji wa fedha bandia wanatumia hivu sasa mbinu za kisasa zaidi hivyo ni muhimu wananchi kutambua alama za utambulisho wa noti halisi.
Hilo linabainishwa wakati aombao takwimu za Hali ya uhalifu na Matukio ya Usalama Barabarani 2024 zinaonyesha kuwapo kwa ongezeko la ukamataji wa noti bandia kwa asilimia 32.4.
Matukio hayo yalitoka 105 mwaka 2023 hadi 139 mwaka 2024 huku kukuwa kwa uelewa wa watu ikitajwa kuwa sababu ya ongezeko ka kuripotiwa kwa matukio hayo.
Mwakabalula ameeleza baadhi ya vipengele vya kiusalama vilivyojumuishwa kwenye noti kuwa ni pamoja na nembo ya maji (watermark) inayobeba sura ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere iliyopo katikati ya noti inayoweza kuonekana noti ikinyanyuliwa.
“Noti pia zinakuwa na alama ya michoro midogo iliyochapishwa pande zote mbili za noti ambayo huungana ipasavyo inapopitishwa kwenye mwanga,” amesema.
“Pia kuna picha fiche (latent image) zinazoonekana noti inapoyumbishwa, huku alama za mguso kwenye pembe zikisaidia watu wenye ulemavu wa kuona kutambua dhamani ya noti.
Alama hizo za mguso katika noti zimewekwa katika mfumo wa mistari midogo ambapo katika noti ya Sh10,000 zimewekwa katika muundo wa ‘V’ zikiwa tatu, Sh5,000 zikiwa mbili.
Afisa huyo wa benki kuu pia fedha za Tanzania zina kiraka cha wino kinachobadilika rangi pamoja na uzi wa kiusalama uliowekwa ndani ya noti na unaoonekana wazi inapoinuliwa kwenye mwanga.
Baadhi ya alama, ikiwemo nyuzi zilizofichwa na viashiria vya thamani, huonekana tu chini ya mwanga wa maalumu wa dhambarau jambo linalofanya iwe vigumu kwa waghushi kuiga.
“Hivi ni viwango vya ulinzi vilivyowekwa kwa makusudi,” amesema.
Kwa mujibu wa kanuni ya adhabu, utengenezaji, umiliki au usambazaji wa fedha bandia umeainishwa chini ya makosa ya kughushi na kuigiza sarafu na adhabu yake ya juu kabisa ni kifungo cha maisha.
Mamlaka zinachukulia kosa hilo kuwa tishio kwa uthabiti wa uchumi, kwani linapunguza imani katika mfumo wa fedha na kupotosha miamala ya soko.
Mwakabalula amewasihi wananchi kukagua noti kwa makini, hususan wakati wa miamala ya haraka kwenye masoko, vituo vya usafiri na katika biashara za usiku ambako mara nyingi fedha bandia hupenya kirahisi.
Aliwahimiza pia wananchi kuripoti noti zinazotia shaka katika taasisi za fedha au polisi, akisisitiza kuwa mwananchi aliyeelimika ndiyo ngao imara zaidi. BoT imesisitiza kuwa kulinda sarafu ya nchi ni jukumu la pamoja.