Watoto njiti 315 wapatiwa huduma maalumu Shinyanga

Shinyanga. Wastani wa watoto 30 wanaozaliwa kila mwezi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga ni watoto waliozaliwa kabla ya wiki 37 za ujauzito, jambo linaloonyesha ukubwa wa changamoto hii katika jamii.

Hayo yameelezwa na Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk John Luzila, Novemba 22, 2025, wakati wa kuadhimisha Siku ya Watoto Njiti (Pre-mature Babies).

Dk Luzila alisema kuwa kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka huu, watoto 315 waliozaliwa kabla ya muda wameshapatiwa huduma.

Pia, amebainisha kuwa maboresho makubwa ya huduma za watoto wachanga yamewezesha hospitali kuokoa maisha ya watoto waliozaliwa wakiwa na uzito mdogo kati ya gramu 600, 800 hadi 900, hali ambayo miaka ya nyuma ilikuwa nadra kutokea.

“Hatua hii ni ushindi mkubwa unaotokana na juhudi za watumishi, wazazi na uwekezaji wa Serikali katika huduma za watoto wachanga na inaendelea kushughulikia changamoto zilizopo ikiwemo upatikanaji wa vifaa muhimu vya watoto njiti na ukamilishaji wa majengo muhimu ya hospitali,” amesema Dk Luzila.

Amesema zamani  mtoto akizaliwa chini ya kilo 1.5 uwezekano wa kuishi ulikuwa mdogo, lakini kwa sasa  watoto wa gramu 600 na 800 wanakuwa na kuendelea vizuri kutokana na miundombinu kuboreshwa kwa kuwa na mazingira mazuri.

Dk Luzila amebainisha kuwa, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kati ya wanawake 10 wanaojifungua, mmoja hujifungua mtoto aliyezaliwa kabla ya umri, hivyo kuhitaji huduma maalum na ufuatiliaji wa karibu.

Kwa upande wake, Dk Martha Munuo kutoka Idara ya Watoto na Afya ya Uzazi, ameweka bayana mafanikio makubwa ya Hospitali ya Rufaa Shinyanga.

Mafanikio hayo ni pamoja na uokoaji wa watoto wenye uzito wa gramu 600 hadi 900 kupitia huduma za NICU, ushirikiano wa wazazi waliokubali kufanya Kangaroo Mother Care, pamoja na ushirikiano wa wadau wa afya.

Baadhi ya wazazi, akiwemo Sophia Juma mkazi wa Old Shinyanga, wametoa shukrani kwa madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kwa kuokoa maisha ya watoto njiti.

Wamepongeza huduma waliyopewa, zikisema ni ya kiwango cha juu na yenye huruma.