Wahitimu wa udaktari watakiwa kuacha kukimbilia siasa

Mwanza. Wahitimu wa fani za afya wametakiwa kuacha tabia ya kukimbilia siasa mara baada ya kuhitimu, na badala yake wajikite katika kuitumikia jamii kwa moyo wa huruma, uadilifu, na maadili ya taaluma yao.

Wito huo umetolewa leo, Jumamosi Novemba 22, 2025, na Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Katoliki cha Afya na Sayansi Shirikishi (CUHAS), Severine Niwemugizi, wakati akihutubia mahafali ya 18 ya chuo hicho.

Askofu Niwemugizi amesema kuwa jamii inakabiliwa na changamoto nyingi, hususan katika sekta ya afya, hivyo wahitimu wa udaktari, uuguzi, na taaluma nyingine za tiba wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto hizo, badala ya kutafuta madaraka ya kisiasa.

“Nyinyi madaktari acheni kukimbia kwenda kwenye siasa kutafuta vyeo vya kisiasa… tafadhali tibu wagonjwa. Hayo mambo mengine huko waachie wengine.

“Mkifanya hivyo mtaacha kumbukumbu nzuri na thawabu yenu kwa Mungu itakuwa kubwa,” amesema Askofu Niwemugizi.

Amesema maarifa na ujuzi walioupata chuoni unapaswa kujengwa juu ya utu, huruma na upendo kwa wagonjwa bila kujali matabaka yao.

“Nendeni mkawatue mizigo ya afya mbaya za kiroho na kimwili kwa wote watakaokuja kwenu. Mjue mnamuwakilisha Mungu… mnamuwakilisha Kristo katika kuwatua hiyo mizigo,” amesisitiza.

Askofu Niwemugizi pia ametoa pongezi kwa wataalamu wa CUHAS walioshinda tuzo za kimataifa mwaka huu, akiwemo Profesa Humphrey Mazigo aliyepokea tuzo ya Tumaini Corrah kupitia Africa Research Excellence Fund.

Wengine ni Dk Haruna Dika aliyepata tuzo ya  International Career Achievement Award kutoka Chuo Kikuu cha Calgary, Canada pamoja na Profesa Rose Laisser aliyepokea tuzo kutoka National Institute for Health and Care Research (NIHR)  ya Uingereza.


Awali, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Erasmus Kamugisha amesema jumla ya wahitimu 886 wametunukiwa stashahada na shahada mbalimbali mwaka huu, ambapo asilimia 50.1 ni wanawake na 49.9 ni wanaume.

Katika mahafali hayo, CUHAS imetoa kwa mara ya kwanza wahitimu wa Shahada ya Uzamili katika Sayansi za Epidemiolojia na Takwimu za Kibaiolojia (Master of Science in Epidemiology and Biostatistics).

Profesa Kamugisha amesema wahadhiri wa CUHAS wameendelea kufanya tafiti zenye matokeo ya moja kwa moja katika kuboresha huduma za afya nchini, ambapo kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka huu wamechapisha machapisho 122 ya kisayansi ndani na nje ya nchi.

Amesema chuo hicho, kwa kushirikiana na Hospitali ya Bugando na Hospitali ya Taifa Muhimbili, imefanikiwa kuweka mikakati mahsusi ya kuboresha utambuzi na matibabu ya ugonjwa wa Kiharusi (Stroke) kupitia uboreshaji wa utunzaji kumbukumbu, mafunzo kwa watoa huduma na kutengeneza mwongozo wa matibabu.

“Mafanikio haya yametengeneza msingi mzuri wa protokali za utambuzi na matibabu ya kiharusi kwa nchi nzima,” amesema.

Katika mahafali hayo wahitimu 886 wametunukiwa stashahada na shahada mbalimbali wakiwemo wanawake watano kati yao waliotunukiwa Shahada ya Daktari wa Falsafa (PhD) na Askofu wa Jimbo la Kigoma, Joseph Mlola aliyemuwakilisha Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Mkuu wa chuo hicho.