Tanga/Pemba. Kutoka Maziwe, Pangani mkoani Tanga hadi Panza, kisiwani Pemba, Zanzibar, simulizi ni moja ya namna mawimbi ya bahari yanayoongezeka mwaka hadi mwaka, yanavyoathiri historia na maisha ya kila siku ya wananchi.
Kwa Juma Idd Hassan, maarufu Fundi Ten, mkazi wa Kisiwa cha Maziwe, hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa kudhibiti hali hii inayochangiwa na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa wengi, akiwamo Fundi Ten, suluhu ya haraka ni ujenzi wa kuta za kuzuia maji, kupanda mikoko na kudhibiti ukataji wa miti.
Haji Ali Shaame, Sheha wa Kisiwa Panza anasema awali kisiwa hicho kilikuwa na mandhari nzuri ya miti kama mivinje na mikoko na fukwe zenye mawe mazuri ya asili.
“Lakini kutokana na mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira unaofanywa na binadamu, ikiwamo uchimbaji wa mchanga na mawe, mandhari yake imepotea,” anasema.
Haji anaeleza kuwa bahari imeendelea kusogea na hata kutishia mashamba ya watu.
“Serikali ilijenga ukuta kuzuia maji ya chumvi yasiyavamie mashamba. Wakulima wapatao 60 walikosa sehemu ya kulima, lakini tunatarajia kuanza tena shughuli mwaka huu baada ya ukuta kukamilika,” anasema.
Anasema Oktoba, 2025 walipata mradi kutoka Shirika la Umoja wa mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) kupitia Wizara ya Elimu, ambao ofisi ya sheha, shule za msingi na sekondari zilishirikiana kupanda miti takribani 10,000.
“Tunapaswa kuendeleza juhudi hizi. Miti ikipandwa bila kulindwa ni kazi bure,” anasema.
Anaeleza kuwa mabadiliko haya yameathiri hata makaburi ya watu.
“Makaburi ya Madauni yanafukuliwa kutokana na kujaa maji, mifupa huibuka juu, inabidi izikwe tena sehemu za juu. Lakini muda si mrefu maji yatafika huko pia,” anasema.
Anaeleza kuwa daraja lililounganisha Panza na Mtondooni, lililojengwa mwaka 1975 sasa limezidiwa na maji.
“Daraja hilo hutumika na wanafunzi kwenda shule, lakini maji yakija hujaa na kuziba matobo ya kuyapitisha. Hali imekuwa hatarishi,” anasema.
Anaonya kuwa kisiwa kinaendelea kupungua.
“Maeneo tuliyokuwa tukilima yamechukuliwa na bahari. Mtoakae na Maduwini yamegeuka bahari kabisa. Hata eneo la bandari lililokuwa uwanja wa michezo sasa nusu yake ni baharini,” anasema.
Tafiti, sheria zinasemaje?
Haji anasema kukosekana kwa sheria madhubuti za kuwajibishana kunachangia uharibifu wa mazingira kuendelea.
“Kungekuwa na sheria za kusimamia haya mambo ingekuwa rahisi. Sasa mtu akiharibu unamwonya, anakujibu vibaya au unamuonea muhali. Sheria zikiwepo, zitachukua mkondo wake,” anasema.
Anasema elimu ina umuhimu, lakini lazima iende sambamba na utekelezaji wa sheria.
“Tuendelee kutoa elimu, lakini wasipozingatia, sheria zichukue mkondo wake,” anasema.
Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa Zanzibar wenye jina: “Economics of Climate Change in Zanzibar” umebainisha athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi katika visiwa hivyo na kuonyesha njia za kukabiliana nazo.
Kwa mujibu wa utafiti huo, uchumi wa Zanzibar unategemea sana hali ya hewa, hasa katika sekta za kilimo, uvuvi na utalii.
Visiwa hivi vimeanza kushuhudia ongezeko la joto, mabadiliko ya mtiririko wa mvua, upepo mkali na kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari.
Hali hii imeathiri uzalishaji, kipato na shughuli za kiuchumi, ikionyesha kuwa Zanzibar bado haijajiandaa kikamilifu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Ingawa Zanzibar imeweka mikakati ya maendeleo kupitia Mpango wa Utekelezaji wa Mkuza II, mpango huo haujajumuisha kikamilifu athari za tabianchi katika miradi ya maendeleo.
Ripoti ya awali imeonyesha hatari kubwa za kiuchumi endapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
Utafiti unaonya kuwa bila mikakati madhubuti, sekta muhimu kama utalii, kilimo, nishati, afya, maji na miundombinu ziko hatarini, jambo linaloweza kuzuia jitihada za kufikia uchumi wa kati.
Hata hivyo, zipo fursa za kuchukua hatua za haraka kama uwekezaji katika nishati mbadala, usimamizi endelevu wa ardhi na ujenzi wa miundombinu rafiki kwa mazingira.
Changamoto kubwa ni upungufu wa fedha na uwezo wa kitaasisi. Hivyo, Zanzibar inahitaji kuimarisha ushirikiano wa kimataifa ili kupata fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kujenga uwezo wa ndani.
Hali hii haipo Zanzibar pekee. Tanzania kwa ujumla inakabiliwa na changamoto kama hizo, hasa katika visiwa vya Bahari ya Hindi na Ziwa Victoria, ambako ongezeko la maji limeanza kuteketeza maeneo ya makazi kutokana na kutotekelezwa kwa sheria za mazingira.
Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, Serikali ina wajibu wa kulinda maeneo nyeti kama visiwa na ukanda wa pwani.
Pia, Sheria ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1982 inazitaka mamlaka za wilaya kushirikiana na jamii katika mikakati ya kuzuia maafa ya kimazingira.
Kutotekelezwa kwa sheria hizi kumesababisha visiwa vingi kuharibika na vingine kutoweka kabisa, hali inayohatarisha urithi wa Taifa na maisha ya wananchi wanaotegemea bahari kwa kipato.
Hivyo, Mkaguzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (Zema), Sheha Mjaja Juma, anasema ipo haja ya kuweka uwajibikaji wa kisheria kwa taasisi na viongozi wanaoshindwa kutekeleza wajibu wao wa kulinda mazingira.
Mkurugenzi wa Idara ya Uhifadhi Zanzibar, Dk Makame Omary Makame, anathibitisha kuwa ongezeko la joto duniani linaongeza kina cha maji ya bahari, jambo linalotishia uhai wa visiwa vidogo vilivyoko katika maeneo ya pwani.
Kwa upande wa wataalamu, tatizo hili ni sehemu ya mfululizo mpana wa mabadiliko ya tabianchi duniani.
Mtaalamu na Mabadiliko ya Tabianchi, Paul Kyando anasema kuongezeka kwa joto duniani kumesababisha kuyeyuka kwa barafu iliyoganda kwa muda mrefu (glacial) na kuongezeka kwa kina cha maji yanapopata joto.
“Haya yanasababisha kuongezeka kwa kina cha bahari kwenye maeneo ya nchi kavu,” anasema.
Kyando anasema suluhu ya haya ni kutumia njia za asili kama upandaji wa miti, ikiwamo mikoko na majani bahari ambayo hayategemei ukataji miti kwenye maeneo yaliyoathirika na yale yaliyo hatarini kuathirika.
“Tafiti lazima zifanywe mapema kubaini maeneo yaliyo kwenye hatari na kuhakikisha hatua zinachukuwa mapema,” anashauri.
Ili kufanikisha hayo, Munda Amri, mtaalamu wa mazingira anashauri kujiandaa kwa ujenzi wa miundombinu imara kwenye fukwe kama ukanda mpana wa mchanga (beach nourishment) na ujenzi wa mabwawa ya kujikinga na mafuriko.
“Lazima kuwe na mipango bora ya matumizi ya ardhi na tafiti zitakazobaini mapema na kuhamisha jamii zilizo kwenye hatari ya majanga haya,” anasema.
Anasema mipango ya matumizi ya ardhi ijumuishe maeneo ya hifadhi ya pwani na miongozo inayozuia ujenzi ndani ya eneo la hatari.
Anashauri badala ya kusubiri maafa, uhamishaji ulioandaliwa mapema utasaidia watu kupata ardhi salama bila kupoteza utu au mali zao.
Imeandikwa kwa udhamni wa Taasisi ya Gates Foundation.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.