Siku saba za presha umeya, uenyekiti wa halmashauri

Dar es Salaam. Joto la uteuzi wa kuwania umeya wa majiji, manispaa na wenyeviti wa halmashauri limehamia ngazi ya kamati za siasa za mikoa, zitakazochuja na kupendekeza majina ya wagombea hao kwa ngazi ya kitaifa.

Hatua hiyo ni baada kamati za siasa za wilaya za Chama cha Mapinduzi (CCM) zilizoketi leo Jumamosi Novemba 22 nchi nzima kumaliza kazi kuyachakata majina ya wagombea na kuyapeleka ngazi ya mkoa itakayoketi kesho.

Kabla ya kuanza kwa vikao vya kamati za siasa za wilaya, vilitanguliwa na vikao vya sekretarieti za halmashauri kuu za wilaya vilivyojadili pia majina ya wagombea hao watakaopeperusha bendera ya CCM.

Kesho wajumbe wa kamati za siasa mikoa ambao nao watafanya kazi ile ile ya kuchambua na kupendekeza majina matatu ya waliochukua fomu kwa vikao vya juu.

Ni siku saba za presha na matumbo joto kwa wagombea wanaosaka umeya, unaibu, uenyekiti na umakamu uenyekiti wa halmashauri za wilaya mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa ratiba ya mchakato huo, ambayo Mwananchi imeipata, kwa upande wa Zanzibar, mchujo wa majina ya wagombea utaanza katika sekretarieti ya Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar.

Kikao cha Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar kimepangwa kufanyika Novemba 25, ambapo kitakamilisha mapendekezo yake ya majina ya wagombea waliyochukua fomu.

Kati ya Novemba 27 na 28, Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM itaketi jijini Dodoma kufanya uchambuzi wa majina ya wagombea kutoka nchi nzima.

Baada ya hapo, Kamati Kuu itakutana Novemba 29 kufanya uteuzi wa wagombea kati ya majina yaliyopewa mapendekezo.

Aidha, baada ya uteuzi huo, Novemba 30, vitafanyika vikao vya kamati za madiwani wa CCM katika halmashauri za miji na wilaya ili kuthibitisha wagombea waliopitishwa.

Hadi jioni leo Jumamosi, ukimya umetawala katika ofisi mbalimbali za CCM za wilaya, ambapo wajumbe wa kamati ya siasa ya chama hicho walijifungia kujadili majina hayo.

Mwananchi limezungumza na Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Stanley Mkandawile, ambaye amesema mchakato wa vikao vya kamati za siasa za wilaya unaendelea kwa utulivu na hakuna malalamiko yoyote yaliyojitokeza.

“Tunakwenda vizuri, sijapokea malalamiko yoyote hadi sasa. Wakimaliza wataleta ofisini kwangu bado sijaletewa malalamiko kutoka kwa wagombea,” amesema Mkandawile.

Wagombea 67 wajitokeza Dar

Mkandawile amesema Mkoa wa Dar es Salaam, wenye manispaa tano umetoa madiani 67 wa CCM waliochukua na kurejesha fomu za kuwania umeya katika halmashauri hizo.

“Jiji la Dar es Salaam wanaotaka umeya wapo 12 unaibu 10; Ubungo meya tisa, unaibu watano; Kinondoni wapo meya saba na manaibu watano. Kigamboni waliochukua fomu wapo wanne, naibu mmoja, wakati Temeke wapo tisa na manaibu watano,” amesema Mkandawile.

Baadhi ya wagombea waliozungumza na Mwananchi kwa sharti ya kutotaja majina yao wamesema wapo katika hali ya presha.

“Hadi sasa hivi sijui kinachoendelea na uwezekano mdogo wa kujua kama nimependekezwa au sijapendekezwa, maana haya mambo yanakwenda kwa usiri mkubwa si unajua hiki chama dola?” alisema mmoja wa wagombea wa umeya.

Mgombea mwingine amesema “hadi sasa sijui, maana nasikia wilayani kwangu wamechelewa kuanza. Ni ngumu kujua kinachoendelea maana ni vikao vya wakubwa, hatuthubutu kupeleka pua kunusa kinachoendele,” amesema.